Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Mapanga Kahama!!! WAFUASI WA CCM WACHARANGWA MAPANGA KAMPENI ZA UCHAGUZI WA DIWANI UBAGWE ,CHADEMA 13 WADAKWA AKIWEMO MBUNGE WA MASWA MASHARIKI

 Katibu mwenezi wa CCM  wilaya ya Kahama Masood Melimeli aliyeumia sehemu ya mkono na bega katika vurugu kati ya Chadema na CCM akiwa katika hospitali ya wilaya ya Kahama
Afisa  mtendaji wa Kata ya Ubagwe Stephen Kimario aliyepigwa vibaya sehemu za kichwani katika vurugu hizo
Dereva  wa CCM Charles Muhiga aliyejeruhiwa sehemu za kichwani -PICHA ZOTE NA RAYMOND MIHAYO-Kahama.


Kampeni za uchaguzi mdogo wa kiti cha udiwani katika kata Ubagwe Wilayani Kahama Mkoani Shinyanga,zimeingia doasari baada ya watu wanaodhaniwa kuwa ni wafuasi CHADEMA kuwavamia na kuwajeruhi vibaya kwa  kuwacharanga mapanga wafuasi watano wa CCM.

Akiongea na waandishi wa habari akiwa katika hospitali ya Wilaya ya Kahama akiwa miongoni mwa majeruhi waliolazwa katika hospitali hiyo  Katibu mwenezi wa CCM Wilaya ya Kahama Masood Melimeli amesema tukio hilo limetokea jana majira ya saa moja na nusu usiku wakati wakitokea katika kijiji cha Ihata kwenda Itobola katika kampeni.

Amesema akiwa na wenzake walipofika katikati ya pori walikutana na gari la CHADEMA aina ya Toyota land Cruser ikiongozwa na Mbunge wa Jimbo la Maswa Mashariki mkoani Simiyu Sylivester Kasulumbayi na kuanza kuwashambulia kwa kutumia mapanga, nondo pamoja na fimbo.

 Katibu mwenezi  huyo wa CCM Masood Melimeli amesema  ameumia sehemu ya mkono na bega huku wenzake akiwemo Ramadhani Salumu aliyepigwa panga la mguu na Mkono, Sebastian Masonga aliyevunjwa mkono wa kushoto, dereva Charles Muhiga aliyejeruhiwa sehemu za kichwani na mtendaji wa Kata ya Ubagwe Stephen Kimario aliyepigwa vibaya sehemu za kichwani na wengine wawili walikimbia kusikojulikana.

Akizungumzia kuhusu tukio hilo mwenyekiti wa chama cha TADEA ,ambacho pia kinafanya kampeni zake katika kata hiyo,Wilaya ya Kahama Charles Lubala amesema vurugu hizo zilianza baada ya mfuasi mmoja wa CHADEMA kuvamia katika mkutano wa CCM na ndipo CCM walipomkamata na kumuweka katika gari la CCM kwa lengo la kumpeleka katika kituo kidogo cha Polisi Bulungwa.

Baada ya kumuweka katika gari la CCM  ndipo wafuasi wa CHADEMA walipotangulia mbele na kuweka vizuizi barabarani na hivyo kusababisha vita hivyo kufanyika na kupelekea watu hao kujeruhiwa akiwemo mtendaji wa kata hiyo.

Hata hivyo akizungumza na malunde1 blog kwa njia ya simu mwenyekiti wa CHADEMA wilaya ya Kahama Juma Protas alisema..........

“Siyo kweli kwamba tunahusika katika vurugu hizi,vijana watatu wa CHADEMA ndiyo waliotekwa na CCM katika eneo la makao makuu ya kata ya Ubagwe,baada ya kutekwa,wakafungwa kamba na kuingizwa kwenye gari la CCM,ndipo wananchi walipokwenda kuwasaidia vijana hao ndipo ilipotokea purukushani kati ya wananchi na wafuasi wa CCM”.

“Baada ya purukushani hizo,CCM wakapiga simu polisi,polisi wakaenda kwenye kambi ya CHADEMA na kupiga risasi juu kisha kuwakamata wafuasi 13 wa Chadema akiwemo mbunge wa Maswa Mashariki Sylivester Kasulumbayi,CCM ndiyo waliteka vijana watatu  wa CHADEMA na vijana hawa hadi sasa hawajulikani walipo”,aliongeza Protas.

“Katika vurugu hizi chadema pekee wamekamatwa,nataka tu kuwaambia watu wa CCM,waache demokrasia ifuate mkondo wake,wasitegemee kuwa kutumia nguvu siku zote itasaidia,wananchi wanahitaji mabadiliko kwa njia ya amani na utulivu”,alisema mwenyekiti huyo wa CHADEMA.

Akizungumza na malunde1 blog  kwa njia ya simu Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga ACP Evarist Mangala alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuongeza kuwa jeshi la polisi linawashikilia watu 13 kuhusiana na tukio hilo kwa mahojiano zaidi.


Kampeni za Uchaguzi katika kata ya Ubagwe Wilayani Kahama Mkoani Shinyanga zinafanyika kufuatia aliyekuwa diwani katika kata hiyo Richard Mndula kufariki dunia mwaka jana vyama vitatu vya siasa ikiwemo CCM, TADEA pamoja na CHADEMA vinapigania kiti hicho.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com