Rose Muhando |
John Lisu |
WAKATI
zoezi la upigaji kura wa kuchagua maeneo matatu ya kufanikisha Tamasha
la Pasaka linalotarajia kufanyika kuanzia Aprili 20 mwaka huu, waimbaji
mahiri wa muziki wa injili hapa Tanzania, Rose Mhando na John Lisu
wameonesha shukrani kwa wapiga kura kwa kuwapigia kura nyingi kuelekea
tamasha hilo.
Waimbaji
hao wanaoonesha kukubalika na wadau mbalimbali kushiriki katika tamasha
hilo kutokana na sababu mbalimbali za uwasilishaji wao wa Neno la Mungu
kwa wadau wa tamasha hilo, ingawa zoezi hilo likiendelea. John Lisu amewashukuru
Watanzania kwa kuonesha kumkubali katika utoaji wake wa huduma za
kufanikisha Neno la Mungu kupitia uimbaji wa nyimbo za injili, huku
zoezi la upigaji kura likiendelea.
Lisu
anasema Mkurugenzi wa Msama Promotions, Alex Msama amekuwa baraka kwa
Mungu kwa sababu amekuwa akitumia gharama kubwa kuwaleta waimbaji
mbalimbali wa Kimataifa katika tamasha hilo. “Mchango wa Msama kwa jamii
ni mkubwa hasa katika maendeleo, hivyo natoa shukrani kwa Msama kwa
kufanikisha kufanyika kwa matamasha ya kufikisha neno la Mungu ambayo ni
Pasaka na Krismasi,” alisema Lisu.
Rose Muhando amesema
kupata kura nyingi ambazo zinaashiria kipimo cha kuonekana na Mungu na
watu mbalimbali wanaopenda kazi za mikono yake kwamba anastahili kutoa
huduma ya Neno la Mungu katika tamasha hilo.
Muhando
anasema kwa sababu Mungu na Watanzania wameona umuhimu wa yeye kushiriki
kutoa huduma katika tamasha hilo, anawashukuru kwa hatua hiyo ingawa
zoezi bado linaendelea, kwani ni mwelekeo mzuri kwao kuelekea katika
tamasha hilo. “Namshukuru Mungu na watanzania wenzangu walionipigia kura
kwa wingi ikiwa ni njia pekee ya kufanikisha kuhudumu katika Tamasha la
Pasaka,” alisema Muhando.
Muhando
anasema sababu zinazofanikisha kupata uteuzi wa mara kwa mara ni kwamba
mara nyingi anapenda kazi yake ijieleze yenyewe na anaamini kwamba kazi
yake inatamka neno ambalo linagusa mioyo ya wanadamu ambao wanatakiwa
kumfikishia Mungu matatizo yao. Anatumia fursa hiyo kuishukuru kampuni
ya Msama Promotions kwa kufanikisha matamasha ya kumuimbia na kumtukuza
Mungu kupitia waimbaji mbalimbali wa kitaifa na Kimataifa ambao kwa
pamoja wanatoa elimu kwa jamii kuhusu kumuabudu Mungu.
Muimbaji
huyo amesema atajisikia vibaya iwapo atakosa nafasi ya kufikisha ujumbe
wa neno la Mungu kwa sababu tamasha hilo ni kubwa kwani hata ingekuwa
kuhudumu bure yuko tayari kwa sababu ibada yake inafika vilivyo kwa
Mungu kwa sababu ya wingi wa wanaohudhuria. Muhando anatumia fursa hiyo
kuwaeeleza Watanzania kwamba iwapo atapata nafasi ya kuwemo kwenye
orodha ya waimbaji katika tamasha hilo, atawasilisha albamu yake ya tano
ya Kamata Pindo la Yesu yenye nyimbo nyingi ikiwemo Facebook.
Kwa
mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya tamasha hilo, Alex Msama
waimbaji hao wamepigiwa kura na wadau wa muziki huo ambao wanakubali
kazi zao.
Msama
amesema Tamasha la Pasaka la mwaka huu limekuja katika mfumo mwingine
kabisa ambao ni wa upigaji kura ili kuchagua maeneo matatu
yatakayofanikisha kufanyika kwa tamasha hilo ambalo limekuwa likitumika
katika kufanikisha kuwasaidia wenye uhitaji maalum ambao ni pamoja na
wajane, walemavu na yatima.
Kupitia
matamasha yanayoandaliwa na Msama, viingilio vinavyopatikana katika
matamasha hayo vinafanikisha mipangilio ya kujenga kituo cha wenye
uhitaji maalum katika eneo la Pugu nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam
ambacho kinajulikana kama Jakaya Mrisho Kikwete, rafiki wa wasiojiweza.
Msama
anasema kwa kuanzia kuelekea tamasha hilo linalotarajia kuanza Aprili 20
jijini Dar es Salaam, ambalo litaendelea katika mikoa mingine zaidi ya
nane hapa nchini ambapo kauli mbiu ya tamasha hilo ni ‘Uzalendo Kwanza,
Haki huinua Taifa’ inayochochea na kuimarisha amani na kudumisha
maendeleo ya Tanzania ijayo.
Msama
anatoa wito kwa kuwakumbusha Watanzania namna ya kuwapigia kura wahusika
ambapo utaratibu wa kupiga kura tayari umebainishwa kwa wale ambao
watahitaji kufanya hivyo kwa kuandika Pasaka acha nafasi kisha andika
jina la mwimbaji unatuma kwenda namba 15327.
Pia kwa mgeni rasmi andika neno Pasaka acha nafasi kisha andika jina la mgeni rasmi unayetaka kumpigia kura tuma kwenda 15327, wakati mikoa unaandika Pasaka acha nafasi jina la mkoa unaotaka kuupigia kura tuma kwenda namba 15327, pia
imebainishwa kuwa kila mmoja anaruhusiwa kupiga kura kadri awezavyo ili
kupata mwimbaji na mgeni rasmi na mkoa husika ili tamasha hilo liweze
kufanyika katika mkoa husika.
Msama anasema mojawapo ya wadhamini wa tamasha hilo ni magazeti ya Dira ya Mtanzania na Pata Habari ambayo ni sehemu ya kampuni ya Msama Promotions na kutoa wito kwa wadhamini wengine kujitokeza kufanikisha tamasha hilo.
“Tamasha
la Pasaka linahitaji wadhamini wengine ambao watasaidia kufanyika kwa
ufanisi, hivyo wajitokeze kutusaidia kufanikisha, kwa sababu lina nia
njema kwa Tanzania,” alisema Msama
credit-dar es salaam