Mahakama ya
hakimu mkazi wilaya ya Shinyanga mkoani Shinyanga imewahukumu Mathias
Kalonga(40) na James Moshi(35) wakazi wa kijiji cha Shatimba wilaya ya
Shinyanga vijijini kutumikia kifungo cha miaka 242 jela baada ya kupatikana na kosa
la ubakaji kwa mande(kubaka kwa mpigo),wizi wa kutumia silaha pamoja na kujeruhi.
Mwendesha mashtaka,wakili
wa serikali Salome Mbuguni aliiambia mahakama hiyo jana kuwa mnamo tarehe 18
mwezi Oktoba mwaka 2012 washtakiwa Mathias Kalonga na James Moshi wakiwa na
wenzao walivamia nyumbani kwa mlalamikaji Lesha Jidomela,wakiwa na bunduki na
mapanga kisha kumjeruhi kwa kumpiga ubapa wa panga usoni na shavuni kisha
kupora simu 3 kinyume cha sheria hilo ikiwa ni kosa la kwanza na la pili.
Wakili huyo
aliieleza mahakama hiyo kuwa katika kosa la tatu na nne washtakiwa hao wote kwa
pamoja walivamia nyumbani kwa Sayi
Jidomela(ndugu yake na Lesha Jidomela) kisha kupora shilingi 57,000/= na simu moja na mshtakiwa wa kwanza aliyekuwa
na panga kumjeruhi Sayi Jidomela kwa kutumia panga hilo.
Mwendesha
mashtaka Mbuguni alisema katika kosa la tano na sita washtakiwa kwa pamoja
walimbaka mke wa Lesha Jidomela kwa pamoja(mande),lakini pia wakambaka mke wa
Sayi Jidomela kwa pamoja (mande) kinyume cha sheria.
Akitoa
hukumu,hakimu mkazi wa mahakama ya wilaya ya Shinyanga Thomson Mtani alisema
kutokana na kosa la wizi wa kutumia silaha kila mshtakiwa atatumikia kifungo
cha miaka 30 jela, hivyo kila mmoja jumla ya miaka 60 kila mmoja kwani
walitenda kosa hilo katika nyumba mbili.
Hakimu Mtani
alisema katika kosa la ubakaji kwa mande kila mshtakiwa atatumikia kifungo cha
miaka 30 jela,na kwa kuwa wote kwa pamoja walibaka wanawake wawili kwa zamu
kila mmoja jumla ya miaka atakayotumikia
jela ni miaka 60.
Hakimu huyo
aliongeza kuwa mshtakiwa wa kwanza Mathias Kalonga atatumikia kifungo cha miaka
2 mingine jela kwa kosa la kujeruhi kwa panga na kutakiwa kulipa fidia ya
shilingi laki mbili kwa waliojeruhiwa.
Kufuatia
hukumu hiyo washtakiwa watatumikia kifungo cha miaka 242 jela,ambapo mshtakiwa
wa kwanza Mathias Kalonga(40) atatumikia miaka 122 jela na mshtakiwa wa pili
James Moshi(35) atatumikia miaka 120 jela na wote kwa pamoja kuchapwa viboko 12
kila mmoja.
Hata hivyo
mahakama ya hakimu mkazi Shinyanga imewapa nafasi washtakiwa hao kukata rufaa
kwa hukumu hiyo.
Na Kadama Malunde-Shinyanga