Siku chache tu baada ya bwana Philbert Rweyemamu(Muafrika) kuwa meneja mkuu wa mgodi wa Buzwagi ulioko wilayani Kahama kwa mara kwanza wafanyabiashara mkoani Shinyanga wamekutana katika mkutano wa pamoja na migodi ya Buzwagi na Bulyanhulu katika ukumbi wa hoteli ya Karena iliyoko mjini Shinyanga kujadili masuala mbalimbali ya kibiashara na namna gani wafanyabiashara hao wanaweza kunufaika na migodi inayowazunguka lakini pia kujadili mpango wa migodi hiyo kuendeleza wagavi wa ndani ya nchi na fursa
zinazotolewa na migodi hiyo.
Mgeni rasmi alikuwa mkuu wa mkoa wa Shinyanga Allya Nassoro Rufunga ambaye ametumia fursa hiyo kuwataka wafanyabiashara mkoani Shinyanga kutumia fursa za
kibiashara zinazotolewa na migodi ya kampuni ya uchimbaji wa madini ya
dhahabu African Barrick (ABG) ili kuinua
biashara zao na kukuza uchumi wa mkoa na taifa kwa ujumla.
Katika mkutano wa wafanyabiashara wa
mkoa wa Shinyanga na migodi ya Buzwagi na Bulyanhulu iliyopo wilayani Kahama
mkoani Shinyanga, Rufunga amesema ofisi
yake imekuwa ikipokea malalamiko mengi ya wafanyabiashara kuhusu kutopewa fursa
ya kufanya biashara na migodi hiyo jambo ambalo limekuwa likikwamisha ukuaji wa
biashara zao.
Amesema kupitia fursa zinazotolewa na migodi hiyo ni vyema wafanyabiashara wakazitumia kama inavyotakiwa kwani migodi hiyo ipo katika maeneo yao na
haibagui mtu yeyote na kwamba hata wafanyabiashara wa nje ya mkoa wanaruhusiwa kufanya biashara na migodi hiyo.
Mkuu huyo wa mkoa amesema serikali itaendelea kushirikiana
na migodi huku akiwataka wafanyabiashara kufika katika ofisi za mkoa kama wanapata
matatizo na kuongeza kuwa sekta ya madini ni miongoni mwa sekta zitakazosaidia kuinua uchumi wa mkoa wa
Shinyanga ukiachilia mbali kilimo na viwanda.
Kwa upande wake meneja mkuu wa mgodi wa Buzwagi Philbert
Rweyemamu amesema lengo mkutano huo ni kukutana na wafanyabiashara hao ili
kuwaelimisha kuhusu fursa mbalimbali za kibiashara zinazotolewa na migodi hiyo
ili kuhakikisha kuwa wananchi wanafaidika nayo.
Rweyemamu ambaye ni meneja wa kwanza wa kiafrika kuongoza
migodi amesema kampuni yake inalenga katika kushirikiana na wafanyabiashara wa
ndani kuendeleza uchumi wa nchi na kutoa fursa katika ngazi ya jamii za
kujishughulisha katika biashara ili kuongeza kipato katika familia.
Hii ni mara ya kwanza kwa kampuni ya uchimbaji madini ya
dhahabu ya African Barrick kukutana na wafanyabiashara mkoani Shinyanga na
imeahidi kuuendelea kukutana na wafanyabiashara kila mwaka ili kuangalia namna
gani wananchi wanaozungukwa na migodi wafaidike na madini yao.
Social Plugin