Lori la mizigo aina ya Fusso likiwa limegongana na gari ndogo aina ya Toyota Hilux Pick Up katika eneo la Hedaru, wilayani Same, Kilimanjaro, juzi na kusababisha vifo vya watu 12. |
Mji wa Hedaru uliopo wilayani Same mkoani Kilimanjaro, jana
ulizizima kwa vilio na simanzi baada ya waombolezaji 12 wote ndugu,
kufariki dunia kwa ajali ya barabarani.
Waombolezaji hao wanawake, walipewa lifti ya gari
na Diwani wa Kata ya Hedaru, Gerard Mgwena (CCM), kwa ajili ya
kuwapeleka msibani eneo la Majengo ambako mtu mmoja alifariki kwa
kusombwa na maji.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro (RPC),
Robert Boaz alithibitisha ajali hiyo akisema ilitokea juzi saa 2:00
usiku na kwamba ilikuwa mbaya zaidi tangu kuanza kwa mwaka 2014.
“Ni ajali iliyohusisha magari matatu kwa wakati
mmoja…; watu 11 walifariki pale pale na mwingine alifariki dunia leo
(jana), asubuhi Hospitali ya Rufaa ya KCMC,”alisema Boaz.
Hata hivyo, alisema hakuwa na nafasi nzuri ya
kufafanua kwa undani ajali hiyo kwa vile alikuwa nje ya Mkoa wa
Kilimanjaro na kuelekeza atafutwe Kamanda wa Kikosi cha Usalama
Barabarani Mkoa (RTO), Joseph Mwakabonga.
Akizungumza kwa niaba ya RPC, Mwakabonga alisema,
lori aina ya Mitsubish Fusso lililokuwa likitokea Moshi kwenda Dar
liligonga kwa nyuma gari aina ya Toyota Hilux Pick-Up.
Alisema kuwa baada ya kuligonga gari hilo
lililowabeba waombolezaji hao, nalo lilisukumwa na kwenda kuligonga lori
aina ya Scania lililokuwa na tela lake.
Lori hilo aina ya Scania lilikuwa likitokea Dar es
Salaam kwenda Moshi likiendeshwa na dereva wake, Gabriel David.
Madareva wawili wa Toyota Pick-Up na Toyota Fusso wote hawajulikani
waliko.
Taarifa zilizopatikana baadaye, zilisema dereva wa
Fusso alikuwa amelazwa katika Hospitali ya KCMC, wakati Kigogo wa CCM
aliyekuwa amewabeba waombolezaji akilazwa hospitali moja jijini Arusha.
Mwakabonga aliwataja waliofariki kuwa ni Stella
John(45), Salma Kizoka (33), Marry Senzige (49), Neema Daniel (52),
Rehema George (29) na Sophia Mbike (51).
Wengine ni Ritha Kalani (55), Mama Kalani Stephano
(55), Kolina Mmatha(55), Bahati Daud(25) na Farida Kiondo mwenye umri
wa miaka 25.
Majeruhi mmoja, Maria John (33) ambaye ni miongoni
mwa watu 10 waliojeruhiwa, alifariki dunia jana asubuhi katika
Hospitali ya Rufaa ya KCMC alikolazwa kwa ajili ya kuokoa maisha yake.
Kwa mujibu wa watu walioshuhudia ajali hiyo, watu hao walipata
ajali hatua 10 kutoka katika eneo ambalo ndugu yao aliosombwa na maji na
kufa, ambapo maiti yake iliokotwa eneo hilo.
Alex Shirima mmoja wa mashuhuda alisimulia kuwa gari la diwani lilikwama kweye tope katikati ya Barabara ya Moshi Dar es Salaam.
Alisema, kabla ya kushuka kuangalia namna ya
kulinasua gari lake, likatokea lori gari aina ya Fuso kwa nyuma ambalo
liliigonga gari lake iwani na kulisukuma mita kadhaa mbele ambako
lilikutana uso kwa uso na lori lingine aina ya Scania lililokuwa
likitokea Dar es Salaam.
Alisimulia kuwa kutokana na ukubwa wa ajali hiyo, eneo hilo lilitapakaa viungo vya binadamu na damu.
Shirima ambaye ni dereva aliyefika katika eneo
hilo dakika mbili baada ya ajali kutokea, alisema eneo hilo ni hatari
kwa madereva kwa kuwa mvua zikinyesha, barabara hujaa maji na matope.
Hali ilivyo kijijini
Mmoja wa watoto ambaye mama yake mzazi amefariki
katika ajali hiyo, Sebali Mkwizu alisema kuwa kijiji chao kimekumbwa na
ukimya na majonzi, huku wakishindwa kuamini kilichotokea.
Alisema kuwa ajali hiyo imechukua maisha ya ndugu
zake wanane na kati ya hao, saba walikuwa wakiishi kijijini hapo kwenye
nyumba tofauti zinazofuatana.
“Nimepoteza mama yangu mzazi, mama mdogo, shemeji
zangu watatu, mke wa ndugu yangu na watoto wawili. Hapa nyumba saba zina
msiba,” alisema Mkwizu.
Alibainisha kwamba mazishi ya wanawake hao yanatarajiwa kufanyika leo katika eneo la pamoja kijijini hapo.
“Tumeambiwa watazikwa eneo moja, lakini bado hatujajua ni sehemu gani, hadi kesho (leo) ndiyo tutapata taarifa kamili,” alisema.
Na Daniel Mjema na Rehema Matowo
Na Daniel Mjema na Rehema Matowo
Social Plugin