Mtu mmoja aliyejulikana kwa jina la Mihayo Mhuri (12) Mkazi wa Center Maria Kata ya Kakese Wilaya ya Mpanda Mkoa wa Katavi amefariki dunia baada ya kuzama kwenye maji ya mto wakati akiwa akiogelea kwenye maji akichunga ng’ombe.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi Dhahiri Kidavashari tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa tano na nusu asubuhi katika mto wa Katuma Wilayani Mpanda.
Siku hiyo ya tukio marehemu akiwa na mdogo wake aitwaye Wakasoro Nhuri 7 waliondoka nyumbani kwao na kuelekea kuchunga ng’ombe katika maeneo ya Karibu na mto Katuma.
Wakiwa maeneo hayo marehemu alipatwa na jasho na ndipo alipoamua kuvua nguo na kuingia ndani ya mto Katuma kwa ajili ya kuogelea na kumwacha mdogo wake akiwa kando ya Mto.
Kamanda Kidavashari alisema wakati marehemu akiendelea kuoga alizidiwa na maji na kuanza kuzama chini ya maji ya mto huo kitendo ambacho kilimshitua mdogo wake ambae alikuwa kando ya mto huo.
Mdogo wake alianza kupiga kelele za kuomba msaada kwa watu huku akilia na watu walikusanyika katika eneo hilo na mdogo wa marehemu aliwaeleza kuwa kaka yake amezama kwenye maji ya mto huo wa Katuma.
Kidavashari alieleza watu hao walianza jitihada za kumtafuta marehemu baada ya kitambo kidogo waliweza kuupata mwili wa marehemu ukiwa umekwama kwenye Gogo pembeni ya mto huku akiwa ameshafariki dunia.
Na Walter M guluchuma
Katavi yetu blog
Social Plugin