Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Ukatili wa kutisha!!! WANANCHI WACHOMA NYUMBA KWENYE KAYA 5 KWA UCHAWI SUNGUSUNGU WATAJWA KUHUSIKA

NB picha kutoka maktaba 
Wananchi waliojichukulia sheria mkononi wakiongozwa na kamanda wa sungusungu wamechoma moto nyumba katika familia tano katika kitongoji cha Elimu kijiji cha Kakeneno kata ya Buziku wilayani Chato mkoani Geita  baada ya kuwatuhumu wamiliki wa nyumba hizo kuwa ni wachawi kwa kile kinachosemekana kuwa watoto wamekuwa wakifariki mara kwa mara katika kijiji hicho.

Tukio hilo limetokea jana jioni mara baada ya wananchi kuwatuhumu wanawake watano kuwa ni wachawi na wamekuwa wakiua watoto kwa muda mrefu na hatimaye juzi siku ya Jumamosi wakaitisha mkutano kwa ajili ya kuwapigia kura kubaini nani ni mchawi.

Kufuatia upigaji kura huo ndipo wakapata kura nyingi za kwamba wanahusika ni uchawi kwani matukio ya watoto kufa katika kijiji hicho yameshamili sana.

Shuhuda wa tukio hilo ambaye hakupenda jina lake litajwe na  yuko mafichoni kwa usalama wake amesema baada ya kura hizo kupigwa  Jumamosi, siku iliyofuata (jana) ukatokea msiba ambapo Jumapili hiyo saa 12 jioni walikuwa kwenye msiba kwa familia ya Dadala na ndipo wakatoka msibani na kwenda kuchoma nyumba hizo.

 Shuhuda huyo amesema nyumba zilizochomwa ni ya Mwananzila,Sofia,Mwanabukumbi,Mama Sodoki,kwa Roza  ambapo vitu mbalimbali vimeteketezwa kwa moto na thamani yake haijajulikana.

Imeelezwa kuwa waliochoma nyumba hizo walikuwa wanaongozwa na kamanda wa jeshi la jadi sungusungu aitwae Yela Shokagauje.

Mwenyekiti wa kijiji cha Kakeneno James Mlomba amekiri kuwepo mkutano wa kuwapigia kura watu wanaodhaniwa kuwa ni wezi na wachawi katika kijiji hicho lakini akasema hajui kama wameenda kuwachomea nyumba zao.

 “Ni kweli mwandishi mimi pia nilikuwepo kwenye mkutano huo kama kiongozi na tulipiga kura kabisa lakini baada ya hapo sikujua kilichoendelea tena,wananchi ndiyo wamefanya kitendo hicho’’,alisema Mlomba.

Naye diwani wa kata ya Buziku kilipo kijiji hicho Bwana Zanziba Masanja amekiri kupata taarifa hizo za familia tano kuchomewa nyumba zao kwa imani ya kishirikia na  amelaani kitendo hicho kwani kufanya hivyo ni kukiuka haki za binadamu.
Tukio hili limekuja siku chache tu baada ya kamanda wa polisi mkoa wa Geita Leonard Paul kuwataka wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi na yeyote atakayekamatwa kuchukulia hatua kali za kisheria


Na Valence Robert-Geita

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com