NB-Picha haihusiani na tukio katika habari hapa chini |
Mtoto mdogo mwenye umri wa mwaka mmoja amekufa baada ya kutumbukia
kwenye sufuria ya chai iliyokuwa jikoni katika wilaya ya Bunda, mkoani Mara.
Tukio hilo la kusikitisha lililothibitishwa na polisi limetokea
juzi majira ya asubuhi katika kijiji cha Kibara B, wilayani humo.
Mwenyekiti wa kijiji cha Kibara B, Bw. Mafwili Munyaga, amesema
kuwa mtoto huyo wa jinsia ya kike alitumbukia kwenye sufuria hiyo ya chai
iliyokuwa jikoni wakati mama yake mzazi alipomuacha hapo na kuingia ndani ya
nyumba.
Bw. Munyaga amesema kuwa baada ya kutumbukia kwenye sufuria hiyo
mama yake alisikia kelele za mtoto huyo na kwamba kwa kushirikiana na majirani
walimuokoa na kumpeleka katika hospitali ya misheni Kibara, lakini muda mfupi
akapoteza maisha.
Kufuatia tukio hilo mwenyekiti huyo amewataka wazazi hasa wanawake
kuwa makini na watoto wao kwa kuacha kukaa nao katika mazingira ambayo ni
hatarishi kwa maisha yao, ili kujiepusha na majanga yasiyokuwa ya lazima.
via>> Mara yetu
Social Plugin