Tangu mimba inatungwa na kipindi chote cha ujauzito ni wakati
muhimu mno kwa mjamzito, lakini wakati muhimu zaidi ni wakati wa
kujifungua.
Yapo mambo muhimu ambayo yanapaswa kufanyika mara
mama mjamzito anapofikishwa kwenye chumba cha kujifungulia. Jina la
kituo lazima liandikwe kwenye sehemu yake kwenye kadi ya kliniki.
Tarehe na muda alioanza kupata uchungu na kulazwa,
chupa kupasuka au hapana. Umri wa mimba na kimo chake kwa wiki, mlalo
na kitangulizi cha mtoto pamoja na upimaji wa nyonga ni baadhi ya mambo
muhimu ya kuzingatia.
Upimaji sahihi wa nyonga hutoa taswira ya mwelekeo wa kujifungua kwa kulinganisha na makadirio ya ukubwa wa mtoto.
Ndani ya chumba cha kujifungulia ni lazima
viashiria vyote vya hatari wakati wa ujauzito vijulikane kwa
anayemhudumia mama wakati wa kumlaza kwa ajili ya kujifungua.
Viashiria hivi ni kidokezo A au B katika ujauzito
kama tulivyoona kwenye makala zilizotangulia, chupa kupasuka bila
uchungu, uchungu kabla ya wiki 34, saa 12 kupita tangu uchungu kuanza,
damu kutoka, mapigo ya moyo ya mtoto kuwa juu ya 160 au chini ya 120 kwa
dakika pamoja na kubadilikabadilika, kifafa cha mimba au presha kuwa
zaidi ya 140/90 na upungufu wa damu chini ya gramu 8.5 kwa desilita na
homa juu ya kiwango cha 38 sentigredi.
Mambo haya yanapogundulika kwenye kituo kidogo cha
afya, mhudumu anapaswa kumpeleka kituo kikubwa au hospitali na daktari
kupewa taarifa mara moja.
Ndani ya chumba cha kujifungulia, maendeleo ya uchungu husimamiwa kwa grafu maalumu (partogram).
Matumizi sahihi ya grafu hii ni njia mojawapo ya
kupata matokeo mazuri kwa uzazi salama kwani huonyesha kama mama
anaendelea vizuri au kuna viashiria vya hatari vinajitokeza, hivyo kutoa
nafasi kwa mhudumu kuchukua hatua mapema kabla madhara hayajatokea.
Grafu hii huratibu mambo makuu matano amabyo ni
mapigo ya moyo wa mtoto aliyeko tumboni, kufunguka kwa njia ya uzazi
sehemu ya shingo (cervix) ili kuruhusu mtoto kupita, kushuka kwa mtoto
hadi kutoka, kiwango cha maumivu ya uchungu kila baada ya dakika 10 na
hali ya afya ya mama kwa ujumla.
Uratibu wa mambo haya makuu hufanywa kwa pamoja au kwa mpangilio kutegemea na hali ya kujifungua aliyokuja nayo mzazi mtarajiwa.
Mzazi anaweza kupokelewa wakati uchungu
haujakazana wala njia kufunguka au uchungu umekolea na njia kufunguka
zaidi ya sentimita tatu.
via>>mwananchi
|
Social Plugin