NB-Picha haihusiani habari |
Mtu anayedaiwa kujiita daktari mkazi wa Kijiji cha Mudio, Kata ya Masama
Mashariki wilayani Hai mkoani Kilimanjaro, (jina linahifadhiwa), anadaiwa
kuwafanyia tohara kwa nguvu wanaume 28 nyumbani kwake akisaidiwa na kikundi cha
vijana kinachomsaidia kuwakamata kwa nguvu wanaume ambao hawajatahiriwa.
Habari ambazo zilizothibitishwa na watu mbalimbali akiwemo Mganga Mkuu wa
Wilaya ya Hai, Dkt. Paul Chaote, daktari huyo bandia amekuwa wakiwafanyia
tohara wanaume hao nyumbani kwake sebuleni.
Mganga Mkuu huyo wa Wilaya ya Hai, Dkt. Chaote alithibitisha kuwepo kwa daktari
huyo bandia, anayedai anafanya kazi katika hospitali moja kubwa iliyopo mkoani
Arusha.
Alisema madai ya daktari huyo kuwa anafanya kazi katika hospitali hiyo yalikuwa
hayajathibitishwa.
Alisema tayari serikali imemzuia mtu huyo kuwafanyia tohara watu hao
kutokana na kuwa daktari bandia.
Habari ambazo zimethibitishwa na mmoja wa maofisa wa polisi ambaye hakutaka
kutaja jina lake litajwe alithibitisha daktari huyo bandia kushikiliwa polisi
kwa ajili ya mahojiano kuhusiana na tuhuma hizo.
Dkt. Chaote alisema uchunguzi wa awali umebaini kwamba daktari huyo bandia
amekuwa akiwatibu wagonjwa wake hao kwa kutumia duka lake la dawa, lililopo
kijijini hapo licha ya kwamba halitambuliki na mhudumu wake hana sifa.
“Tulipata taarifa kuhusu kufanyiwa tohara kwa wanaume wa kijiji cha Modio na
baada ya kufuatilia tulibaini ni kweli na tulipomhoji, (daktari bandia) alidai
ni daktari msaidizi katika hospitali iliyopo mkoani Arusha.
Alisema baada ya taarifa za tukio hilo walifuatilia kijijini hapo kwa
kushirikiana na Jeshi la Polisi na kubaini nyumba na vifaa vilivyokuwa
vikitumika kufanya tohara.
Alisema vifaa alivyokuwa akitumia havikubaliki kiafya.
“Tumeanza uchunguzi ili kupata watu waliofanyiwa tohara ili kujua wanaendeleaje
kiafya, hii ni kutokana na aina ya huduma aliyokuwa akiwapa kuwa haikubaliki
kiafya,” alisema.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Masama Mashariki, Ally Mwanga, alikiri
kutokea kwa tukio hilo akisema limesababisha usumbufu kwa wananchi, huku
wengine wakishindwa kwenda katika shughuli za uzalishaji mali kwa hofu ya
kukamatwa na vijana na daktari huyo bandia ili wakafanyiwe tohara.
Mwanga alisema alipokea malalamiko kutoka kwa baadhi ya wananchi ya kufanyiwa
vitendo hivyo na kutoa taarifa polisi wilayani Hai, ambapo baadaye uchunguzi
ulifanyika na mhusika pamoja na timu yake kukamatwa.
Chanzo-Majira
Social Plugin