Na Valence Robert
Diwani wa Kata ya Turwa wilayani Tarime mkoani Mara Charles Mbusilo kupitia tiket ya CHADEMA amehofia kubambikiziwa kesi na baadhi ya askari polisi endapo mamlaka ya juu haitalishugulikia mapema iwezekanavyo sakata la kukamatwa kwake na polisi katika mikoa mitatu tofauti kwa aina moja ya tuhuma.
Mikoa aliyokamatwa ni pamoja na Simiyu,Shinyanga na Mwanza.
Akisimulia chanzo cha kuhofia kubambikiziwa kesi na baadhi ya maaskari polisi Charles alikuwa na haya.....
"Nilikamatwa tarehe 2 mwezi wa 10 mwaka jana nikiwa kwenye duka langu la kuuza madawa ya binadamu lililopo Tarime na watumishi wa Mamlaka ya chakula na dawa Tanzania(TFDA) kutoka kanda ya ziwa,Mwanza na kuondoka na madawa yenye thamani ya shilingi milioni 50........
"Madawa hayo waliyapeleka kusikojulikana na waliokuja kunikamata ni pamoja na mkuu wa wilaya ya Tarime,John Henjewele",aliongeza.
Alisema mara baada ya kukamatwa madawa hayo hakupelekwa mahakamani wala polisi ila waliofika kumkamata waliondoka na madawa hayo.
Anasema kuwa, ilipofika tarehe 7 Februari mwaka huu alipigiwa simu na askari polisi wa Mwanza na kuambiwa hati yake ya mashtaka iko tayari kwa kwenda mahakamani.
Anasema alipofika Polisi Mwanza alipelekwa mahakamani na kusomewa mashtaka matatu ikiwa ni kuuza madawa yaliyoisha muda wake wa matumizi, kuuza dawa zinazotoka nje ya nchi na kuuza dawa za kifua kikuu.
Ameongeza kuwa mahakama ilimpa dhamana baada ya kutimiza vigezo , na alipoachiwa akakamatwa
tena na kufungwa pingu na kuambiwa ana kesi ya kujibu katika mkoa wa Simiyu.
Anasema kukamatwa kwake na kupelekwa huko mkoani Simiyu kulitokana na mtu mmoja aliyekuwa amekamatwa akiwa na risiti ya kununulia madawa iliyokuwa inaonyesha kuwa alikuwa amenunua madawa kwenye duka lake.
"Nilipelekwa rumande kwa amri ya mkuu wa upelelezi wa mkoa wa Simiyu(RCO) Evance Mwijage,Nilipoomba nipelekwe mahakani ili haki itendeke,nilipekwa mkoa wa Shinyanga kwa kigezo eti mkoa wa Simiyu hauna mwanasheria wa serikali" alisema Mbusilo.
Ameongeza kuwa kesho yake wakili wa serikali wa mkoa Shinyanga alimfikisha mahakama ya hakimu mkazi mkoa na kumsomea mashtaka Lakini alitimiza vigezo akapewa dhamana.
"Kilicho nishangaza ni kufunguliwa mashtaka yale yale kama niliyofunguliwa kule Mwanza wakati napelekwa Simiyu niliambiwa makosa tofauti" alisema.
Ameongeza kuwa alipotoka nje alishangaa askari zaidi ya kumi wakiwa na bunduki za kivita kumkamata na kuambiwa ana kesi ya kujibu katika mkoa wa Mara.
Kwa upande wa mkuu wa wilaya ya Tarime John Henjewele amekanusha tuhuma hizo dhidi yake na kusema kuwa yeye hayajui mambo hayo na wala hajahusika kwa namna yeyote.
Naye mkuu wa upelelezi mkoa wa Simiyu alipoulizwa kuhusu kuomba pesa kutoka kwa mtuhumiwa huyo ili ampe dhamana, alisema kuwa yeye hamjui na hajawahi kumuona huku akisema hataki kusikia mambo hayo .
Kwa upande wake mkuu wa upelelezi mkoa wa Shinyanga Hussein Kashindye alisema kuwa yeye ameagizwa na mkuu wa upelelezi mkoa wa Mara na huku akitoa vitisho kwa mwandishi wa habari.
"Mimi niliagizwa na RCO wa Mara na kama ukiandika habari utakiona cha moto na utapotea" alisema. Kashindye
Mkuu wa upelelezi wa mkoa wa Mara alipoulizwa kuhusika na sakata hilo,haraka alijibu kwa vitisho juu ya mwandishi wa habari.
"Atakaye andika habari hii ajiandae kufa, alisema na kukata simu.
Tukio hilo la diwani kukamatwa katika mikoa mitatu tofauti kwa aina moja ya kosa huku maafisa wa jeshi la polisi wakidaiwa kula njama za kupata fedha kutoka kwa diwani huyo,linakuja ikisemekana ni hujuma za kisiasa dhidi yake.
Social Plugin