Mwenyekiti wa taasisi ya Tanzania Mzalendo Foundation ambaye pia ni mwenyekiti wa ccm mkoa wa Shinyanga Khamis Mgeja ameitahadharisha serikali kuwa makini na wageni wanaokuja nchini kwa gia ya uwekezaji kutokana na kwamba wengi wao si wema wanajihusisha na vitendo viovu kama vile ujangiri wa nyara za serikali na utoroshaji wa madini nje ya nchi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini Arusha Mgeja ambaye taasisi yake inajishughulisha na masuala ya haki za binadamu,utawala bora,utamaduni na mila na desturi alisema kuna wageni ambao wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya ujangiri wakishirikiana na vigogo wa serikali hapa nchini wakiwemo wabunge na watendaji waliopewa dhamana ya usimamizi wa mali hizo.
Amesema taasisi yake ya Mzalendo imebaini kuwa wageni hao hawafanyi
matukio hayo peke yao bali wanashirikiana na watanzania ambao wamekosa
uzalendo wa nchi hii kufanya ujangiri wa nyara za serikali, kukithiri kwa usafirishaji wa madawa ya kulevya na utoroshaji wa madini nje ya nchi hivyo kuiomba serikali kuwa mwangalifu kwa wageni hao ambao wengi wao wanakuja wakiwa na malengo mabaya kwa nchi hii.
Mgeja alisema kutokana na uzembe wa watendaji wa serikali kuna
wageni pia wamekua wakikwepa kulipa hata kodi kwa visingizio vya kufilisika kwa mitaji ya makampuni yao hali ambayo inazidi kulididimiza taifa la Tanzania .
Mgeja ameishauri serikali kuutangaza mwaka huu wa 2014 kama mwaka wa kuamsha uzalendo kwa watanzania na kuendesha vipindi maalum katika vyombo vya habari,matamasha kila wilaya ili kurejesha uzalendo kwa wananchi ambao unazidi kupotea kila kukicha.
Social Plugin