Mahakama ya wilaya ya Geita
imemhukumu kwenda jela Selemani Nkwenda(36) mkazi wa mseto mjini Geita baada ya
kutumia jina la katibu wa siasa na uenezi CCM Nape Nnauye kutapeli watu kipindi
cha uchaguzi wa chama 2012.
Akisoma mashtaka hayo mbele ya hakimu wa mahakama hiyo
Zabroni Kesase ,wakili wa serikali Janet Kisabo alisema Selemani Nkwenda alitenda kosa hilo mnamo tarehe 5 na 19 mwaka
juzi akiwa eneo la Mseto ambapo
alimpigia simu Peter Mwininga kwa namba 0767768464 na kujitambulisha kuwa yeye
ni Nape Nnauye na kumwambia kuwa atampigia baadae waongee zaidi.
Aidha katika kosa la pili mtuhumiwa mnamo tarehe 19
mwaka juzi alimpigia simu kwa namba hiyo hiyo na kumwambia amtumie pesa kiasi
cha shilingi milioni moja na laki tano huku akidai yeye yuko Dodoma makao makuu
ya chama na atajitahidi jina la Mwininga alirudishe kwa vile alikuwa anagombea nafasi
ya mwenyekiti wa vijana mkoa wa Geita.
Baada ya kumaliza kusoma mashitaka hayo wakili huyo
aliiomba mahakama itoe adhabu kali dhidi ya mtuhumiwa ili liwe fundisho kwa
wengine wenye nia ya kutaka kutenda kosa kama hilo katika jamii.
Hakimu wa mahakama hiyo Zabroni Kesase aliyekuwa
anaiskiliza kesi hiyo baada ya kujiridhisha na pande zote za mtuhumiwa na
mlalamikaji huku ushahidi ukijitosheleza bila mashaka yoyote ,alitoa
hukumu ya kifungo cha mwaka mmoja ikiwa ni kila kosa ni kutumikia kifungo cha
miezi sita na kwa makosa mawili anatumikia kifungo cha mwaka mzima.
Imeelezwa kuwa mtuhumiwa tangu mwaka juzi katika
uchaguzi wa ndani wa chama cha mapinduzi uliokuwa unafanyika kote nchini alitumia
mwanya huo kuweza kutapeli watu mbalimbali mkoani Geita kabla hajakamatwa na
kutiwa hatiani akitumia jina la katibu siasa, itikadi na uenezi wa chama cha
mapinduzi taifa Nape Nnauye.
Na Valence
Robert-Geita