Na Saimeni Mgalula
Wazazi wa watoto wanaosoma shule ya msingi Lubwe iliyopo kitongoji cha Lubwe Kijiji cha Kikota Kata ya Kiwira Wilaya ya Rungwe Mkoani Mbeya wamemtaka Mwalimu mkuu wa shule hiyo Karim Msisiri kuondolewa shuleni hapo kwa tuhuma za kufuja raslimali za shule.
Kauli hiyo wameitoa katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji hicho ulioitishwa na Mratibu wa elimu Kata Bi Tujengwe Mwangobola na kusimamiwa na Mwenyekiti wa kijiji Godwin Mwakasege ambapo Mratibu Kata ya Ilundo Hard Mwambula alialikwa kusikiliza.
Wazazi walimtuhumu mwalimu Msisiri kufuja zaidi ya shilingi laki tano zilizotokana na mauzo ya mchanga na miti ambazo ni raslimali za kijiji zilizotolewa na kijiji kwa ajili ya kuendeleza shule hiyo lakini amekuwa akizitumia kwa matumizi binafsi huku shule ikikosa madirisha na sakafu katika madarasa.
Akiongea na eddy blog kwa niaba ya kamati ya shule hiyo mjumbe Frank Mwangomo kutokana na vitendo vya Mwalimu mkuu kukithiri na kutoshirikisha kamati imepelekea Mwenyekiti wa kamati ya shule Edward Kabuka kujiuzulu.
Frank amesema kuwa kamati ya shule hiyo pia imesikitishwa na kitendo cha Mwalimu huyo kumtumia Mwenyekiti wa kamati ya awali aliyeenguliwa ambapo mwenyekiti huyo alitafuna pesa za shule shilingi mia moja hamsini elfu,baada ya kubanwa na mtendaji wa kijiji Felix Michael amerejesha shilingi elfu themanini na kiasi kilichosalia kuahidi kurejesha Februari 27 mwaka huu.
Kwa upande wake mwalimu mkuu amekiri kufanya makosa hayo na kuomba msamaha kutokana na majukumu mengi na kuahidi kuwa hatarudia kufanya makosa tena hivyo wazazi wasife moyo bali waendelee kushirikiana ili kukuza taaluma kwa watoto wa shule hiyo.
Aidha mwalimu aliwaambia wazazi kuwa kwa muda wa miezi saba amekusanya kiasi cha shilingi mia moja hamsini na tisa elfu ambazo alikusanya kutokana na mauzo ya mchanga na miti na fedha hizo zilikatiwa stakabadhi.
Baada ya mvutano mrefu Mratibu wa Elimu aliwataka wazazi kupiga kura kujua hatima ya mwalimu kama abaki shuleni au la,ndipo wazai waliotaka mwalimu asamehewe walikuwa 14 na waliotaka mwalimu aondolewe walikuwa 30.
Kwa upande wake Mratibu aliwaambia wazazi kuwa anaheshimu mawazo yao lakini hana mamlaka ya kumwondoa mwalimu bali atapeleka mawazo yao kwa Afisa Elimu Wilaya yeye ndiye ana uwezo wa kutoa maamuzi lakini aliwapa muda kama watabatilisha uamuzi wao watoe taarifa kabla ya Februari 19 mwaka huu katika mkutano watakaoitisha kupitia kwa mwenyekiti wa kijiji.
Wakati huo huo uchunguzi umebaini mlinzi wa shule hiyo Hamisi Mbange anadai mshahara wake kwa kipindi mwa mwaka 2012/2013 jumla ya shilingi laki tatu na elfu ishirini na tano ambazo hajalipwa na uongozi wa shule kwa muda mrefu bila mafanikio licha ya wazazi kuchangia shilingi elfu moja mia mbili kwa mwaka kila mtoto
Social Plugin