Ndugu wawili wa kiume wa familia moja ambao ni wakazi wa Kitongoji cha Milumba , Kata ya Kibaoni ,wilayani Mlele katika mkoa wa Katavi wanadaiwa kumuua kikatili, Kitungulu Luhende (65) kwa kumchinja na kuutelekeza mwili wake porini.
Taarifa kutoka katika eneo la tukio hilo pia kuthibitishwa na polisi zinadai wa kuwa chanzo cha ndugu hao wawili kufanya unyama huo inadaiwa ni wivu waliokuwa wakimwonea Luhende ambaye anadaiwa kuwa hawala wa mama yao , kwa kufanya na mama yao mapenzi mara kwa mara tena bila kificho .
Inadaiwa mama yao aitwae Sai Mponjie (65) ni mjane ambapo kwa muda mrefu sasa amekuwa na mahusiano ya kimapenzi na Luhende .
Akithibitisha Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi , Dhahiri Kidavashari aliwataja wanandugu hao ni pamoja na Luhende Kashila (16) na kakae Nyengu Kashila (19) ambao wanatuhumiwa kumuua kikatili ‘hawala’ ya mama yao .
Akisimulia mkasa huo , Kidavashari alidai kuwa Februari , 22 , mwaka huu saa mbili asubuhi , Luhende ambae pia ni mkazi wa Kitongoji hicho cha Milumba alimwaga mkewe ambaye jina lake halikuweza kufahamiaka mara moja kuwa anaenda kijijini Kirida ambako pia ana mji mwingine .
“Hata hivyo inadaiwa marehemu badala ya kwenda kijijini Kirida mwenye mji wake mwingine alipitia nyumbani kwa rafiki yake katika kitongoji hicho cha Milumba , aitwae Milembe Katembeni ambako aliiacha pikipiki yake yenye aitwae Sai “ alidai Kamanda Kidavashari.
Inadaiwa kuwa marehemu hakuweza kuonekana tena hadharani hadi mwili wake uligundulika ukiwa umetekelezwa katika eneo la milima ya kitongoji hicho cha Milumba ukiwa tayari umeshaharibika kufuatia msako mkali uliofanywa na askari Polisi na askari wa jadi ‘sungusungu’huku pembeni ya mwili huo wa marehemu iliokotwa leseni yake ya udereva Daraja A.
“Baada ya marehemu kutorejea kuchukua pikipiki yake rafiki yake aliingia wasiwasi baada ya wiki kupita bila Luhende kuonekana na kuchukua mali yake hivyo aliamua kutoa taarifa kwa Mtemi wa Sungusungu katika Kitongoji hicho kisha akatoa taarifa katika Kituo kidogo cha Polisi cha Kibaoni ndipo msako mkali ulipoaanza “anadai Kamanda .
Kwa mujibu wa Kidavashari chanzo cha mauaji hao ni wivu wa watoto hao baada ya kuona marehemu akifanya mapenzi na mama yao mara kwa mara kitendo kinachodaiwa kuwakera sana watoto hao .
Anaongeza kuwa tayari mama ya watoto hao Sai Mponje (65) na mwanae aitwae Luhende Kashele (16) wanashilikiwa kwa mahojiano huku polisi ikimsaka mtoto mwingine aitwae Nyengu Kashele (19) ambaye alitoroka mara baada ya kufanyika kwa mauaji hayo na kujificha kusikojulikana .
Na Walter Mguluchuma, Mpanda - Katavi