Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Shinyanga kumekucha!!! WAZEE KUANDAMANA KUDAI HAKI ZAO KWA MUJIBU WA SHERIA YA WAZEE

Picha ya mbunge wa jimbo la Solwa ambapo Wazee  wameomba kukutana na mbunge wao  huyo wa jimbo la Solwa, Ahmed Salum ili wamweleze kilio chao na kumuomba achukue kilio hicho akiwasilishe bungeni kuhoji ni kwa nini serikali imekataa kutunga sheria ya wazee hadi hivi sasa wakati wao kila siku wanaendelea kuteseka katika nchi waliyoitumikia wakati wakiwa vijana
Katika hali inayoashiria kuchoshwa na ahadi zinazotolewa na serikali mara kwa mara kuhusu suala la utungwaji wa sheria ya wazee nchini, wazee hao sasa wametishia kuandamana hadi kwa mkuu wa wilaya ya Shinyanga kudai kutekelezewa haki zao kwa mujibu wa sera ya wazee.


Hali hiyo imejitokeza juzi katika mkutano wa kujadili rasimu ya katiba mpya pamoja na sera ya wazee uliofanyika katika kijiji cha Singita kata ya Usanda wilayani Shinyanga, ambapo wazee hao walielezea masikitiko yao kutokana na danadana zinazopigwa na serikali katika suala zima la utungwaji wa sheria ya wazee hapa nchini.

Wazee hao walisema pamoja na serikali kutunga sera ya wazee lakini kwa zaidi ya miaka 10 sasa sera hiyo haijatungiwa sheria hali ambayo inachangia kwa kiasi kikubwa baadhi ya wazee kukosa haki zao kama zilivyoainishwa ndani ya sera hiyo ikiwemo suala la kupatika bure huduma za matibabu.

Akichangia hoja kuhusu rasimu ya katiba mwenyekiti wa wazee wilayani Shinyanga, Edward Lupimo alisema pamoja na rasimu hiyo kuingiza ibara inayohusu wazee lakini haifafanuliwa mahitaji muhimu ambayo wazee wanapaswa kupatiwa kwa mujibu wa katiba hali ambayo itakuwa na utata katika utekelezaji wake.

Akitoa mfano, Lupimo alisema katika sura ya Nne ya rasimu ya katiba, inayozungumzia, Haki za Binadamu, wajibu wa Raia na Mamlaka za nchi, sehemu ya kwanza fungu la 48 linazungumzia mamlaka za nchi zitaweka utaratibu utakaowezesha wazee kupata fursa ya;

“Kushiriki katika shughuli za kijamii, kuendeleza maisha yao, kutambuliwa utu wao na kuheshimiwa pasipo kudharauliwa; na Kupata mahitaji ya msingi kutoka kwenye familia zao, jamii na mamlaka za nchi.”

“Hapa utaona wazi haikufafanuliwa kwa uwazi, kwamba mzee atapaswa kushiriki katika shughuli zipi za kijamii, lakini pia maisha haya ya wazee yataendelezwa vipi, na hata suala la kupata mahitaji ya msingi ingekuwa vizuri likawekwa wazi ili kuwaondolea wazee hawa usumbufu pale watakapokuwa wanadai haki zao za kikatiba,” alieleza Lupimo.

Kutokana na hali hiyo wazee hao walisema iwapo serikali haitaharakisha mchakato wa kutungia sheria sera ya wazee iliyozinduliwa mwaka 2003, watajikusanya na kufanya maandamano kwenda kwa mkuu wa wilaya ya Shinyanga ili kudai haki zao za msingi ikwemo suala hilo la sheria ya wazee.

Wazee hao pia wameomba kukutana na mbunge wao wa jimbo la Solwa, Ahmed Salum ili wamweleze kilio chao na kumuomba achukue kilio hicho akiwasilishe bungeni kuhoji ni kwa nini serikali imekataa kutunga sheria ya wazee hadi hivi sasa wakati wao kila siku wanaendelea kuteseka katika nchi waliyoitumikia wakati wakiwa vijana.

“Ukweli ni kwamba bila ya kuwepo kwa sheria ya wazee huduma zote tunazostahili kupatiwa kwa mujibu wa sera ya wazee itakuwa ni ndoto, maana watendaji wa serikali wengi ni jeuri, hawapendi kuwahudumia wazee, wanasahau kuwa na wao ni wazee watarajiwa, leo hii pamoja na kuelezwa matibabu kwa wazee ni bure, matibabu hayo hatupati,” alieleza Lupimo.,

Awali mwakilishi wa Shirika la Tanzania Association of Women Leaders in Agriculture and Environment (TAWLAE) mkoani Shinyanga, Judith Kalwani aliyemwakilisha mkurugenzi wa  shirika hilo, Eliasanya Nnko, alisema lengo la mkutano ni kutoa fursa kwa wazee wa Shinyanga kujadili baadhi ya masuala yanayowahusu yaliyomo ndani ya rasimu ya katiba.

Kalwani alisema Shirika lake ambalo pia hushughulikia masuala yanayohusu wazee limeona ni muhimu wakati mchakato wa katiba mpya ukiendelea katika hatua za kujadiliwa kwa rasimu yake ni vizuri wazee pia wakapata fursa ya kutoa mawazo yao ambapo alishauri suala la uharakishwaji wa utungwaji wa sheria ya wazee nchini.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com