Wananchi wa kijiji cha Mgusu kilichopo
wilayani Geita mkoani Geita wameilalamikia kamati ya madiwani walioenda
kuangalia mgawanyo wa rasilimali za halmashauri na kuibua hoja ya kuwa kijiji
chao hakina usajili na kumwomba waziri mkuu aingilie kati suala hilo mapema
iwezekanavyo.
Kijiji cha Mgusu kilichopo katika kata ya Mtakuja
wilayani Geita kimebainika kuwa hakina usajili kama kijiji licha ya wakazi wa
kijiji hicho kufahamu kuwa kijiji chao kina usajili kilichoupata tangu 2009 chini
ya mbunge aliyekuwepo Ernest Mabina.
Sintofahamu hiyo imeibuka hivi karibuni katika kamati
ya maridhiano baina ya halmashauri ya mji wa Geita na halmashauri ya wilaya ya
Geita mara baada ya kugawana eneo la utawala na rasilimali zilizokuwa
zinamilikiwa na halmashauri mama ya wilaya.
Kamati hiyo iliyokuwa na taarifa ya mapendekezo juu ya
mgawanyo wa mapato yatokanayo na shughuli za uchimbaji wa dhahabu katika mgodi
wa Geita Gold Mine (GGM) iliyowasilishwa kwenye baraza la madiwani tar
16.7.2012 ilibaini katika hadidu za rejea za kutambua maeneo/mipaka ya leseni ya
uchimbaji wa dhahabu special mining license(SLM 45/99).
Aidha masuala muhimu yaliyobainika baada ya tume
kukamilisha zoezi la tathmini ni katika kifungu cha 3.4 ambacho kinaeleza kuwa kijiji
cha Mgusu kimo ndani ya hifadhi ya msitu wa Geita (Geita Forest Reserve) na hakijasajiliwa.
Aidha kifungu namba 3.8 kinasema....
“Pia tume
ilibaini vijiji vilivyomo ndani ya leseni ya uchimbaji(SML) kama ifuatavyo,
Nyamalembo,Mtakuja,Katoma,Mgusu(kijiji hiki hakina usajili)’’
Kifungu namba 3.1 nacho kinasema... “Mipaka ya leseni
ya GGM ya uchimbaji wa dhahabu (SML 45/99) imo ndani ya hifadhi ya msitu wa
Geita (Geita Forest Reserve –GN 10 ya mwaka 1953 ambapo mmiliki wake ni Wizara
ya mali asili na utalii kupitia wakala wa msitu (Tanzania Forest Agency)’’.
Nukuu hizi zote zinaonyesha kuwa kamati hiyo ilibaini
kijiji cha mgusu hakijasajiliwa na kinakaliwa na watu ambao wako kwenye hifadhi
ya msitu na wanafanya kazi za uchimbaji kwenye eneo la hifadhi ambapo pia ni
leseni ya mgodi wa GGM special mining license ya mwaka 1953 hivyo basi hawatambui
uwepo wa kijiji hicho kisheria.
Mwenyekiti wa wachimbaji wadogo wadogo Mhoja Kiyuga
ambaye alikuwa mwenyekiti wa kijiji hicho cha Mgusu alipoulizwa kuhusu suala
hilo alisema kijiji hicho kimesajiliwa kisheria.
“Ninasema kuwa kijiji kimesajiliwa tangu 2005 na Jamhuri
ya muungano wa Tanzania kwa sheria namba 7 ya mwaka 1984 na kupewa namba
MZ.KIJ/734 tarehe 8 julai 2005 na kipo katika kata ya Mtakuja wilaya ya Geita
Mkoa wa Mwanza kipindi hicho na kilisainiwa na B.B. Claudio msajili wa vijiji.
Bwana Mhoja aliongeza kuwa eneo hilo ni hifadhi
na tena sio eneo la GGM.
“Sisi tumepewa
leseni viwanja 20 vya Saccos yetu kwa ajili ya kuchimba wachimbaji wadogo
wadogo, na tulipewa leseni hizo na naibu waziri wa nishati na madini Stephen
Masele mwaka 2012 hivyo huwezi kusema kuwa ni eneo la GGM ama ni hifadhi
tena kwa ushahidi wote wa kiserikali niliokutajia hapo mwandishi na tunalipa
mapato yote na mrahaba kama sheria ya madini inavyosema hata ukienda ofisi ya
madini’’ alisema Mhoja.
Kwa upande wa Michael Malebo ambaye ni mchimbaji mdogo
mdogo katika kijiji hicho cha Mgusu amesema kuwa licha ya maeneo ambayo wanayafanyia
kazi hata GGM wana maeneo yao tofauti na sehemu walizopewa wananchi lakini bado
athari za kimazingira zinawaathiri sana mfano ulipuaji wa maeneo mbalimbali.
Baadhi ya wananchi walioongea na waandishi wa habari
hizi wamesema kuwa wanafikiria kuishitaki kamati hiyo ambayo iliundwa kwa ajili
ya kutengua usajili wa kijiji hicho.
“Hata waziri
mkuu Mizengo Pinda alishawahi kufika hapa kwa nyakati tofauti tofauti akijua ni
kijiji leo hii wanatuambia tunakaa kwenye hifadhi na leseni ya GGM kwa hiyo GGM
anaruhusiwa kukaa kwenye hifadhi ila wananchi hawarusiwi? “,alihoji mmoja
wananchi hao.
“Kama tulishapewa na leseni za uchimbaji 20 na
serikali hiyo hiyo ,ina maana hata naibu waziri wa madini alikuwa hajui au kuna
kitu gani wanachokitafuta hawa watu?”,mwingine alihoji.
Mmoja wa wajumbe waliokuwa kwenye kamati hiyo ambaye
si msemji wa kamati alisema kuwa....
“sisi
tulimaliza kazi yetu ya kugawana raslimali za halmashauri na hayo yote yalikuwa
yakifanyika kwa mujibu wa hadidu za rejea tulizopewa kwa hiyo tulimaliza kazi
sisi”.
Aliongeza kuwa hali hiyo inaweza kuleta mgongano kati
ya wananchi wanaoishi kijiji hicho na baadhi ya viongozi ambao walikuwemo
kwenye kamati hiyo huku wakijua kuwa ni kijiji kilichosajiliwa lakini wao
wanasema kuwa hakina usajili na wameenda mbali zaidi wakitaka waziri mkuu
aingilie suala hili ili wananchi wajue hatma yao ya makazi ndani ya kijiji
hicho.
Na Valence Robert-Geita
Social Plugin