Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MWANAMKE AKAMATWA AKITUPA MTOTO MCHANGA CHOONI HUKO MBEYA

Rukia Fungameza[20]mkazi wa mtaa wa Ilembo Kata ya Iwambi Anaetuhumiwa kutupa mtoto chooni
Hii ndilo shimo la choo alimotumbukizwa mtoto huyo 
Wakina mama wakilia kwa uchungu
Mwenyekiti wa mtaa huo Juma Mbuza mwenye Flana ya bluu akiwa na barozi kushoto na mashuhuda wengine wakimsikiliza mwenyekiti huyo

Mwanamke mmoja aliyefahamika kwa jina la Rukia Fungameza[20]mkazi wa mtaa wa Ilembo Kata ya Iwambi anashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoani Mbeya kwa tuhuma za kutupa chooni kichanga jinsi ya kiume na kusababisha kifo chake.

Mwenyekiti wa mtaa huo Juma Mbuza amesema walimtilia shaka mtuhumiwa Februari 18 mwaka huu katika klabu ya pombe za kienyeji baada ya kutoonekana na ujauzito,ndipo walipomuuliza kulikoni naye kudai kuwa amejifungua lakini mtoto yupo nyumbani.

Kauli hiyo haikumridhisha Mwenyekiti huyo ndipo alipoamua kumtafuta balozi wake aitwae Daud Dule na kumuuliza mtoto yupo wapi ndipo alipoanza kuwa na wasiwasi hali iliyowalazimu kumkamata kutoa taarifa kituo cha Polisi Iyunga ambapo kabla ya kufika Kituoni majira ya saa kumi na moja jioni mtuhumiwa alikiri kujifungua na kutupa kichanga chooni Februari 18 mwaka huu.

Baada ya taarifa hiyo mtuhumiwa alikamatwa na kupelekwa kituo kikuu cha kati Febuari 19 ambapo Polisi hawakuweza kufika eneo la tukio licha ya Mwenyekiti wa mtaa kufuatilia mara kwa mara kwa mkuu wa kituo cha Polisi Iyunga ambapo alijibiwa kuwa watafika.

Hata hivyo baada ya Polisi kutofika eneo la tukio kwa siku mbili tangu kukamatwa mtuhumiwa Mwenyekiti wa mtaa alitoa taarifa katika kikao cha kata  Februari 21 kufuatia tukio lililotukia mtaani kwake na Polisi kushindwa kufika kwenye tukio siku tatu baada ya tukio hali ambayo ilikuwa kero mtaani kwake.

Polisi walifika eneo la tukio Februari 22 majira ya saa tano na nsu asubuhi wakiambatana na Kikosi cha Zimamoto Jiji la Mbeya ndipo walipoanza anza kuibua mwili wa mtoto ambapo ulikutwa umeharibika vibaya kutokana na kukaa kwa muda wa siku nne bila kuibuliwa umbali wa kilometa saba tu kutoka Jijini.

Baada ya mahojiano mtuhumiwa alidai sababu za kutupa kichanga hicho cha kiume ni kutokana na kuogopa aibu kwa mumewe aliyepo Songea mkoani Ruvuma kikazi ambapo mimba hiyo aliipata nje ya ndoa.
Uchunguzi umebaini kuwa mwanamke huyo aliagizwa na mumewe kurejea Songea mwishoni mwa mwaka jana lakini alikataa akidai kuwa angeenda mwaka huu baada ya kumsaidia kaka yake shughuli za palizi.

Kabla ya kichanga kilichotupwa chooni mtuhumiwa ana mtoto mwingine jinsi ya kike anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka miwili na nusu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mtaa amelilalamikia Jeshi la Polisi kwa kutoenda eneo la tukio mapema hali ambayo inasababisha wananchi kujichukulia sheria mkononi hali ambayo inweza kuepukika.

Baadhi ya mashuhuda akiwemo mama Emilly Amnoni na Paulo Mbawala wamelaani vikali kitendo kilichofanywa na mwanamke huyo kwani wamedai ni cha kinyama na ni cha kwanza mtaani kwao hivyo wanaomba sheria iweze kuchukua mkondo wake ili kukomesha kabisa vitendo vya kikatili Mkoani Mbeya.
Credit-folclassic.com

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com