Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAFANYABIASHARA WAUMANA NA MANISPAA YA SHINYANGA SAKATA LA KUPANGA KWA ZABUNI,WAFUNGA MADUKA YAO SIKU NZIMA,BARAZA LA ARDHI NA NYUMBA LATOA ZUIO KWA MANISPAA KUPANGISHA VIBANDA KWA NJIA YA ZABUNI

Maduka yakiwa yamefungwa hapo jana na wafanyabiashara katika eneo hilo la soko kuu mjini Shinyanga waliamua kufunga vibanda vyao na kwenda katika baraza la ardhi na nyumba hali ambayo iliwafanya wananchi kukosa huduma muhimu siku nzima katika soko hilo
Baraza la ardhi na nyumba wilaya  ya Shinyanga limesitisha kusudio la halmashauri ya manispaa ya Shinyanga kutaka kugawa vibanda vya biashara  katika eneo la Soko kuu mjini Shinyanga kwa njia ya zabuni mpaka pale kesi ya msingi iliyofunguliwa na wafanyabiashara wanaomiliki vib anda hivyo hivi sasa itakaposikilizwa.

Akitangaza uamuzi wa kusitisha utaratibu huo,JANA mwenyekiti wa Baraza hilo la Ardhi na nyumba, Emmanuel Sululu alisema baada ya kusikiliza maelezo yaliyotolewa na upan de wa walalamikaji  amekubaliana na maombi yao ya kusitishwa kufunguliwa kwa zabuni kazi ambayo ingekuwa ifanyike Januari 13, mwaka huu.

Sululu alisema baada ya kusikiliza kwa kina maelezo ya walalamikaji  yaliyotolewa katika baraza hilo na mwakilishi wao kampuni ya uwakili ya Beda amekubaliana na ombi  hilo baada ya kubaini kwamba yapo mambo ya msingi yaliyopaswa kusikilizwa kabla ya hatua ya kufunguliwa kwa zabuni iliyotangazwa na mkurugenzi wa manispaa ya Shinyanga.
“Nimeamua kutoa zuio la tenda iliyotangazwa na manispaa kuhusu utaratibu wa kugawa vibanda katika eneo la soko kuu kwa njia ya tenda baada ya kusikiliza sababu zilizotolewa na walalamikaji mpaka pale kesi ya msingi itakaposikilizwa tarehe 27 mwezi Januari 2014”,alisema  Sululu.
Awali akizungumzia sababu za kuweka kuzio wakili wa upande wa walalamikaji Norbert Bedder alisema miongoni mwa sababu hizo ni kutokana na wadau wa soko kuu kutoshrikishwa katika mchakato mzima wa zabuni namba LGA/112/2013/2014/NC/03 iliyotangazwa na halmashauri ya manispaa ya Shinyanga kwa wafanyabiashara wa eneo la soko kuu.

Aliitaja sababu nyingine kuwa ni wadau wa soko hilo kupinga kushindanishwa kununua vibanda vya biashara kwa zabuni na mwenye zabuni nyingi kuwa na uwezo wa kumiliki vibanda vingi hali ambayo itawanyima fursa wafanyabiashara wa hali ya chini kukosa maeneo ya kuendeshea biashara zao.

“Lakini pia sababu nyingine ni kwamba lengo la serikali ni kutoa huduma kwa wananchi siyo kufanya biashara kama inavyofanya manispaa ya Shinyanga”,aliongeza wakili huyo.

Akizungumza katika baraza hilo kwa niaba ya mkurugenzi wa manipaa ya Shinyanga Festo Kang’ombe,afisa utumishi wa manispaa hiyo Boniface Maheri alisema msimamo wa manispaa bado upo pale pale kugawa vibanda hivyo kwa njiaya zabuni.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutolewa maamuzi ya zuio la kugawa vibanda kwa njia ya zabuni mwenyekiti wa wafanyabiashara hao Erick Njau wao hawakubaliani na maombi hayo ya manispaa ya Shinyanga kwani wana zaidi ya miaka 30 wakifanya biashara katika eneo hilo la soko kuu huku wakilipa kodi ya kila kibanda shilingi elfu 30 kila mwezi na sasa wanapaswa kulipa shilingi elfu 30 kuomba tenda na fedha hiyo hairudishi hata kama umekosa zabuni hiyo.
“Hapa soko kuu kuna vibanda 149,kwa kweli tumeshangazwa sana na tangazo la ghafla la manispaa  yetu,hivi inakuwaje tayari mtu ni mpangaji halafu unatangaziwa kuomba tena kibanda wakati tayari unakitumia,huu ni uonevu mkubwa kwa watu maskini,matajiri ndiyo watafaidika”,alisema Njau.

Aidha kutokana na malalamiko hayo ya wafanyabiashara hayo,wafanyabiashara katika eneo hilo walifunga vibanda vyao na kwenda katika baraza hilo hali ambayo iliwafanya wananchi kukosa huduma muhimu siku nzima katika soko hilo.

Kwa mujibu wa tangazo la tarehe 31.12.2013 lilisainiwa na mkurugenzi wa halmashauri ya manispaa ya Shinyanga Festo Kang’ombe barua kumbukumbu namba SHY/MO/C.50/8VOLXV111/23 kuhusu maombi ya kukodi vibanda katika eneo la soko kuu,mwisho wa kutuma maombi ilipaswa  tarehe 13 Januari 2014 zabuni zifunguliwe na waombaji kusherehekea sherehe za ufunguzi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com