Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga SACP Evarist Mangala |
Kijana mmoja mwenye umri wa miaka 22 ameuawa kwa kuchomwa moto na wananchi wenye hasira kali waliojichukulia sheria mkononi baada ya kutuhumiwa kuiba kuku wanne siku ya mwaka mpya katika kijiji cha Isagala kata ya Mwamashele wilayani Kishapu mkoani Shinyanga.
Tukio hilo limetokea Januari mosi mwaka huu majira ya saa mbili asubuhi ambapo kijana huyo aitwaye Nganga Shija (22) mkazi wa kijiji cha Isagala tarafa ya Negezi wilayani Kishapu aliuawa kwa kuchomwa moto na wananchi waliojichukulia sheria mkononi baada ya kuiba kuku wanne kutoka kijiji cha Ikonda.
Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga SACP Evarist Mangala alisema wananchi hao walimuua kijana huyo baada ya kumtuhumu kuiba kuku hao ambao hata hivyo mmiliki wake hajajulikana.
Alisema awali marehemu alikuwa akikabiliwa na kesi za unyang’anyi wa kutumia silaha (panga) KISH/IR/186/2013 na kupatikana na mali ya wizi KISH/IR/188/2013 na alikuwa nje kwa dhamana ya mahakama.
Kufuatia tukio hilo ambalo chanzo chake ni wananchi kujichukulia sheria mkononi jeshi la polisi kwa kushirikiana na wananchi linaendelea na msako mkali wa kuwabaini na kuwakamata wahusika wa mauaji hayo.
Aidha kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga anatoa wito kwa wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi kwani ni ukiukwaji wa sheria na sheria za nchi na katiba.
Social Plugin