HOTUBA YA RAIS WA
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA,
MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE,
WAKATI WA KULIHUTUBIA BUNGE
MAALUM LA KATIBA, TAREHE 21 MACHI, 2014, DODOMA
Mheshimiwa
Samuel Sitta, Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba;
Mheshimiwa
Dkt. Mohamed Gharib Bilal, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa
Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi;
Mheshimiwa
Mizengo Peter Pinda, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa
Maalim Seif Sharif Hamad, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar;
Mheshimiwa
Balozi Seif Ali Iddi, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Mheshimiwa
Anne Semamba Makinda; Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano;
Mheshimiwa
Pandu Ameir Kificho, Spika wa Baraza la Wawakilishi na Mwenyekiti wa Muda wa
Bunge Maalum la Katiba ;
Mheshimiwa
Rashid Othman Chande, Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa
Othman Makungu, Jaji Mkuu wa Zanzibar;
Viongozi
Wakuu Wastaafu;
Waheshimiwa
Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba;
Waheshimiwa
Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba;
Wageni
waalikwa;
Pongezi
Nakushukuru
sana Mheshimiwa
Mwenyekiti kwa kunipa fursa ya kuja kuzungumza na Waheshimiwa Wajumbe wa Bunge
letu Maalum la Katiba katika siku hii muhimu na ya kihistoria kwa nchi yetu. Nimekuja kuwatakia heri na naungana na
Watanzania wenzetu wote kuwaombea baraka za Mwenyezi Mungu, ili muweze kuifanya
kazi yenu kwa utulivu, hekima, umakini mkubwa na kuimaliza kwa salama na kwa
mafanikio yanayoyatarajiwa na Watanzania.
Natoa pongezi nyingi kwako na
kwa Makamu wako kwa kuchaguliwa kwenu kuongoza Bunge hili maalumu na la
kihistoria. Ushindi mkubwa mliopata ni
kielelezo tosha cha imani kubwa na matumaini waliyonayo Wajumbe wenzenu kwenu. Matumaini
yao ndiyo matumaini ya Watanzania wote, kwamba
mtaliongoza vizuri Bunge hili, ili liweze kutimiza kwa ufanisi mkubwa jukumu lake muhimu sana katika historia ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Niruhusu pia niwapongeze kwa dhati
Wajumbe wote wa Bunge Maalum la Katiba kwa bahati ya aina yake waliyopata ya
kutunga Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Fursa hii hutokea mara chache sana katika historia ya nchi yo yote na watu
wake. Mkifanikiwa kuipatia nchi yetu
Katiba nzuri majina yenu yataandikwa kwa wino wa dhahabu, katika kumbukumbu za
historia ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ni matarajio ya Watanzania
kuwa mtatunga Katiba itakayokubalika na wengi.
Katiba inayotekelezeka. Katiba
itakayoimarisha Muungano wetu kwa kuondoa changamoto zilizopo sasa. Katiba itakayoipa nchi yetu mfumo bora wa kuongoza
na kuendesha mambo yetu. Katiba
itakayoimarisha umoja, upendo, ushirikiano na mshikamano miongoni mwa wananchi
wa Tanzania,
licha ya tofauti zao za asili za upande wa Muungano na maeneo watokako, au tofauti
za jinsia, rangi, kabila, dini na ufuasi wa vyama vya siasa. Katiba itakayodumisha amani, usalama na
utulivu nchini. Katiba itakayostawisha zaidi
demokrasia, haki za binadamu, utawala wa sheria, utawala bora na kudhibiti
maovu.
Na, mwisho ingawaje siyo
mwisho kwa umuhimu, Katiba itakayoweka mazingira mazuri kwa uchumi wa nchi
kukua, na wananchi wengi kunufaika sawia na maendeleo yatayopatikana.
Historia
ya Katiba Nchini
Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa
Wajumbe;
Hii itakuwa mara ya tatu
tangu kuzaliwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Aprili 26, 1964, kwa nchi
yetu kuwa na mchakato wa kutunga Katiba mpya.
Mara ya kwanza ilikuwa mwaka 1965 ilipotungwa Katiba ya Muda na mara ya
pili ni mwaka 1977 ilipotungwa Katiba ya Kudumu tuliyonao sasa. Tofauti na mara mbili zilizopita, safari hii
mchakato unahusisha watu wengi zaidi. Wananchi
wameshiriki moja kwa moja kutoa maoni yao
kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, na ndio watakaofanya uamuzi wa mwisho kuhusu
Katiba mpya kwa kura ya maoni. Wananchi
pia walipata nafasi ya kuchagua Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya yaliyojadili
Rasimu ya Kwanza ya Katiba. Pia walipata nafasi ya kutoa maoni yao kupitia Mabaraza ya Katiba
ya taasisi. Katika Bunge hili wapo
wananchi 201 kutoka makundi
mbalimbali.
Katika mchakato wa kutunga
Katiba za mwaka 1965 na 1977 kulikuwapo Tume za Kuandaa Rasimu na Bunge Maalum
la Katiba kama ilivyo katika mchakato
huu. Hata hivyo, kwa Katiba zilizopita
Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano pekee ndio waliounda Bunge Maalum. Safari hii Bunge Maalum linajumuisha Wabunge,
Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na wananchi 201 wanaotoka kwenye jamii,
wakiwakilisha asasi na makundi mbalimbali ya Watanzania kutoka Zanzibar na Tanzania Bara. Mchakato wa sasa utaishia kwenye kura ya
maoni itakayoshirikisha wananchi wote wa Tanzania wanaoruhusiwa kupiga
kura. Michakato iliyopita iliishia Bunge
Maalum pekee.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Tangu kutungwa kwake, tarehe
25 Aprili, 1977, mpaka sasa Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977
imefanyiwa mabadiliko takriban mara 14.
Mabadiliko hayo yalitokana na kufanyika au kutokea kwa mabadiliko muhimu
ya kiuchumi, kisiasa na kijamii katika nyakati mbalimbali hapa nchini na katika
Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Kwa ruksa yako naomba nitaje
baadhi ya mabadiliko yaliyofanywa:-
1. Mabadiliko
ya 1979 yaliunda Mahakama ya Rufani ya Tanzania kufuatia kufa kwa Mahakama
ya Rufani ya Afrika Mashariki baada ya kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika
Mashariki mwaka 1977.
2. Mabadiliko
ya mwaka 1980 yalifanyika baada ya kutungwa kwa Katiba ya Zanzibar, hivyo kulazimu Katiba hiyo
kutambulika kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano.
3. Mabadiliko
ya mwaka 1984 yaliweka utaratibu wa ukomo wa vipindi vya Urais ambao haukuwepo
kabla ya hapo. Aidha, masuala ya Haki za
Binadamu (Bill of Rights) yaliingizwa kwa mara ya kwanza katika Katiba. Vilevile,
Mahakama ya Rufani ya Tanzania
na mambo mengine ya iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki yaliongezwa katika
Orodha ya Mambo ya Muungano.
4. Mwaka
1992, yalifanyika mabadiliko yaliyoanzisha Mfumo wa Vyama Vingi vya Siasa
badala ya ule wa Chama kimoja uliokuwepo tangu 1965. Pia utaratibu wa uchaguzi wa Rais na Wabunge
ulirekebishwa ili uendane na mfumo wa vyama vingi vya siasa. Vilevile utaratibu wa kuwa na viti maalum vya
wanawake katika Bunge ulianzishwa. Wakati ule ilikuwa asilimia 15 ya Wabunge
wote. Aidha, kwa mara ya kwanza katika
historia ya nchi yetu Bunge lilipewa mamlaka ya kumwajibisha Rais na Waziri
Mkuu kupitia kura ya kutokuwa na imani.
5. Mabadiliko
ya mwaka 1994 yaliweka mfumo mpya wa kumpata Makamu wa Rais kupitia Mgombea
Mwenza.
6. Mwaka
2000 na 2005, pamoja na mambo mengine yalifanyika mabadiliko yaliyopanua wigo
wa Haki za Binadamu na kuongeza
uwakilishi wa wanawake.
Umuhimu
wa Mabadiliko ya Katiba
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kufanyika kwa mabadiliko hayo
kunathibitisha utayari wa Serikali kufanya mabadiliko kila ilipoonekana inafaa
kufanya hivyo. Pamoja na kufanya yote hayo
na Serikali kuwa na msimamo huo, kumekuwepo na madai yaliyokuwa yanajirudia ya
kutaka Katiba ya Tanzania
iandikwe upya. Wako watu walioimithilisha
Katiba yetu na nguo yenye viraka vingi mno kiasi kwamba ingefaa kununua mpya
badala ya kuendelea kuivaa.
Madai ya kutaka Katiba mpya yalipazwa sauti
baada ya kuanza kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa. Wapo waliokuwa wanadai Katiba mpya kwa imani,
eti kwamba, itawawezesha kuishinda CCM.
Lakini, si hayo tu, hata katika mchakato wa Serikali zetu mbili kushughulikia
kero za Muungano, imedhihirika kuwa baadhi ya changamoto zilikuwa zinahitaji mabadiliko
ya Katiba ili kuzipatia ufumbuzi wa uhakika na wa kudumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kwa kutambua ukweli huo na baada
ya kushauriana na kukubaliana na viongozi wenzangu wakuu wa Chama tawala na
Serikali zetu mbili wakati ule, ndipo tarehe 31 Desemba, 2010, nikatangaza dhamira
ya kuanzisha mchakato wa kutunga Katiba mpya.
Nilieleza siku ile kuwa katika mchakato huo tutakuwa na ushirikishwaji
mpana wa wananchi wa Tanzania
kwa makundi yao
ya jinsia, dini, siasa na shughuli wazifanyazo kujipatia riziki na kwa maeneo
wanayotoka katika pande zetu mbili za Muungano.
Mchakato
wa Katiba Mpya
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Tarehe 16 Machi, 2011 Baraza la Mawaziri liliridhia
kutungwa kwa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya kuliongoza taifa katika mchakato
wa kutunga Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tarehe
18 Novemba, 2011 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha Muswada wa Sheria
ya Mabadiliko ya Katiba. Kwa mujibu wa Sheria hiyo, mchakato wa kutunga Katiba
Mpya ulikuwa unaanza kwa kuunda Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Tume hiyo imepewa
jukumu la kusikiliza maoni ya wananchi mmoja mmoja na kwa makundi yao ya maslahi, taasisi
zao na kupitia Mabaraza ya Katiba.
Mwishowe Tume imetakiwa kutengeneza Rasimu ya Katiba mpya itakayofikishwa
kwenye Bunge Maalum la Katiba kujadiliwa na Katiba mpya kutungwa. Mchakato wa Katiba utahitimishwa kwa wananchi
kupiga kura ya maoni ya kuamua kama
wanaikubali au kuikataa Katiba mpya.
Tarehe 6 Aprili, 2012
nilifanya uteuzi wa Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kuwaapisha tarehe
13 Aprili, 2012. Tume ilianza kazi
tarehe 2 Mei, 2012 na kuikamilisha kwa mafanikio, hatua zote zilizoihusu na
kukabidhi kwangu na kwa Rais wa Zanzibar,
Taarifa ya Tume na Rasimu ya Katiba tarehe 30 Desemba, 2013. Kitendo cha Mwenyekiti wa Tume, Mheshimiwa
Joseph Warioba kuwasilisha Rasimu hiyo mbele ya Bunge hili tukufu tarehe 18
Machi, 2014, kinahitimisha rasmi kazi ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Kazi inayofuatia ni ya Bunge hili kujadili,
kuamua na kutunga Katiba mpya. Baada ya
hapo Katiba mpya itafikishwa kwa wananchi kwa uamuzi wa mwisho kwa njia ya kupiga
kura ya NDIYO au HAPANA.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Rasimu ya Katiba ilichapishwa
kwenye gazeti la Serikali na magazeti mengine yanayosomwa na wananchi kama ilivyoagizwa katika Kifungu cha 20(2) cha Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba. Pamoja na hayo,
Taarifa ya Tume na Rasimu ya Katiba viliwekwa wazi kwenye tovuti ya Tume kwa
kila mtu kusoma. Inafurahisha kuona kuwa
watu wengi wameisoma Taarifa ya Tume na Rasimu ya Katiba na kumekuwa na mjadala
mpana kuhusu nyaraka zote hizo muhimu. Watu wengi wametoa maoni yao na wanaendelea kufanya
hivyo. Kwa maoni yangu hili ni jambo
jema sana na ni kielelezo thabiti kuwa
demokrasia imestawi na inazidi kuota mizizi Tanzania. Pia, kwamba, Watanzania wako huru kushiriki
na kutoa maoni yao
kwa mambo yanayowahusu.
Pongezi
kwa Tume
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kwa mara nyingine tena narudia
kutoa pongezi za dhati kwa Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya
uongozi wa Mheshimiwa Jaji Joseph Warioba akisaidiwa na Mheshimiwa Jaji
Augustino Ramadhani, kwa kazi kubwa na nzuri waliyofanya. Kazi yao haikuwa rahisi hasa ukizingatia ukubwa wa
nchi yetu, wingi wa watu wake, utitiri wa taasisi na pigo la kumpoteza Mjumbe
mwenzao muhimu Dkt. Sengondo Mvungi aliyetangulia mbele ya haki katikati ya
mchakato.
Pamoja na hayo, kwa bidii
kubwa Wajumbe wa Tume wameweza kutembelea mikoa yote nchini na kuwafikia watu 351,644 waliotoa maoni yao kwa mdomo na kwa maandishi. Halikadhalika, walipokea na kuchambua maoni 772,211
kutoka kwa wananchi na taasisi mbalimbali.
Baada ya kupokea maoni ya wananchi, kufanya utafiti na kwa kutumia
maarifa na uzoefu wao, Wajumbe wakafanya kazi ngumu, kuliko yote, ya
kutengeneza Rasimu ya Katiba iliyoko mbele ya Bunge hili. Ni kweli kwamba Wajumbe hawakuweza kuwafikia
wananchi wote wa Tanzania,
lakini wameweza kuwafikia wananchi wengi, ambao kwa kiasi kikubwa wanawakilisha
taswira na mitazamo mipana ya jamii yetu.
Baadhi
ya Masuala Yaliyojitokeza Katika Mjadala wa Mapendekezo ya Tume
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Tume imefanya kazi nzuri,
yenye thamani kubwa na ya manufaa kwa taifa la Tanzania. Rasimu imeandikwa vizuri na kwa weledi wa hali
juu. Tume imetoa mapendekezo ambayo kwa
kiasi kikubwa yanahuisha na kuboresha Katiba ya nchi yetu, kwa namna ya
pekee. Katiba inayopendekezwa,
imejumuisha dhana na mambo kadhaa mapya yanayokwenda vyema na wakati tulionao
na kuweka msingi mzuri kwa huko mbele tuendako.
Kwa taratibu za kawaida za marekebisho ya Katiba tuliyonayo, isingekuwa
rahisi kuingiza mambo mengi mapya kiasi hiki.
Wajumbe
Wana Kazi Kubwa
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Waheshimiwa Wajumbe;
Rasimu
ya Katiba ni kitabu kikubwa kilichosheheni mambo mengi. Kina kurasa 106, sura 17 na ibara 271.
Wajumbe wa Bunge hili mnatakiwa kusoma na kuelewa vizuri kila
kilichoandikwa ili muweze kufanya uamuzi ulio sahihi. Mnawajibika kuchambua kwa kina na umakini
mkubwa kila kilichomo, sura kwa sura, ibara kwa ibara, sentensi kwa sentensi na
hata neno kwa neno. Hamna budi kujiridhisha
kuhusu uandishi wa vifungu vya Rasimu ya Katiba na kufaa kwa dhana mbalimbali zilizoingizwa na
kujengeka katika Rasimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kile ambacho Wajumbe mtaona
kinastahili kuboreshwa au kurekebishwa au kufutwa msisite kufanya hivyo ili
Watanzania wapate Katiba iliyo bora.
Msipofanya hivyo kuna hatari ya kupata Katiba ambayo ni ngumu
kuitekeleza. Aidha, tunaweza kuwa na Katiba
ambayo itanung’unikiwa na watu wengi na kusababisha madai ya kutaka ifanyiwe
marekebisho muda mfupi baada ya kupitishwa.
Bunge hili linao wajibu maalum wa kuzuia balaa hilo lisitokee katika nchi yetu. Ngazi mbalimbali zilizowekwa katika mchakato
huu ni kama chujio la kuepusha hali hiyo isitokee. Kile ambacho hakikuonekana katika hatua moja
kitaonekana katika hatua inayofuata na kurekebishwa. Nawaomba fursa mliyonayo muitumie vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Nimekwishaeleza
kuwa moja ya jambo mnalotegemewa kufanya ninyi wenzetu mliopewa dhamana ya
kutunga Katiba ya nchi yetu ni kujiridhisha na uandishi wake. Yapo maoni yaliyotolewa kuhusu uandishi
ambayo naomba myatafakari na kuamua ipasavyo.
Kwa mfano, kuna baadhi ya vifungu vya Katiba vinayopendekezwa vimekuwa
na mambo mengi mno kuliko inavyostahili Katiba kuwa (too prescriptive). Pia kuna mawazo kwamba baadhi ya mambo hayangetakiwa
kuwa katika Katiba bali yawe kwenye Sheria zinazotafsiri utekelezaji wa Katiba
yenyewe.
Yako mambo yaliyotajwa kwenye
Katiba ambayo yanatakiwa kuelezwa wazi kuwa mtu hatakwenda mahakamani kuidai
Serikali impatie (non justiciable). Mambo yaliyotajwa kwenye Katiba ni mazuri na
yanavutia, lakini lazima yaendane na uwezo wa nchi na uchumi wake
kuhimili. Simaanishi kwamba tuyatoe
kwenye Katiba, bali yabakie kama dhamira pale
uwezo wa nchi utakaporuhusu yatekelezwe.
Tusipofanya hivyo, kuna hatari ya Serikali kujikuta inalaumiwa au hata
kufikishwa mahakamani kila wakati kwa
madai ya jambo moja au jingine ambayo haina uwezo nayo. Ni muhimu sana
mambo kama hayo muyatazame ili tusije kuwa na
Katiba ambayo ni ngumu kutekeleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Yapo pia maoni kuwa baadhi ya
vifungu vina upungufu katika uandishi wake, hivyo kuhitaji kufanyiwa marekebisho. Isipofanyika hivyo kunaweza kuwepo athari na
nyingine zinaweza kuwa mbaya. Kwa mfano,
Ibara ya 2 ya Rasimu inayotambulisha eneo na mipaka ya nchi yetu. Ibara hiyo inasomeka kuwa “Eneo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni eneo lote la Tanganyika likijumuisha sehemu yake ya bahari na
eneo lote la Zanzibar
likijumuisha sehemu yake ya bahari”.
Maelezo hayo yameacha
kutambua, kwa upande wa Tanzania Bara, sehemu yetu ya maziwa na mito ambayo ni kubwa sana. Kwa nini tuache kuitaja? Je hatutoi nafasi kwa nchi tunazopakana nazo
siku moja wakaja kupora sehemu zetu hizo na sisi kukosa utetezi kwa kuwa hata
Katiba yetu haikuyatambua maeneo hayo kuwa ni yetu? Hili ni jambo kubwa ambalo Bunge hili lazima mlirekebishe. Wakati
ndiyo huu hakuna mwingine.
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Jambo
jingine kuhusu uandishi ni mgongano kati ya pendekezo la msingi la Tume la kuwa
na muundo wa Serikali tatu na majukumu ya Serikali ya Muungano ambayo kimsingi
ni majukumu ya Serikali za nchi washirika.
Katika Rasimu hii malengo ya
taifa yameainishwa na Serikali ya Muungano inatakiwa kuhakikisha kuwa malengo
hayo yanatekelezwa na itoe taarifa Bungeni.
Katika mfumo wa Serikali tatu unaopendekezwa na Tume masuala yahusuyo uchumi
na maendeleo ya jamii kama vile kukuza kilimo,
ufugaji, uvuvi, viwanda, biashara, pembejeo, elimu, hifadhi ya jamii na
kadhalika yako chini ya mamlaka ya Serikali za nchi washirika. Mamlaka ya Serikali ya Muungano ni kwa mambo
saba tu yafuatayo:- Katiba na Mamlaka ya Jamhuri ya Muungano, Ulinzi na Usalama
wa Jamhuri ya Muungano, Uraia na Uhamiaji, Sarafu na Benki Kuu, Mambo ya Nje,
Usajili wa Vyama vya Siasa, Ushuru wa Bidhaa na Mapato yasiyo ya kodi
yatokanayo na Mambo ya Muungano.
Kwa Rasimu kupendekeza muundo
wa Serikali tatu na kuipa Serikali ya Muungano majukumu ambayo haina mamlaka
nayo, ni kuzusha utata na migongano kati ya Serikali ya Muungano na nchi
washirika. Mkichagua mfumo wa Serikali
tatu, inawalazimu muyaondoe mambo hayo kwani Serikali ya Muungano haistahili
kuyatekeleza na wala haina uwezo wa kuweka masharti kwa Serikali za nchi
washirika kwa mambo yaliyo kwenye mamlaka ya nchi hizo. Lakini kama mtaamua tuendelee na muundo wa
Serikali mbili, mambo haya mazuri yanatekelezeka na Serikali ya Muungano bila
ya matatizo. Katika uandishi wa Rasimu Utumishi
katika Serikali ya Muungano haumo katika Orodha ya Mambo ya Muungano. Ni lazima liwemo. Hayo ni baadhi tu ya masuala yahusuyo
uandishi katika Rasimu. Naamini mkiisoma
Rasimu kwa makini mnaweza kuyagundua mengineyo.
Dhana
Mpya
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Katika Rasimu kuna dhana mpya
na mambo mapya kadhaa yaliyoingizwa ambayo yanabadili utaratibu wa sasa wa uendeshaji
wa nchi na mambo mbalimbali. Nawaomba
mfanye uchambuzi wa kina kwa kila kinachopendekezwa na kujiridhisha kuhusu
kufaa kwake na manufaa yake. Fanyeni hivyo ili tujihakikishie kuwepo kwa mambo
mazuri na uendeshaji mzuri wa shughuli katika taifa letu changa.
Mambo ni mengi na kwa ufinyu
wa muda sitaweza kuyazungumzia yote. Niruhusuni
nizungumzie baadhi ya dhana na mambo mapya yaliyomo katika Rasimu. Jambo la kwanza, kwa mfano, linahusu Ibara ya
128 (2)(d) inayoleta dhana ya “Mbunge kupoteza Ubunge iwapo atashindwa kufanya
kazi za Mbunge kwa miezi sita mfululizo
kutokana na maradhi au kizuizi ndani ya gereza”.
Watu hawana tatizo na Mbunge kuwa kizuizini ndani
ya gereza kama amepatikana na hatia Mahakamani
na kuhukumiwa kifungo. Lakini, isijekuwa
yuko rumande kwa tuhuma akisubiri kesi kusikilizwa. Je akija kuonekana hana hatia na
kuachiliwa? Naungana na wale wanaoshauri
kuwa jambo hili lifafanuliwe vizuri na kutambua Mbunge kutiwa hatiani na kupata
adhabu ya kifungo cha kipindi hicho. Ni bora ifanyike hivyo sasa ili kuondoa
mikanganyiko. Hakuna haja ya kusubiri mpaka
jambo hili lije kufafanuliwa baadaye kwa Sheria itakayotungwa na Bunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kwa upande wa mtu kupoteza
Ubunge kwa sababu ya “kuugua kwa miezi
sita mfululizo” ni maoni ya watu wengi kuwa huu ni ukatili ambao
haustahili
kufanywa na Katiba. Kuugua ndiyo
ubinadamu na wakati mwingine Mbunge anaweza kupata ajali akiwatumikia
wananchi
wa Jimbo lake. Anaweza kuugua kwa miezi
sita au zaidi na kupona kabla ya kipindi chake cha Ubunge kufika
mwisho. Kwa nini awekewe ukomo wa miezi sita? Katiba ya mwaka 1977
tunayotumia sasa haina
sharti hilo. Watu wanauliza hoja na haja ya kuwa na sharti
hili kwenye Katiba mpya ni ipi? Wanasema
kwa kweli anachostahili Mbunge huyu kufanyiwa ni kuuguzwa afya yake iimarike
ili aendelee kutumikia watu wake, na siyo kupoteza uongozi wake. Tusiwatie watu kishawishi cha kukatiza
matibabu ili kukwepa sharti hilo. Ni vyema jambo hili mkalitazama kwa makini,
na muone kama linastahili kuwepo au hapana.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Katika Rasimu hii imeingizwa
dhana mpya ya kuweka ukomo wa vipindi vitatu kwa Wabunge. Tena mapendekezo haya hayasemi vipindi vitatu
mfululizo au la!. Jambo hilo limezua mjadala motomoto katika jamii. Ni vizuri mkajiridhisha juu ya sababu za
msingi na manufaa ya kufanya hivyo hapa Tanzania. Mazoea yetu na ya kwingineko duniani ni kuweka
ukomo kwa Wakuu wa Nchi kwa sababu nzuri na rahisi kuzielezea. Lakini, kuwawekea ukomo Wabunge ni jambo jipya
na huenda Tanzania
tukawa wa kwanza. Nashawishika kuungana na
wale wanaopendekeza kuwa pengine ni mapema mno kuanzisha utaratibu huo hapa
kwetu.
Nachelea kuwa tutainyima nchi yetu fursa ya
kupata watu wenye maarifa na uzoefu mzuri wa uongozi kwa nafasi ya Ubunge au kwa
nafasi za uongozi wa Taifa bila ya sababu za msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Jambo lingine jipya
linalopendekezwa na Tume ni utaratibu wa kumuondoa Mbunge katikati ya kipindi
chake cha uongozi. Kwa hoja linaonekana
kuwa jambo jema lakini naomba athari zake mzitafakari vizuri. Kuna hatari ya kuanzisha
misuguano kwenye Majimbo na kuwaacha Wabunge wasifanye kazi zao kwa utulivu bali
wawe wanajihami dhidi ya wapinzani wao kuwatengenezea fitna za kuwatoa. Utaratibu unaopendekezwa wa Chama chake
kujaza nafasi ya Mbunge inapokuwa wazi katika mazingira hayo nao unaweza kuwa
ndicho kichocheo kikubwa cha vuguvugu la kumuondoa Mbunge. Walioshindwa kwenye kura ya maoni wanaweza
kufanya kazi ya kuwachimba wenzao mpaka waondoke. Jipeni muda wa kupima faida na hasa thamani
inayoongezwa na kuanzisha utaratibu huo.
Naomba tujiridhishe kama jambo hili
jipya lina tija. Hivi kupewa nafasi kila miaka mitano kurudi kwa wananchi
hakutoshi kumuondoa Mbunge ambaye watu wamemchoka?
Muundo
wa Muungano
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Jambo lingine kubwa lililopendekezwa na Tume
ambalo limevuta hisia za karibu watu wote nchini linahusu muundo wa Muungano
wetu kuwa wa Serikali tatu badala ya mbili za sasa. Pendekezo
hili limezua mjadala mkubwa tangu lilipotolewa katika Rasimu ya kwanza na
kurudiwa katika Rasimu ya pili. Wakati
mwingine mjadala umekuwa mkali na wa hisia kali kwa kila upande.
Kwa kweli hili ndilo jambo
kubwa kuliko yote katika Rasimu kwa sababu linapendekeza kuanzishwa kwa muundo
na mfumo mpya wa kuendesha nchi yetu. Hii
ndiyo agenda mama ya Bunge hili ambayo kila Mtanzania anasubiri kwa hamu uamuzi
wenu utakuwa upi. Ombi langu kwenu ni
kuwa watulivu mnapojadili suala hili.
Epukeni jazba ili mfanye uamuzi ulio sahihi. Lazima mtambue uamuzi usiokuwa sahihi kwa
jambo hili una hasara kubwa. Tunaweza
kupoteza kitu tulichokijenga kwa gharama kubwa kwa nusu karne iliyopita. Tanzania inaweza kuwa nchi iliyojaa
migogoro na matatizo mengi ambayo hatunayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa
Wajumbe;
Kama
alivyoeleza Mwenyekiti wa Tume Mheshimiwa Jaji Joseph Sinde Warioba, mara
kadhaa, mjadala au madai ya kutaka muundo wa Serikali tatu si jambo jipya.
Ulikuwepo hata wakati wa mazungumzo ya kuunganisha nchi zetu mbili mwaka 1964. Ulikuwa kiini cha kuchafuka kwa hali ya hewa
ya kisiasa Zanzibar
mwaka 1984. Muundo huu uliwahi
kupendekezwa na Tume ya Nyalali mwaka
1992, ndiyo hoja ya G55 mwaka 1993 na umependekezwa pia na Tume ya Jaji Kisanga
ya mwaka 1998. Lakini mara zote hizo mapendekezo
hayo hayakukubaliwa.
Waasisi wa taifa letu, yaani Mwalimu Julius Nyerere, aliyekuwa Rais wa
Jamhuri ya Tanganyika wakati
ule na Sheikh Abeid Amani Karume, aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar wakati ule, waliamua kuchagua Muungano wa Serikali mbili tulionao
sasa. Walitoa sababu mbili kuu: “ni muundo unaoihakikishia Zanzibar
kuwa haimezwi na Tanganyika;
na pia unaiepusha Tanganyika
kubeba mzigo mkubwa wa kugharamia Serikali ya Tanganyika na ile ya Muungano”.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Natambua kuwepo kwa rai ya kutaka
Mwalimu Nyerere asitumiwe katika mjadala huu.
Nionavyo mimi ni vigumu kuacha kujadili fikra za Mwalimu Nyerere na
Sheikh Karume katika jambo hili. Wao
ndiyo wa mwanzo kujadili na kukubaliana kuwa mfumo wa Serikali mbili ndiyo bora
kwa nchi yetu. Iweje leo tunapozungumzia
kuubadili, mawazo yao
yawe hayafai kutumika au hata kuzungumzwa.
Hivi hasa mawazo ya nani pekee ndiyo bora zaidi kutumika? Tutakuwa hatuutendei haki mjadala huu na sisi
wenyewe tunaoshiriki katika mchakato huu.
Rai yangu kwenu ni kuwa mzitazame hoja zote kwa marefu na mapana yake ili
mpime kama zipo sababu za kuubadili muundo wa sasa wa Muungano wa Serikali
mbili na kuleta wa Serikali tatu. Na, kama
zipo mabadiliko hayo yaweje! Lazima mfanye uamuzi kwa utambuzi na hoja zenye
mashiko. (you must make an informed
decision).
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Tume imetoa sababu mbili
kubwa za kupendekeza muundo wa Serikali tatu.
Sababu ya kwanza ni kwamba ndiyo matakwa ya Watanzania wengi kote Zanzibar na Tanzania
Bara. Inaeleza kuwa idadi kubwa ya Watanzania
waliotoa maoni, yaani asilimia 60.2 wa
kutoka Zanzibar
wanaunga mkono muundo wa Serikali ya Mkataba, na asilimia 61.3 wa kutoka Tanzania
Bara wanaunga mkono muundo wa Serikali tatu.
Sababu ya pili ni kwamba muundo huo unatoa majawabu ya uhakika na
endelevu kwa changamoto za muundo wa sasa wa Serikali mbili zinazonung’unikiwa
na watu wa pande zetu mbili za Muungano.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Sababu hizi mbili kuu
zilizotolewa na Tume zimezua mjadala mkali katika jamii. Wapo wanaokubaliana na
Tume na wapo wasiokubaliana nayo. Wapo wanaosema
Tume imesema kweli kwamba Watanzania wengi wanaunga mkono muundo wa Serikali
tatu, hivyo muundo wa Serikali tatu hauepukiki.
Ndiyo matakwa ya wengi hivyo msemo wa Kiswahili usemao wengi wape
uheshimiwe.
Lakini wapo wanaodai kuwa takwimu
za Tume hazionyeshi ukweli huo. Wanasema
kuwa taarifa ya Tume imeonesha kuwa Watanzania
waliotoa maoni yao
kwa Tume kwa mdomo na maandishi walikuwa 351,664. Kati yao
ni wananchi 47,820 au sawa na asilimia 13.6 ndiyo waliokerwa na muundo
wa Muungano hivyo wakauzungumzia. Wananchi
303,844 au sawa na asilimia 86.4 muundo wa Muungano kwao
halikuwa tatizo, ndiyo maana hawakuuzungumzia kabisa. Wanahoji kuwa iweje leo asilimia 13.6 ya Watanzania wote waliotoa maoni wageuke kuwa ndiyo Watanzania
walio wengi!
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Wanasema pia, kwamba mbona
Taarifa ya Tume yenyewe, kuhusu takwimu (uk. 66 na 67), inaonesha kwamba kati
ya hao watu 47,820 waliotoa maoni
kuhusu Muungano, ni watu 17,280 tu ambao
ni sawa na asilimia 37.2 ndiyo waliotaka muundo wa Serikali tatu, asilimia 29.8 walitaka Serikali mbili, asilimia 25.3 walipendekeza Serikali ya
Mkataba na asilimia 7.7 walipendekeza
Serikali moja. Hii hoja ya Watanzania
wengi kutaka Serikali tatu msingi wake upi?
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Takwimu za Tume (uk. 57) zinaonyesha,
vilevile kuwa Tume ilipokea maoni 772,211. Kati ya hayo asilimia 10.4 tu ndiyo yaliyozungumzia muundo wa Muungano na asilimia 88.6 hayakuzungumzia Muungano
bali mambo mengine. Hivyo basi wanahoji pia
kwamba kama muundo wa Muungano ungekuwa ni jambo
linalowakera Watanzania wengi, lingedhihirika kwenye idadi ya watu waliotoa
maoni na kwenye idadi ya maoni yaliyotolewa.
Yote hayo hayakujitokeza. Waliouzungumzia Muungano walikuwa asilimia 13.6 tu ya watu wote waliotoa
maoni na maoni yanayohusu Muungano yalikuwa asilimia 10.4 ya maoni yote.
Hivyo basi, wanauliza “usahihi wa hoja ya Watanzania wengi kutaka
Serikali tatu uko wapi?”
Changamoto
za Muundo wa Serikali Mbili
Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa
Wajumbe;
Kama
nilivyokwishagusia awali, sababu ya pili ambayo Tume inatoa kuhusu kufaa kwa muundo
wa Serikali tatu ni kwamba mfumo huu unajibu changamoto nyingi za muundo wa
Serikali mbili. Tume imeainisha vizuri changamoto za muundo wa Serikali mbili. Kwa upande wa Zanzibar
wanalalamikia kile kinachoitwa Tanzania Bara kuvaa koti la Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania
na hivyo kutumia mamlaka ya Serikali ya Muungano kujinufaisha yenyewe. Fursa hiyo Zanzibar hainayo. Aidha, wanasema mipaka na mamlaka ya Serikali
ya Muungano kwa mambo ya Muungano, na kwa mambo ya Tanzania Bara haijaainishwa
vizuri ikaeleweka. Wazanzibari pia, wanazungumzia mkanganyiko kuhusu ugawanaji
wa mapato, na jinsi ya kuchangia shughuli za Muungano baina ya Serikali ya
Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Vilevile, wanalalamikia Rais wa Zanzibar
kuondolewa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano.
Aidha, kuna malalamiko kuwa orodha ya mambo ya
Muungano iliyoongezwa kutoka mambo 11 mwaka 1964 mpaka 22 mwaka 1992 imepunguza uhuru wa Zanzibar kwa mambo yake ya ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kwa upande wa Tanzania Bara,
Tume inaeleza kuwepo kwa manung’uniko kuwa Muungano wa Serikali mbili umepoteza
utambulisho wa kihistoria wa Tanganyika na fursa ya watu wa upande wa Tanzania
Bara kutetea maslahi yao ndani ya Muungano. Wanasema Zanzibar sasa imekuwa nchi
huru; ina bendera yake, wimbo wake wa taifa na Serikali yake. Aidha, wanasema Zanzibar
imebadili Katiba na kujitambulisha kama nchi na kuchukua madaraka ya Bunge la
Muungano, kwa vile Sheria zinazotungwa na Bunge lazima zipelekwe kwenye Baraza
la Wawakilishi kupata kibali cha kutumika Zanzibar. Wananchi wa Tanzania Bara pia wanalalamikia kutokuwa
na haki ya kumiliki ardhi Zanzibar wakati wenzao wa kutoka Zanzibar wanayo haki
hiyo Tanzania Bara. Na wao vilevile wananung’unikia
mkanganyiko kuhusu ugawaji wa mapato na jinsi ya kuchangia gharama za
uendeshaji wa shughuli za Muungano baina ya Serikali ya Muungano na Serikali ya
Zanzibar. Hizi ndizo baadhi ya changamoto
ambazo Tume inaona jawabu lake ili kuzitanzua ni kubadili muundo wa Muungano
kuwa wa Serikali tatu badala ya mbili za sasa.
Faida
za Muundo wa Serikali Tatu
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Tume ya Mabadiliko ya Katiba
imefafanua kwamba mfumo wa Serikali tatu utagawanya vizuri madaraka kati ya
mamlaka tatu za Muungano. Unawezesha
Washirika wa Muungano kubaki na utambulisho wao wa kihistoria na kiutamaduni na
hivyo, utawezesha kuondoa hisia za Zanzibar kumezwa na Muungano. Pia unawezesha
kila upande wa Tanzania kuendesha mambo yake yasiyo ya Muungano kadri wanavyoona
inafaa. Vile vile unaweza ukaleta ushindani wa kimaendeleo baina ya washirika
na hivyo kusaidia kukuza maendeleo ya nchi.
Faida
za Muundo wa Serikali Mbili
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Pamoja na kuainisha
changamoto za muundo wa Serikali mbili na kupendekeza kuwa muundo wa Serikali
tatu ndio utakaosaidia kuzitatua, Tume haikuacha kutambua manufaa na mchango
muhimu uliotolewa na muundo wa Serikali mbili kwa nchi yetu. Tume inasema kuwa muundo wa Serikali mbili
unapunguza gharama za uendeshaji wa shughuli za umma. Umesaidia kujenga
uhusiano na ushirikiano mzuri katika nyanja mbalimbali baina ya wananchi wa
pande zetu mbili za Muungano. Umezuia mkubwa
kummeza mdogo; na umedumisha Muungano mpaka kuufikisha hapa ulipo tangu
kuasisiwa kwake takriban miaka 50 iliyopita (1964). Aidha, umesaidia kudumisha amani, umoja na
utulivu hapa nchini.
Changamoto
za Muundo wa Serikali Tatu
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Pamoja na kuelezea ubora wa muundo wa Serikali
tatu kama jawabu kwa changamoto za Serikali mbili, Tume inakiri kuwa hata muundo
huu nao una changamoto zake. Kwanza
kabisa, Taarifa ya Tume inaeleza kuwa kutakuwa na gharama kubwa za uendeshaji
wa shughuli za umma. Mheshimiwa Jaji
Joseph Warioba alitutoa hofu kuhusu gharama ingawaje mwaka 1993, Mwalimu alikuwa
na mawazo tofauti. Alisema kwamba: “watu …wanaodhani kuwa gharama ya Serikali yo yote kati ya hizo ingekuwa
ndogo, (Waulizeni Wazanzibari) na wala
gharama ya Serikali ya Shirikisho isingekuwa ndogo hata bila gharama ya mambo
yasiyo ya Shirikisho”. Ni matumaini yangu kwamba katika mjadala wenu
mtajipa nafasi ya kulitafakari suala hili kubwa na nyeti.
Tume imesema pia kwamba, Muundo
huu, unaweza kuibua tatizo la uchangiaji wa gharama za uendeshaji wa shughuli
za umma baina ya nchi washirika. Vilevile,
kuna uwezekano wa kuwepo sera zinazokinzana au kutofautiana juu ya masuala ya
msingi ya nchi na kuzua mgogoro kati ya washirika wa Muungano na baina ya nchi
washirika na Serikali ya Muungano. Aidha, upo uwezekano mkubwa kwa muundo huu kuleta
tofauti za kimaendeleo baina ya pande mbili za Muungano kutokana na kila upande
kuwa na sera na mipango tofauti.
Tume pia imeelezea hatari ya
muundo wa Serikali tatu kukuza hisia za utaifa (nationalistic feelings) kwa nchi washirika, hivyo kuweza kudhoofisha
Muungano. Muundo huu pia unaweza kuleta
misuguano (paralysis and deadklocs in
decision making) katika kufanya uamuzi juu ya masuala muhimu ya
kitaifa. Changamoto hizo si tu zinaweza
kuwa tishio kwa ustawi wa Muungano bali pia hata uhai wake. Kwa ajili hiyo kuchagua muundo wa Serikali
tatu kuna maana ya kufanya kazi ya ziada ya kuzikabili changamoto hizi ili
zisiue Muungano wenyewe. Changamoto
ambazo si ndogo hata kidogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Wanaounga
mkono muundo wa Serikali mbili wanasema kuwa kwa mlolongo huu wa changamoto
zilizoainishwa na Tume yenyewe, unadhihirisha kuwa muundo wa Serikali tatu hautapunguza
matatizo ya Muungano wetu bali utayaongeza maradufu kuliko ilivyo sasa. Wanakiri kuwepo kwa changamoto katika muundo
wa sasa wa Muungano. Hata hivyo, wanaamini
zinaweza kushugulikiwa na kupatiwa ufumbuzi bila ya kuhitaji kuwa na Serikali
ya tatu. Wanatoa mifano kadhaa ya jinsi Serikali zetu zilivyoshughulikia
changamoto za Muungano katika kipindi cha uhai wake na mafanikio
yaliyopatikana.
Katika kushughulikia kero za
Muungano, Serikali zetu mbili ziliunda Tume ya Shelukindo mwaka 1992 na Kamati
ya Pamoja ya Serikali zetu mbili mwaka 1993. Mambo mengi yaliyoainishwa katika
Tume ya Shelukindo na Kamati ya Pamoja yameshughulikiwa na kupatiwa ufumbuzi. Kwa upande wa kero zilizoelezwa kwenye Tume
ya Shelukindo, ilipofikia mwaka 2006 yalikuwa yamebakia mambo 13 kati ya 31. Kwa jumla, kwa kero zilizoibuliwa
na Tume ya Shelukindo na Kamati ya Pamoja, hivi sasa yamesalia mambo sita tu. Kimsingi ni mambo yahusuyo maslahi ya
kiuchumi na yote yapo katika hatua nzuri za kuyamaliza. Mambo hayo ni:
1.
Mgawanyo wa mapato:
(a)
Hisa za
SMZ zilizokuwa katika Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki
(b)
Mgawanyo wa Mapato yatokanayo na faida ya
Benki Kuu.
2.
Utafutaji na uchimbaji mafuta na gesi asili.
3.
Ushirikiano wa Zanzibar na taasisi za nje.
4.
Ajira kwa watumishi wa Zanzibar katika taasisi
za Muungano.
5.
Usajili wa vyombo vya moto.
6.
Tume ya Pamoja ya Fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Serikali zetu mbili zimeamua kwa
dhati kutumia fursa ya mchakato huu wa mabadiliko ya Katiba kuyamaliza yale
yanayohitaji kuingizwa kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mambo
hayo ni matatu yafuatayo:
1.
Utafutaji na uchimbaji mafuta na gesi asili.
2.
Ushirikiano wa Zanzibar na taasisi za nje.
3.
Tume ya Pamoja ya Fedha.
Matatu mengine yatamalizwa kwa kutumia
taratibu za kiutawala. Hali kadhalika, katika
kipindi cha mpito kinachopendekezwa na Tume yaani 2015 – 2018 ni nafasi nzuri ya
kushughulikia masuala yenye migongano kati ya Katiba ya Zanzibar na ile ya Jamhuri
ya Muungano. Mimi naishi kwa matumaini
na kwa vile tunayo dhamira njema ya kuimarisha Muungano wetu, naamini tutaweza
kuziondoa tofauti zilizopo.
Orodha
ya Mambo ya Muungano
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kuhusu orodha ya mambo ya
Muungano kuwa 22 badala ya 11 ya awali, napenda kuwahakikishia
kuwa Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hazina kigugumizi
wala upungufu wa dhamira ya kisiasa ya kuyapunguza yale yanayopunguzika.
Napenda kwanza kabisa, ieleweke kuwa kilichoongeza orodha hiyo si hila za
Serikali ya Muungano kutaka kupunguza madaraka ya Zanzibar kwa mambo yake ya
ndani. Na, wala siyo udhaifu wa viongozi
wa Zanzibar katika kutetea maslahi ya nchi yao.
La hasha.
Pili, naomba ieleweke kuwa, kila
kilichoongezwa katika Orodha ya Mambo ya Muungano kilikuwa na sababu inayoeleweka,
inayoelezeka na iliyokubalika na pande zote mbili za Muungano. Hakuna hata jambo moja lililoingizwa kwenye
Katiba kwa kificho. Taratibu stahiki za
kikatiba na kisheria zilifuatwa. Hoja
ziliwasilishwa Bungeni na kujadiliwa kwa uwazi na uamuzi ulifanywa na Bunge kwa
kuzingatia kanuni ya theluthi mbili ya kura za kila upande wa Muungano. Kumbukumbu zipo katika Hansard za Bunge la
Muungano, ambazo ziko wazi kwa kila mtu anayetaka kuzisoma asome. Nashauri mkazisome ili mpate kujua ukweli na
undani wa kila kilichoongezwa na sababu za kufanya hivyo.
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Nchi
zetu mbili zilipoungana mwaka 1964 na kuzaa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kulikuwa
na mambo 11 kwenye Orodha ya Mambo
ya Muungano. Mambo hayo ni haya
yafuatayo:
1.
Katiba ya Jamhuri ya Muungano,
2.
Mambo ya Nje,
3.
Ulinzi,
4.
Polisi,
5.
Hali ya Hatari,
6.
Uraia,
7. Uhamiaji,
8. Biashara
ya nje na mikopo,
9. Utumishi
katika Serikali ya Muungano,
10. Kodi
ya Mapato, Kodi ya Makampuni, Ushuru wa Forodha na Ushuru wa Bidhaa,
11. Bandari,
Mambo ya Anga, Posta na Simu.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kati ya mwaka 1965 na 1992
mambo ya Muungano yaliongezeka kutoka 11
hadi kufikia 22, kimsingi kutokana
na mambo mbalimbali yaliyotokea nchini na kwenye ukanda wetu wa Afrika Mashariki. Pande
zetu mbili za Muungano zilikubaliana kuwa mambo hayo yaongezwe katika Katiba na
taratibu za kisheria na Kikatiba zilifuatwa.
Kwa idhini yako naomba nitoe maelezo kwa ufupi kwa yale yaliyoongezwa na
kitu kilichosababisha mabadiliko hayo kufanywa.
1. Jambo la kwanza kuongezwa, yaani la 12 lilikuwa ni “sarafu, mabenki na
fedha za kigeni”. Hii ilifanyika tarehe
10 Juni, 1965 kufuatia kuvunjika kwa Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki (East
African Currency Board) mwaka 1964. Kwa
ajili hiyo, kila nchi mwanachama wa Jumuiya ililazimika kuwa na sarafu yake na mipango
yake ya kusimamia mambo yake ya kibenki na fedha. Serikali zetu mbili zilikubaliana masuala hayo
yashughulikiwe na Serikali ya Muungano na Muswada husika wa Bunge uliidhinishwa
kuwa Sheria na Mzee Abeid Amani Karume aliyekuwa akikaimu Urais tarehe 10 Juni,
1965.
2.
Tarehe 11 Agosti, 1967 yaliongezwa mambo yafuatayo kwenye Orodha ya
Mambo ya Muungano:-
(a)
Leseni
za Viwanda na Takwimu, (Jambo la 13)
(b)
Elimu
ya Juu, (Jambo la 14)
(c) Jambo
la 15 lilikuwa ni mambo yote
yaliyokuwa kwenye Nyongeza ya 10 ya
Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Nyongeza hiyo ilikuwa na mambo 27
ambayo Serikali ya Muungano ilipewa jukumu la uratibu. Mambo hayo ni pamoja na Mahakama ya Rufani ya
Afrika Mashariki, Utabiri wa Hali ya Hewa, Utafiti, Vipimo na Mizani, Huduma ya
Usafiri wa Reli, Barabara, Usafiri wa Majini na kadhalika.
3.
Tarehe
22 Julai, 1968 “rasilimali ya mafuta, petroli na gesi asilia” iliongezwa kwenye
Orodha ya Mambo ya Muungano na kuwa jambo la 16. Kimsingi Serikali ya
Muungano ilipewa jukumu la kuagiza mafuta ya petroli na gesi asilia kwa ajili
ya nchi nzima. Baada ya kupanga upya
Orodha ya Mambo ya Muungano, suala la rasilimali ya mafuta likawa la 15.
4. Tarehe
22 Novemba, 1973 Baraza la Mitihani la Taifa liliongezwa na kuwa jambo la 16. Hii
ilifuatia kuvunjika kwa Baraza la Mitihani la Afrika Mashariki mwaka 1971 na hivyo
nchi yetu kulazimika kuunda Baraza la Mitihani la Taifa mwaka 1973.
5. Mwaka
1984 yalipofanyika mabadiliko makubwa katika Katiba ya mwaka 1977, Orodha ya
Mambo ya Muungano ilipangwa upya. Mambo
yaliyokuwemo kwenye Nyongeza ya 10
ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na kuorodheshwa kama Jambo la 15 katika Orodha ya Mambo ya Muungano
yalipunguzwa na kubaki matano. Mambo hayo yalipewa namba kama
ifatavyo:- Usafirishaji wa Anga kuwa
Jambo la 17, Utafiti kuwa la 18, Utabiri wa Hali ya Hewa kuwa la 19 na Takwimu kuwa la 20 na
Mahakama ya Rufani ya Tanzania ikawa jambo la 21.
6. Tarehe
17 Mei, 1992 likaongezwa jambo la “Uandikishaji
wa Vyama vya Siasa” na kuwa jambo la 22. Hii ilifuatia kuanzishwa kwa Mfumo wa
Vyama Vingi vya Siasa na hasa uamuzi kuwa vyama vitakuwa vya kitaifa.
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Bila
ya shaka maelezo haya yatasaidia kuelezea nini kimeongezwa na mazingira
ya
kuongezwa kwake ni yepi. Kulikuwepo na
sababu za msingi na wala siyo hila ya namna yo yote ile iliyofanywa na
mtu ye
yote mwenye nia mbaya na Zanzibar. Kama
tulivyoona mambo mengi yalihusu kilichokuwa kinatokea ndani ya Jumuiya
ya
Afrika Mashariki. Kila yalipotokea
mabadiliko katika uendeshaji wa shughuli za Jumuiya ya Afrika Mashariki,
huduma
zilizokuwa zikitolewa na Jumuiya zilikabidhiwa Serikali ya Muungano
kubeba kwa
sababu ya uwezo wake mkubwa wa kiuchumi. Yale yaliyokuwa yanagusa
sehemu zetu mbili za
Muungano yaliingizwa katika Orodha ya Mambo ya Muungano. Mengineyo
yaliachiwa kila upande
kushughulikia ilivyoona inafaa. Kwa
maana hii basi, mambo ambayo yalitokana na uamuzi wetu wenyewe ni mawili
tu. Mambo hayo ni rasimali ya mafuta na gesi asilia (1968), na
uandikishaji wa vyama vya siasa (1992).
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Ni msimamo wa Serikali zetu mbili, tangu
mwanzo mpaka leo kwamba, iwapo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeshajenga
uwezo wake wa kufanya baadhi ya mambo katika Orodha ya Mambo ya Muungano ipewe uhuru
wa kufanya hivyo. Lililo muhimu ni kuwa zisiondolewe
tunu zenyewe za Muungano wetu. Ndiyo
maana, mambo kama vile bandari, takwimu, kodi ya mapato, leseni za biashara, utafiti
na mengineyo, yanasimamiwa na kuendeshwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
pamoja na kuwemo kwenye Orodha ya Mambo ya Muungano. Imekuwa hivyo kwa miaka kadhaa sasa na
imethibitika kuwa Zanzibar inayamudu. Ni
makusudio yetu kutumia fursa ya mchakato huu sasa kuyaondoa rasmi mambo hayo na
mengineyo tutakayokubaliana kutoka kwenye Orodha ya Mambo ya Muungano.
Rasilimali
ya Mafuta na Gesi Asilia
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kwa ajili hiyo tumekubaliana kuliondoa
suala la rasilimali ya mafuta na gesi asilia lisiwe jambo la Muungano. Jambo hili tulishakubaliana tangu wakati wa
Rais Amani Abeid Karume tuliondoe na hata alipokuja Rais Shein msimamo
haukubadilika. Kilichotuchelewesha
kutekeleza ni kuibuka kwa fikra za kuwa na mchakato huu wa Katiba mpya. Tuliona
kuwasilisha Bungeni Muswada wa Sheria wa kuondoa jambo hili katikati ya
mchakato huu, ingeweza kuzua matatizo yasiyokuwa ya lazima. Tungeulizwa haraka ni ya nini tungeweza
kukosa majibu.
Hatimaye wakati wake wa
kulimaliza suala hili sasa umefika.
Misemo ya wahenga ya “subira yavuta heri” na “kawia ufike” imetuongoza
vyema tumefika mahali tunaweza kufanya hivyo. Zipo sababu mbili
zilizotushawishi kuamua kuitoa rasilimali hii kwenye Orodha ya Mambo ya
Muungano. Kwanza kwamba, siku hizi
Serikali haiagizi mafuta. Kazi hiyo
hufanywa na makampuni binafsi. Pili,
kwamba, rasilimali ya mafuta na gesi yakipatikana Zanzibar ni suala la kiuchumi
ambalo lipo kwenye mamlaka ya Zanzibar kama ilivyo karafuu, hiliki, mwani na
kadhalika. Au kama ilivyo dhahabu, gesi,
pamba, kahawa na kadhalika kwa upande wa Tanzania Bara. Hivyo, Zanzibar iachwe kumiliki rasilimali
yake ya kiuchumi.
Zanzibar
na Ushirikiano wa Kimataifa
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Jambo lingine muhimu ambalo
Serikali zetu mbili zimelizungumza na kukubaliana tulitafutie ufumbuzi ni
kuhusu Zanzibar kupata fursa ya kujiunga na mashirika ya kimataifa, kukopa na
kupata misaada kutoka nchi za nje bila kizuizi.
Kwa sasa fursa hiyo ina vikwazo vya namna mbalimbali. Ni ukweli usiopingika kuwa jambo hili limechangia
kwa kiasi kikubwa kujenga hisia hasi kuhusu Muungano kwa upande wa Zanzibar. Aidha, limechangia sana kuchafua hali ya hewa
ya kisiasa Zanzibar kwa nyakati mbalimbali.
Hata zile kauli kwamba Tanzania Bara imejificha kwenye koti la Serikali
ya Muungano, na kutaka itoke ionekane ili iache kunufaika isivyostahili, zinazochangiwa
sana na mazingira haya iliyonayo Zanzibar. Serikali zetu mbili zinaamini kuwa mambo
haya yakipatiwa ufumbuzi tutakuwa tumeondoa kizingiti kikubwa katika ustawi wa
Muungano wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Serikali
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
tumekubaliana kuwa, tutumie fursa za mchakato huu kuyamaliza mambo haya yaishe! Bahati nzuri dhana iliyopo katika Ibara ya
65(2) ya Rasimu inatoa jawabu mwafaka kwa tatizo hili. Tukikubaliana, itaipa Zanzibar “uwezo na
uhuru wa kuanzisha uhusiano na ushirikiano na jumuiya au taasisi yo yote ya
kikanda na kimataifa kwa mambo yaliyo chini ya mamlaka yake kwa mujibu wa
Katiba ya nchi” bila kizuizi. Ni maoni ya Serikali zetu mbili kuwa fursa hiyo inaweza kutolewa kwa Zanzibar
bila ya kulazimika kuwa na muundo wa Serikali tatu. Hatuuoni ulazima huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kwa maoni yangu kitu kingine muhimu
cha kufanya ni kuongeza msukumo, utakaohakikisha kuwa Tume ya Pamoja ya Fedha
inatimiza ipasavyo majukumu yake. Wanaohusika
na utekelezaji wa maamuzi yake wabanwe ipasavyo kutimiza wajibu wao. Iwekwe mifumo na masharti katika sheria au Katiba
ya kuwabana watekelezaji kwa ajili hiyo.
Hali kadhalika ihakikishwe kuwa, Akaunti ya Pamoja inaanzishwa bila
ajizi na kutumika na pande zote. Aidha, mfumo
wa mawasiliano na ushirikiano baina ya Serikali zetu mbili yaani Kamati ya
Pamoja ya Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, upewe nguvu
ya kisheria na kama hapana budi upewe nguvu ya Kikatiba. Tukifanya hivyo tutafanikiwa kuyaweka mambo
yote sawa hata bila ya kuhitaji kuunda Serikali ya tatu.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Waheshimiwa Wajumbe;
Katika mjadala kuhusu mapendekezo
ya kuwa na muundo wa Muungano wenye Serikali tatu, wananchi wametoa maoni na
mapendekezo mengi mazuri kuhusu changamoto za Serikali tatu zilizoainishwa na
Tume na namna ya kuzitatua. Tena yapo
maoni ya watu wanaopenda muundo wa Serikali tatu na wasiopenda muundo wa
Serikali tatu. Nawaomba myatafakari kwa
uzito unaostahili. Yapo mambo muhimu ya kuyatafutia ufumbuzi. Kwanza, kwa mfano ni ile hoja kwamba Serikali
ya Muungano inayopendekezwa haikujengeka kwenye msingi imara. Haina nguvu yake yenyewe
za kusimama. Inategemea mno ihsani ya
nchi washirika. Kwa sababu hiyo inaweza kuanguka
wakati wowote, na Muungano kusambaratika, iwapo itakosa ihsani ya nchi
washirika. Tena inaweza kuwa hivyo hata
kama ni mmoja wa washirika amefanya hivyo.
Pili, kwamba, haielekei Serikali
hiyo ina chanzo cha uhakika cha mapato ya kuiwezesha kusimama yenyewe na kutekeleza
majukumu yake. Ushuru wa bidhaa unaopendekezwa unatiliwa shaka kuwa
hautatosheleza mahitaji. Pia, kwamba,
hakuna uhakika wa fedha hizo kupatikana kwa vile, Serikali ya Muungano haina
chombo chake chenyewe cha kukusanya mapato hayo. Itategemea vyombo vya nchi washirika
kuikusanyia na kuipelekea. Kuna hatari
ya shughuli za Serikali ya Muungano kusimama wakati wo wote au hata kusimama
kabisa kwa sababu ya nchi washirika kuchelewa au kushindwa kuwasilisha
makusanyo ya kutoka kwao.
Bahati mbaya Serikali ya
Muungano haina uwezo wala nyenzo za kuhakikisha kuwa mapato yake
yanawasilishwa. Serikali hiyo haina
mamlaka ya kuzibana nchi washirika kuwasilisha au kuziwajibisha zisipofanya
hivyo. Katika mazingira hayo ni rahisi
kwa Serikali ya Muungano kukwama na kushindwa kutekeleza majukumu yake. Huu
ni muundo ambao inakuwa ni rahisi sana kwa Muungano kuvunjika.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Katika Rasimu ya Katiba, Serikali
ya Muungano inapewa fursa ya kukopa kama chanzo cha kujipatia mapato ya
kuendesha shughuli zake. Lakini, kwa
sababu ya kukosa rasilimali zake yenyewe, huenda ikawa vigumu kwa Serikali hiyo
kukopesheka. Kwa jumla hii ni Serikali ambayo ukuu wake hauna nguvu iliyo
thabiti, na watu wengine wanaona kama vile ukuu huo haupo kabisa. Akitokea kiongozi ye yote wa nchi washirika
akatunisha misuli dhidi ya Rais wa Muungano au kupinga maamuzi ya Serikali au
chombo cha Muungano, Rais na Serikali yake watakuwa hawana lo lote la
kufanya. Kwa kweli uhai wa Muungano
katika muundo wa Serikali tatu ni wa mashaka makubwa.
Hofu hizi kuhusu udhaifu wa
Serikali ya Muungano chini ya mfumo wa Serikali tatu unaopendekezwa, zinawasumbua
hata wale wanaopendelea mfumo wa Serikali tatu kuwepo. Wao wangependa iwepo Serikali ya Muungano
yenye nguvu na inayoweza kusimama yenyewe kwa kujitegemea. Wanaona kilichopendekezwa hakitoi matumaini
hayo. Hii ina maana kuwa lazima mawazo
bora zaidi yatolewe ili kupata Serikali ya tatu yenye ukuu unaoonekana na
inayoweza kusimama yenyewe bila kuwa tegemezi na egemezi kwa nchi washirika. Pia inaweza kuwa nguzo ya kutegemewa na nchi
washirika. Bila ya shaka Bunge hili likiamua tufuate mfumo huo linaweza
kuonyesha njia ya kuondoa hofu hizo. Kwa waumini wa Serikali mbili wanaona kuwa huu
ni uthibitisho wa ubora wa muundo wa Serikali mbili.
Changamoto
za Hisia za Utaifa
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Katika kuainisha changamoto
za muundo wa Serikali tatu, Tume ya Mabadiliko ya Katiba imeyataja mambo mengine
mawili makubwa ambayo ningependa Waheshimiwa Wajumbe muyape tafakuri
stahiki. Mambo hayo ni mosi, misuguano na mikwamo (deadlocks and paralysis) katika kujadili
na kufanya uamuzi kuhusu mambo muhimu ya Muungano. Na pili,
ni kuibuka kwa hisia za utaifa (nationalistic
sentiments) wa zamani kwa nchi washirika.
Nawaomba myatafakari kwa makini sana mambo haya, kwa sababu ya uwezo wake
mkubwa wa kuhatarisha siyo tu ustawi na uhai wa Muungano, bali hata usalama wa
raia na mali zao. Naona hata Tume
haikuweza kupata ufumbuzi ulio mwafaka kabisa kwa changamoto hizi. Bila ya shaka katika mijadala yenu
Waheshimiwa Wajumbe mnaweza kusaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Ni lazima lifanyike kila
linalowezekana kuhakikisha kuwa maamuzi hayakwami kwani yakikwama maana yake
shughuli za Muungano zitakuwa zimekwama.
Kama hazitakwamuliwa kwa wakati ustawi wa Muungano utaathirika. Ikishindikana kabisa kupatikana ufumbuzi
Muungano unaweza kuvunjika. Kuibuka na kukua
kwa hisia za utaifa (nationalistic
feelings) kwa nchi washirika, yaani Utanganyika na Uzanzibari ni tishio
kubwa sana kwa uhai wa Muungano. Hebu
fikiria, watu walioishi pamoja kidugu na kwa kushirikiana, kama watu wamoja na
raia wa nchi moja yaani Watanzania kwa miaka 50, kuja kujikuta uhusiano wao
kuwa ni kati ya Watanganyika na Wazanzibari na siyo kati ya Watanznaia. Kwa mujibu wa sensa iliyopita takriban asilimia 90 ya Watanzania waliopo sasa wamezaliwa
baada ya mwaka 1964. Nchi wanayoijua ni
Tanzania. Litakuwa ni jambo lenye
mshtuko mkubwa na athari zisizoweza kutabirika, watu hao watakapojikuta ni
wageni wanaotakiwa kutengenezewa utaratibu maalum wa kusafiri na kuishi wakiwa
upande wa Muungano ambao siyo kwao kwa asili.
Wanakuwa wageni na fursa walizokuwa wanazipata waendapo popote haiwi
rahisi tena kuzipata.
Katika mazingira hayo ni rahisi sana chuki kupandikizwa
na watu waliokuwa ndugu mara moja watajikuta maadui. Aidha, watu wanaweza kujikuta wakilazimika
kurudi kwao kwa asili ama kwa kufukuzwa au kwa sababu ya mazingira kuwa magumu
kiasi cha kuona bora waondoke. Watu hao
wanaweza kulazimika kuondoka huku wakiacha nyuma kila kitu walichokichuma
maishani.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Changamoto hizi kubwa mbili
za mfumo wa Serikali tatu ambazo Tume imeziona, ni za kweli. Si mambo ya kufikirika. Yale yaliyowakuta watu wenye asili ya
Tanzania Bara ya kuchomewa moto biashara zao Zanzibar mwaka 2012 na watu wenye
hisia kali za Uzanzibari, na kuwataka watu wa Bara waondoke Zanzibar, huenda
yakawa madogo. Matukio ya namna hii
yanaweza kutokea pande zote mbili na kusababisha maafa makubwa. Itaanza baina ya watu, baadaye itakuwa baina
ya Serikali zetu mbili na kuzifikisha nchi zetu mbili zilizokuwa ndugu na
rafiki, kwa nusu karne, ghafla kuwa maadui wasioombana chumvi na wasiotakiana
heri. Umoja wetu utatetereka na Muungano
wetu unaweza kuvunjika. Kwa nini tufike
huko?
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Sisi viongozi tuliopewa dhamana ya kuamua kwa
niaba ya wananchi wetu, hatuna budi kuyapima mambo haya kwa umakini mkubwa ili
tufanye uamuzi ulio sahihi. Tusije
tukajutia uamuzi wetu tutakapoona watu wanafukuzana, wanauana na mali zao kuporwa. Na, tukifikia hatua hiyo Muungano
kusambaratika halitakuwa jambo la ajabu.
Kwa
kweli, unapoyatafakari
haya, ni rahisi kuelewa kwa nini wazee wetu waasisi waliamua
walivyoamua. Waliona mbali. Tusipuuze fikra zao na maono yao. Kuna
hatari ya nchi yetu na watu wake kupoteza
kila kitu tulichokijenga kwa miaka 50. Badala
ya kujenga tunaweza kujikuta tumebomoa hata msingi katika nchi
washirika. Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1993 alituasa
kuhusu
hatari hiyo: “Hamuwezi kutenda dhambi kubwa
namna hiyo bila adhabu… na adhabu nyingine zimo mle mle ndani ya kitendo
hazisubiri.”
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Siku moja kiongozi mmoja wa juu wa madhehebu ya dini nchini aliniuliza: “Hivi Serikali mbili zikiwa na matatizo jawabu
ni kuongeza ya tatu? Si matatizo ndiyo yatazidi? Je, matatizo yakizielemea hizo Serikali tatu
si kila mtu atachukua njia yake? Mtakuwa
mmepoteza kila kitu. Mimi nawashauri
msichoke kutafuta majawabu kwa matatizo ya hizi mbili! Huko mnakotaka kwenda kuna hatari nyingi”.
Pengine na ushauri huu wa mtu
wa Mungu nao ni vyema kuupa nafasi na kuutafakari.
Kazi
Yenu Kubwa
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Mambo
ya kuyasemea ni mengi
mno lakini kwa sababu ya ufinyu wa muda, nisingeweza kuyazungumzia
yote. Naamini, mtayaona katika kuipitia Rasimu na kwenye
majadiliano yenu. Napenda kusisitiza kwenu kuwa kazi iliyo mbele yenu ni
kubwa
sana. Ni kubwa kwa maana mbili. Kwanza, jukumu lenyewe la kutunga
Katiba ya
nchi ni zito sana. Taswira ya nchi yetu
itakuwaje na itaendeshwa vipi kwa miaka mingi ijayo iko mikononi mwenu.
Ipeni nchi yetu hatima njema. Pili, ni kubwa kwa maana ya uzito wa
mambo ya kujadili na kuyafanyia
uamuzi. Kwa ajili hiyo, ni muhimu sana kuisoma
Rasimu na Taarifa ya Tume kwa makini na kuzielewa. Jipeni muda wa
kutafakari kila neno, kila sentensi,
na kila dhana ili muweze kufanya uamuzi ulio sahihi. Mkifanya hayo
mtakuwa mmeisaidia nchi yetu na
Watanzania wote kupata Katiba nzuri.
Nimefarijika sana kusikia
kuwa mtajigawa kwenye Kamati 12 wakati wa kujadili Rasimu. Huu ni utaratibu mzuri kwani mkiwa katika vikundi
vya watu wachache, mtakuwa na mijadala ya kina zaidi. Watu wote wanaweza kupata fursa ya kutoa
maoni yao, kwa kila kifungu na kila jambo linaloibuliwa na kuzungumzwa. Kwa kufanya hivyo, mtatimiza kwa ukamilifu
jukumu lenu la kutunga Katiba. Wote
mtakuwa mmeshiriki kujadili kila sura na vipengele vyake vyote. Mkimaliza kazi yenu mtapokea kwa haki sifa
nzuri kama Katiba itakuwa nzuri, au lawama stahiki iwapo itakuwa kinyume chake.
Pongezi
kwa Mwenyekiti wa Muda
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Nitakuwa mwizi wa fadhila
kama nitamaliza hotuba yangu bila ya kutambua kazi nzuri iliyofanywa na Mheshimiwa
Pandu Ameir Kificho, Spika wa Baraza la Wawakilishi, alipokuwa
Mwenyekiti wa Muda wa Bunge hili. Kazi
yake haikuwa rahisi hata kidogo, lakini kwa umahiri na ustadi mkubwa ameweza
kufanikisha mambo kwa kiasi ambacho anastahili pongezi zetu sote. Anastahili pongezi kwa sababu yeye aliendesha
Bunge hili bila ya kuwepo kwa kanuni.
Tatizo hili hatakuwa nalo Mwenyekiti wa Kudumu kaka yangu Mheshimiwa
Samuel Sitta.
Napenda pia kuwapongeza
Waheshimiwa Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kwa hatua mliyofikia. Hata hivyo, mmechukua muda mwingi katika hatua
ya awali hivyo hamna budi kuongeza kasi.
Naomba niwakumbushe kuwa mijadala yenu hii inafuatiliwa kwa karibu sana
na Watanzania. Wamewekeza sana matarajio
yao kwenu. Hamna budi, haiba na taswira
ya uongozi muionyeshe wakati wote wa kuendesha mijadala yenu kwa lugha na vitendo
vyenu. Wakati wa semina na mjadala wa kupitisha Kanuni za Bunge hili, baadhi ya
wananchi wamekwazika sana na mwenendo wa baadhi ya Wajumbe. Hawakutegemea kuyaona matendo waliyoyaona mkifanya
na kusikia maneno waliyoyasikia kutoka kwenye vinywa vya baadhi yenu.
Ni matumaini yangu na ya
Watanzania wote kuwa hali ile haitajirudia tena katika awamu hii. Tusiwafikishe mahali Watanzania wakakata
tamaa na Wajumbe wao au na hata chombo hiki muhimu sana kwa mustakabali wao na
wa nchi yao. Tutoe hoja badala ya kupiga
kelele (argue don’t shout) au kuzomea. Hakuna haja ya kutumia
lugha isiyokuwa ya
staha katika kujieleza. Hakuna haja ya kukingiana ngumi, kutishiana
hili na lile au hata kugombana. Ni utovu wa uungwana usiotegemewa
kutoka kwenu. Tusiwaangushe wananchi wa Tanzania
wanaotutegemea sana.
Wekeni
Maslahi ya Taifa Mbele
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Ombi langu la mwisho kwenu ni
kuwasihi kuwa wakati wote muongozwe na kujali maslahi mapana ya nchi yetu na
watu wake badala ya kujali maslahi yenu binafsi au ya makundi yenu. Naomba kaulimbiu yenu iwe “Tanzania Kwanza”. Najua kila mmoja wenu amekuja na maoni
yake au atakuwa nayo kwa kila jambo litakalojadiliwa. Wengine wamepewa misimamo na vyama vyao au makundi
yao. Si jambo baya na ni hatua muhimu ya
kuleta mafanikio, kama misimamo hiyo na mawazo hayo ni ya kujenga.
Hata hivyo, mnachotegemewa
kufanya ni kuwa tayari kuwianisha na kuunganisha mawazo yenu mazuri na ya wenzenu,
ili kupata msimamo wa pamoja na uamuzi wa pamoja ulio bora. Kwa sababu hiyo, hamna budi kuwa tayari
kusikiliza mawazo ya wengine, hata kama ni tofauti na yenu mliyokuja nayo. Tafuteni kilicho chema kwa yale yanayosemwa
na watu wengine hata kama ni watu usiokubaliana nao au huwapendi au hampendani. Kunaweza
kuwepo kitu chenye manufaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa
Wajumbe;
Nawaomba muwe hodari wa
kushawishi badala ya kulazimisha.
Mkifanya hivyo hamtalazimika kutumia muda mwingi wa kula njama za namna
ya kuwazidi maarifa wale mnaotofautiana nao kwa mawazo. Lazima pia mtafute namna ya kushirikiana na
kuwasiliana na makundi mengine.
Msitafute kushindana, hili ni jambo ambalo lazima wote mtoke hapa mkiwa washindi. Yaani lazima Watanzania wote washinde kwani
wao ndiyo wenye Katiba yao. Nawapongeza viongozi wa vyama vya siasa na
asasi mbalimbali kwa kutambua na
kuthamini umuhimu wa kuwa na taratibu za
mawasiliano, mashauriano na ushirikiano.
Daima muwe watu wa kutafuta maridhiano. Mmefanya vizuri katika hatua ya
awali. Mmejiwekea taratibu nzuri za
kufanya hayo, tafadhalini zitumieni. Jengeni
madaraja imara zaidi katika awamu hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Naomba nimalize kwa kuwaomba
Watanzania wote tukiongozwa na viongozi wetu wa dini tumuombe Mola wetu ajalie
rehema zake ili mchakato wa kutunga Katiba uende salama. Aliongoze Bunge hili na Wajumbe wake waweze
kufanya uamuzi ulio sahihi na wenye manufaa kwa taifa letu kwa kila
watakaloliamua.
Baada ya kusema maneno yangu mengi hayo, nirudie
kukushukuru Mheshimiwa Mwenyekiti kwa kunipa fursa hii adhimu ya kulihutubia
Bunge Maalum la Katiba. Nawatakieni kila
la heri na mafanikio mema. Katiba Mpya Inawezekana, Timiza Wajibu Wako.
Mungu
Ibariki Tanzania!
Mungu
Libariki Bunge Maalumu la Katiba!
Asanteni
sana kwa kunisikiliza!
Social Plugin