Ndege
wa ajabu wakiwa juu ya miti katika Kisiwa cha Musira kilichopo Manispaa
ya Bukoba mkoani Kagera. Ndege hao wamezua hofu kwa wakazi kutokana na
kinyesii chao kudhuru mifugo na ndege.
NDEGE
wa ajabu wanaosadikiwa kutoa kinyesi chenye sumu kali, wamevamia Kisiwa
cha Musira kilichopo Manispaa ya Bukoba na kusababisha vifo vya mifugo
na ndege wafugwao, huku ukali wa sumu hiyo ukisababisha kutoboka mabati
ya nyumba zilizopo kisiwani humo.
Ndege
hao wanaoaminika kuvamia kisiwa hicho mwezi mmoja uliopita tayari
wameshasababisha vifo vya kuku 516 na mbuzi 12 wanaodaiwa kugusa au kula
kinyesi chao.
Hata hivyo, bado haijafahamika ndege hao wanatokea nchi
gani.
Akithibitisha
habari hizo, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kanali Mstaafu, Fabian Massawe
alisema Serikali ilipata taarifa hizo kupitia Kamati ya Ulinzi na
Usalama ya Wilaya na baadaye kuundwa timu ya kutafuta taarifa za awali
za tatizo hilo.
Massawe
alisema ndege hao, pamoja na kusababisha vifo vya mifugo na ndege
wafugwao pia baadhi ya miti katika kisiwa hicho imekauka na mabati
kutoboka inapotokea kinyesi chao kitaangukia kwenye paa za nyumba zao.
Pia
Massawe alisema kuwa, taarifa ya kuwapo kwa ndege hao katika Kisiwa cha
Musira, ilifikishwa kwa Naibu Waziri wa Afya, Dk. Kebwe Stephene Kebwe
aliyekuwa mkoani humo wiki iliyopita na kuwa suala la kuwapo kwa ndege
hao siyo la ghafla kwa kuwa walikuwapo hapo awali.
Dk.
Kebwe alisema wizara imetuma wataalamu kuchunguza tatizo hilo na kuwa
wizara hiyo itaangalia ukubwa wa tatizo hilo linavyoweza kuwaathiri
wananchi.
Hata
hivyo, alisema suala hilo pia linahitaji ufuatiliaji kutoka Wizara ya
Mifugo na Uvuvi na Dk. Munda Elias alikwishawasili kwa ajili ya
uchunguzi na kuthibitisha kuwa tayari kinyesi cha ndege hao kimepelekwa
maabara kwa ajili ya uchunguzi na Mkoa unasubiri matokeo ya utafiti
huo.
Naye
Ofisa Tarafa wa Rwamishenye, Abdon Kahwa akizungumza kwa niaba ya Mkuu
wa Wilaya hiyo, Ziporah Pangani alisema tayari Serikali imechukua hatua
za kupiga marufuku kupeleka au kusafirisha mifugo kutoka kisiwani humo
kwenda maeneo mengine kwa hofu ya kusambaa kwa sumu hiyo.
Pia
alisema ndege hao wameleta hofu kwa wakazi wa kisiwa hicho, kwani
kinyesi chao kinapodondoka kwenye bati hupata kutu na kutoboka, huku
kukiwa na hofu nyingine kwamba huenda mifugo nayo imeathiriwa.
via >>mwananchi