Majanga!! MAHINDI YA WANAFUNZI YACHAKACHULIWA KATA YA NDEMBEZI
Tuesday, January 21, 2014
Aliyesimama ni diwani wa kata ya Ndembezi pia naibu meya wa manispaa ya Shinyanga David Nkulila akiwa amepigwa bumbuazi baada ya kuangalia mahindi ndani ya gari lake ambayo yalionekana kuwa pungufu kiujazo baada ya kutolewa katika ofisi ya afisa mtendaji wa kata ya Ndembezi mjini Shinyanga mapema leo tayari kwa ajili kusambaza katika shule tatu za msingi katika kata hiyo. Diwani huyo amesema kata ya Ndembezi hivi karibuni ilipata magunia
197 ya mahindi ya msaada kutoka ofisi ya waziri mkuu kitengo cha maafa yagawiwe kwa vijiji 19 vya kata hiyo kwa
ajili ya kupunguza makali ya njaa.Katika
magunia hayo 197,yeye binafsi kama diwani wa kata hiyo aliamua kununua magunia
11 kwa ajili ya kusaidia wanafunzi wanaosoma katika shule ya Msingi Bugoyi A na
B pamoja na shule ya msingi Ndembezi ili mahindi yatumike kwa ajili ya uji
wawapo shuleni huku magunia mengine yakigawiwa kwa wakazi wa kata hiyo.
Magunia hayo yakishushwa katika shule ya Bugoyi A.Pamoja na juhudi za kusaidia wanafunzi hao lakini magunia hayo yalionekana kuwa na dosari kutokana na magunia hayo kuwa na ujazo usiotakiwa. Hiki ndicho alichosema Diwani huyo.....
“Lengo lilikuwa ni kutaka wanafunzi wetu wapate uji bila
ubaguzi, lakini pia kuwahamasisha wazazi kuchangia suala la uji kwa watoto wao,
nikawashirikisha wenyeviti wa vijiji wakakubaliana na wazo langu, ,nikanunua magunia
11 kwa pesa zangu,kila gunia likigharimu shilingi elfu tano lakini nashangaa
kuona magunia haya yakiwa hayana ujazo unaotakiwa,yako pungufu”,alieleza Diwani
huyo.
“Katika shule hizi
kuna baadhi ya wanafunzi hawana uwezo wakulipia uji ,sikuwa na nia mbaya,kwa ubunifu wangu nikaona
mahindi haya ya msaada mbali na
kuwasaidia wanakijiji lakini pia yawasaidie wanafunzi wetu ,kwa shule ya Bugoyi A,magunia matatu,Bugoyi B magunia matatu na Ndembezi magunia matano",aliongeza
Ni katika shule ya Msingi Bugoyi A baada ya mahindi kuwekwa kwenye mifuko huo ndiyo mwonekano halisi wa magunia hayo.Akizungumzia kuhusu dosari ya mahindi hayo,Afisa mtendaji wa
kata ya Ndembezi James Dogani aliyekuwa anasimamia zoezi zima la kugawa mahindi katika kata
hiyo alisema suala la upungufu wa mahindi katika magunia linatokana na wananchi
kujichagulia magunia na kwamba kuna mahindi yalimwagika mwagika wakati wa zoezi
la kugawa mahindi hayo.
Afisa
kilimo wa manispaa ya Shinyanga Jeremiah Inegeja alipohojiwa na waandishi wa
habari kuhusu dosari katikak magunia hayo ya mahindi alisema hakuna upungufu
wowote na kwamba tumwulize afisa mtendaji wa kata pengine ndiyo anajua upungufu
umetokana na nini.
Kwa upande wake mwalimu mkuu wa shule ya msingi Bugoyi B
Anord Rweshabura alishukuru kupokea mahindi hayo na kuongeza kuwa hataruhusu
mahindi hayo yatumike hadi pale yatakapoletwa mahindi mengine kujazia magunia hayo kwani sasa hivi yako pungufu.
Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Social Plugin