Mkazi wa kijiji cha Ibamba katika kata ya Uyovu tarafa ya Siroka wilaya ya Bukombe mkoani Geita aitwaye Shija Hamis (28) amemuua mtoto wake mwenye umri wa wiki mbili kwa kumnyonga shingo kwa kutumia mikono yake mwenyewe.
Tukio hilo limetokea tarehe 4 mwezi huu
ambapo chanzo chake kinadaiwa kuwa ni ugomvi wa kifamilia ambapo inasemekana
Shija Hamis alikamatwa mwezi wa pili mwaka jana kwa kosa la wizi wa mifugo
wilayani Biharamulo mkoani Kagera akafungwa alipotoka mahabusu alimkuta mke
wake aitwaye Julian Juma (20) akiwa mjamzito.
Imeelezwa kuwa baada ya kumkuta mke wake
akiwa mjamzito jamaa alianza kumtilia mashaka mke wake kwamba huenda mimba
aliyokuwa nayo siyo ya kwake.
Hata hivyo baada ya mwanamke huyo
kujifungua tarehe 22 Januari mwaka huu jamaa alidai kuwa mtoto aliyezaliwa siyo
wa kwake.
Inadaiwa
kuwa tarehe 4 mwezi huu jioni,Bi Juliana alikuwa anapika nyumbani kwake wakati
huo huo mme wake alikuwa nje huku mtoto wao ambaye hata hivyo walikuwa
hawajampa jina alikuwa amelala ndani.......
Wakati anaendelea kupika muda mchache
akasikia sauti ya mtoto wao akilia na ndipo Shija Hamis akaingia ndani ili
kumwangalia mtoto... lakini alipofika humo ndani alimchukua mtoto huyo na
kumnyonga hadi kufa.
Habari zinasema kuwa mara baada ya kufanya
mauaji hayo Shija Hamis alitoka ndani na
kuchukua baiskeli kama anatoka kidogo na kutokomea kusikojulikana.....
Aidha wakati Bi juliana akiendelea kupika baada ya muda hakuweza
kumsikia tena mtoto akilia huku mme wake akiwa ametoweka ,ndipo akahisi
kuwa huenda kuna kitu kimetokea akaamua
kwenda ndani na ndipo akamkuta mtoto wake amenyongwa na kutupwa chini kitu
kilichomfanya aangue kilio hajui cha kufanya na mme wake akiwa amekimbia
kusikojulikana.
Baadhi ya wananchi walioshuhudia tukio
hilo wamesema kuwa ni jambo la ajabu sana kwa bwana huyo kufanya kitendo cha
kinyama namna hiyo na kwamba watu wanaofanya vitendo kama hilo wanatakiwa
kuchukuliwa hatua kali na ikiwezekana wafungwe kifungo cha maisha.
Kamanda wa polisi mkoani Geita Leonard
Paul amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuongeza kuwa mtuhumiwa hadi sasa
jeshi la polisi linaendelea kumsaka kutokanana na kitendo alichokifanya cha
kinyama dhidi ya haki za binadamu.
Na Valence Robert-Geita
Social Plugin