mwanamme mmoja ameuawa kwa kupigwa na mpini wa jembe na mtu mmoja aliyejulikana kwa jina moja la Majaliwa kutokana na kile kilichotajwa marehemu kudaiwa shilingi elfu 3 katika kijiji cha Ibelansuha kata ya Ushetu tarafa ya Dakama wilayani Kahama mkoani Shinyanga.
Tukio hilo limetokea juzi majira ya saa mbili asubuhi katika kijiji hicho cha Ibelansuha.
Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga SACP Evarist Mangala amemtaja aliyeuawa kuwa ni bwana Magulu Mhangwa (35) mkazi wa kijiji hicho ambaye aliuawa kwa kupigwa na mpini wa jembe sehemu za ubavuni na mtu mmoja aliyejulikana kwa jina moja la Majaliwa.
Amesema chanzo cha tukio hilo ni kutokana na marehemu kumdai mtuhumiwa wa mauaji hayo kiasi cha shilingi elfu tatu alizokuwa anamdai.
Aidha kufuatia kudaiwa pesa hizo mtuhumiwa alikasirika na kuamua kumpiga kwa mpini wa jembe na kusababisha kifo chake papo hapo huku mtuhumiwa akifanikiwa kukimbia.
Kamanda Mangala amesema jeshi la polisi linaendelea kufanya msako mkali wa kumtafuta na kumkamata mtuhumiwa wa mauaji huku akiwaomba wananchi kutoa taarifa zitakazosaidia kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo.
Social Plugin