NB-Picha haishusiani na tukio katika habari |
Jeshi la polisi mkoani Mwanza linafanya utafti wa kina kubaini askari mmoja wa kituo cha Nyakarilo wilayani Sengerema anayetuhumiwa kuomba mchango wa fedha ya mafuta kwenye familia ya mwanamke aliyefariki kwa kujinyonga.
Mwanamke huyo,Suzana James(28)mkazi wa kijiji cha Nyanzenda wilayani hapa anadaiwa kuchukua uamuzi wa kujinyonga kutokana kile kilichoelezwa na ndugu kwamba ni baada ya kuugua ugonjwa wa kuchanganikiwa akili kwa muda mrefu.
Askari huyo akiwa na mgambo mmoja alifika eneo la tukio hilo alhamisi iliyopita kufanya uchunguzi kuhusiana na kifo cha mwanamke huyo aliyejinyonga kwa kutumia kitenge alichokifunga juu ya mti wa mwembe umbali wa mita 200 kutoka nyumbani kwake.
Kaimu kamanda wa polisi mkoani Mwanza,ambaye ni mkuu wa upelelezi makosa ya jinai,Joseph Konyo akizungumza kwa njia ya simu na Mwandishi wa habari hizi alisema kitendo hicho ni kinyume na utaratibu wa polisi.
''Tunafanya utafti kujua kilichotokea hasa.Mimi kaimu RPC,ninayeshughulika na masuala ya uharifu najua mambo mengi zaidi kwa hiyo,huyo askari akibainika kweli alichukua fedha hizo atachukuliwa hatua za kisheria''alisema Konyo.
Aidha Konyo,alikiri kuwepo baadhi ya askari ndani ya jeshi hilo ambao ni waovu wanaoweza kuchukua hela kwa mazingira kama hayo kinyume na kanuni,taratibu na sheria za jeshi la polisi nchini.
Pia alisema wapo watu ambao wamekuwa wakitumia jina na wadhifa wake(RCO)kwa kujifanya polisi na kwenda kwenye maduka ya wahindi yaliyopo jijini Mwanza kisha kuchukua kwa kusingia wametumwa na RCO(Mkuu wa upelelezi mkoa).
Inadaiwa kabla ya kufika eneo la tukio askari huyo alipiga simu kwa kaimu mtendaji wa kata ya Nyanzenda,Mathias Wiliam akitoa maelekezo ya kumtaka mme wa marehemu,Simeon Katisho(32)kuandaa mchango wa mafuta kiasi cha sh.100,000ya kuwarudisha.
Kwa mujibu wa mme wa marehemu,Katisho baada ya kufanya uchunguzi huo kaimu mtendaji wa kata ya Nyanzenda Mathias Wiliamu alimvuta pembeni na kumuomba sh.100,000 zikiwa ni mchango wa mafuta ya askari hao.
Alisema kutokana na matatizo ya kufiwa na mkewe hakuwa na kiasi hicho na hivyo kutoa sh.50,000 ambazo alimkabidhi mtendaji huyo kisha kuwapatia askari na mgambo huyo ambao waliongozana kutoka msibani hadi ofisi ya mtendaji wa kata.
Na Valence Robert- Mwanza
Social Plugin