Katika kile kilicholezwa kuwa ni kutofurahishwa na hatua ya mkuu
wa mkoa wa Geita, Magalula Said Magalula kuagiza kukamatwa na kuwekwa ndani kwa
wawekezaji wa zao la pamba wanaofanya shughuli zao katika mkoa huo kwa madai
hawajatekeleza agizo la kufunga mikataba na wakulima wa zao la pamba,Chama Cha
Wakulima wa Zao la Pamba nchini (TACOGA) kimemlalamikia mkuu huyo wa mkoa kikimtuhumu kutumia vibaya madaraka yake
aliyopewa na Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania mheshimiwa Dkt Jakaya Mrisho
Kikwete.
Kwa mujibu wa tamko rasmi lililotolewa kwa
waandishi wa habari mjini Kahama na
mwenyekiti wa TACOGA, Elias Zizi agizo hilo linapingana na maelekezo
yaliyotolewa hivi karibuni na rais Kikwete akiagiza wakulima kutolazimishwa
kujiunga katika kilimo cha mkataba mpaka kwanza wapewe elimu ya kutosha.
Mwenyekiti huyo wa TACOGA alisema mapema wiki
iliyopita mkuu huyo wa mkoa aliagiza kukamatwa kwa wawakilishi wa kampuni
zinazonunua pamba waliokuwa wamehudhuria kikao cha wadau wa zao hilo
kilichofanyika mjini Geita baada ya kuwataka watoe taarifa ya vikundi vingapi
vya wakulima ambavyo wamefunga navyo mkataba.
Zizi alisema wawekezaji waliokamatwa na kuwekwa
ndani kwa agizo la mkuu huyo wa mkoa kuwa ni pamoja na mwakilishi wa kampuni ya
Fresho Investment, Kampuni ya ICK Cotton Co. Ltd na Kahama Oil Mill Ltd ambao wote
wanafanya shughuli zao katika mkoa huo wa Geita.
Zizi alisema TACOGA wameshangazwa na hatua ya
mkuu huyo wa mkoa na kudai ni matumizi mabaya ya madaraka aliyopewa na Rais
Kikwete na kwamba suala la kilimo cha mkataba pamoja na kuwa ni hiari hata hivyo
lilisitishwa kwa muda baada ya kujitokeza kwa changamoto kadhaa baada ya
majaribio yake katika baadhi ya maeneo.
Hata hivyo mkuu wa mkoa wa Geita, Magalula Said
pamoja na kukiri kutoa agizo la kukamatwa kwa wawekezaji hao alikanusha sababu
zilizotolewa na uongozi wa TACOGA walizodai ni kutokana na kutokujiunga na
mpango wa kilimo cha mkataba na kuongeza kuwa wawekezaji hao walikamatwa kutokana na kitendo chao cha kukiuka
utaratibu wa usambazaji wa pembejeo za kilimo katika upande wa viuatilifu
ambapo walitakiwa kuvisambaza kwa wakulima kwa njia ya mkopo na siyo kuwauzia
kwa fedha taslimu.
Mmoja wa wawakilishi wa makampuni hayo alithibitisha
kukamatwa kwao na kuwekwa mahabusu ya polisi kwa zaidi ya masaa manne ambapo
hata hivyo alisema baadae waliachiwa huru baada ya polisi kukosa shitaka la
kuwafungulia ili kuweza kuwafikisha mahakamani.
Social Plugin