Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Vita dhidi ya watoa mimba!!! WAWILI WAKAMATWA WAKITOA MIMBA YA MIEZI 6,HAWALA NA MGANGA MTOA MIMBA WATOROKA

NB-Picha haihusiani na habari hapa chini
Ikiwa ni siku chache tu baada ya mwanamme mmoja kufanya  tukio la kunyonga   mtoto wake mwenye umri wa  wiki wilayani Bukombe mkoani Geita na mtuhumiwa kutoroka kusikojulikana , Jeshi la polisi mkoani humo linashikilia  watu wawili  huku wengine wawili wakiendelea kusakwa akiwemo mganga wa duka la dawa muhimu kwa tuhuma za kumtolea mimba  ya miezi 6 msichana aliyefahamika kwa jina la Pendo katika kijiji cha Rwezera kata ya Rwezera wilayani Geita.

Tukio hilo limetokea Februari 6 majira ya saa tano asubuhi  ambapo Pendo (19)alitolewa mimba na mganga aliyejulikana kwa jina la Okong’o maarufu kama Mjaruo.

Imeelezwa kuwa siku hiyo asubuhi kwenye chumba cha duka moja  la madawa, mganga huyo baada ya kutenda unyama huo alitoweka katika mazingira ya kutatanisha.

Akieleza tukio hilo afisa mtendaji wa kijiji hicho Peter Chota alisema kuwa binti huyo aliyekuwa anaishi na shangazi yake baadae alienda kukaa na rafiki yake aitwae Pendo Obadia (23) na siku iliyofuata akaenda kwa mganga huyo ili kutimiza adhima yake.

Alisema  baada ya kumaliza kutoa mimba hiyo ya miezi sita alirudi kwa rafiki yake na baadaye alianza kusikia maumivu ndipo rafiki yake akaenda kwa shangazi yake kumpa taarifa kuwa wajina wake Pendo anaumwa.

“Hata hivyo shangazi yake ambaye hakufahamika jina mara moja alimwambia rafiki yake amlete nyumbani kwake na ndipo akafuatwa Pendo lakini alipomfikisha nyumbani shangazi yake alishtuka kuona ujauzito haupo tena akawa na wasiwasi huku hali ya binti huyo ikiendelea kuwa mbaya”,alisema afisa mtendaji wa kijiji.

“Baada ya shangazi kuona hali inazidi kuwa mbaya akawauliza kulikoni!!, wakamwambia kuwa mimba imeharibika, ndipo shangazi akadai wanadanganya,akaanza kuwajulisha watu juu ya kilichotokea,huku mtoa mimba akimtaja aliyemtolea mimba”,aliongeza afisa mtendaji Chota.


“Kufuatia hali hiyo jeshi la sungusungu lilianza msako mkali kumtafuta mganga, likipekua nyumba zote za kulala wageni bila mafanikio”,alieleza Chota

Alisema baada ya mtuhumiwa aliyetoa mimba kusikia kuwa anatafutwa na jeshi la polisi alitoroka na mwanamme aliyempa ujauzito (hawala wa Pendo).

Kamanda wa polisi mkoani hapa Kamishina msaidizi mwandamizi Leonard Paul amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na juhudi za kuwasaka waliotoroka zinaendelea na kwamba watuhumiwa wote wawili( Pendo anayetuhumiwa kutoa mimba na Pendo rafiki anayetuhumiwa kumshauri mwenzie kutoa mimba)wameshikiliwa na polisi wilayani Geita baada ya Pendo kulazwa katika kituo cha afya Nzera kabla ya kupelekwa Geita.


Na Valence Robert-Geita

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com