Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Migogoro ya Ndoa Hatarii!! MWALIMU AUNGUZWA MAFUTA YA MOTO NA MKE WAKE,ALIKARIBISHWA CHAKULA AKAMWAGIWA MAFUTA YA MOTO

Lugano Mwambuja(50) ambaye ni mwalimu wa Shule ya Sekondari Sange iliyopo Wilaya ya Ileje Mkoani Mbeya. akiwa amelala nyumbani kwake akiuguzwa majeraha yaliyotokana na mafuta ya moto.
 
 KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida Mwanamke mmoja Mkazi wa Mtaa wa Ilembo  kata ya Iyela Jijini Mbeya amemjeruhi mume wake  kwa kumwagia mafuta ya moto kichwani kwa kile kilichodaiwa kuwa ni mgogoro wa ndoa baina yao.
 
Mwanamke huyo aliyefahamika kwa jina la Beatrice Lusamba (37) alitenda tukio hilo mwishoni mwa wiki majira ya saa saba mchana ambapo alimwagia mafuta hayo Mume wake Lugano Mwambuja(50) ambaye ni mwalimu wa Shule ya Sekondari Sange iliyopo Wilaya ya Ileje Mkoani Mbeya.
 
Akizungumzia tukio hilo Mhanga wa kisa hicho alisema yeye makazi yake yako Wilayani Ileje lakini Mkewe pamoja na baadhi ya watoto wake huishi Jijini Mbeya hivyo hufika nyumbani hapo mara chache kwa ajili ya kutembelea familia na kupeleka huduma mbali mbali kama baba wa familia.
 
alisema siku ya tukio alialikwa na Mkewe huyo kula chakula cha mchana ambapo baada ya kukaribishwa ndani mwanamke huyo aliingia jikoni akiwa na mayai matatu na galoni la mafuta ya kupikia, ambapo yeye alibaki SebuLeni akisubiri chakula alichokaribishwa  apikiwe.
 
Alisema baada ya dakika kumi Mkewe huyo alirejea Sebuleni akiwa ameshika kikombe chenye mafuta yaliyochemshwa ambayo alimwagia mwilini na kisha kukimbilia nje akimwacha mumewe akiugulia maumivu makali yaliyotokana na kuungua na mafuta ya moto mwilini mwake.
 
Mwalimu huyo aliongeza kuwa baada ya kupiga kelele ya kuomba msaada ndipo alipojitokeza jirani yake aliyefahamika kwa jina la Andamisye Kajange ambaye baada ya kumuona katika hali hiyo alimkimbiza katika Hospitali ya Rufaa ya Mbeya alikopatiwa matibabu na kuruhusiwa.
 
Mjumbe wa Mtaa Ilembo, Philly Mwakapimba alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuongeza kuwa kabla ya kupeleka Hospitali Mhanga waliripoti Kituo cha Polisi na kupewa fomu namba tatu (PF3) pamoja na kufungua faili  namba IR/2253/2014 na kuendelea kutibiwa.
 
Aliongeza kuwa mtuhumiwa hajakamatwa hadi leo baada ya kutorokea kusikojulikana huku lawama likipewa Jeshi la Polisi kutokana na kushindwa kumkamata mtuhumiwa kwa wakati hadi anapata mwanya wa kutoweka katika eneo la tukio.
 
Akizungumzia mahusiano yake na mkewe Mwalimu huyo alisema alioana na mkewe mwaka 2007 kwa ndoa ya kimila baada ya kufiwa na mkewe wa awali mwaka 2006 alimyemwachia watoto wawili ambao ni Doris(20) na Happy Mwambuja(21) ambapo aliamua kuoa mke huyo kwa ajili ya kusaidia malezi ya watoto hao.
 
Alisema akiwa kazini mara nyingi alikuwa akipata taarifa za mgogoro kati ya mkewe huyo na watoto jambo lililosababisha usuluhishi wa mara kwa mara kufanyika ukiongozwa na Serikali ya Mtaa huku sababu ikibainika kuwa ni tamaa ya mwanamke huyo kutaka kumiliki Nyumba ya Mwalimu huyo ili iwe mikononi mwake na siyo Familia.
 
Alisema mara nyingi Mwanamke huyo amekuwa akijaribu kuiba hati ya nyumba ili abadilishe majina na umiliki lakini anashindwa hali iliyoml;azimu Mwalimu huyo kuamua kununua eneo lingine na kujenga ili kumtengnisha mkewe pamoja na watoto lakini hali bado ilikuwa tete baada ya mwanamke huyo kutaka amilikishwe yeye nyumba.
 
hadi sasa Mwalimu huyo anaendelea kupatiwa matibabu Nyumbani kwake huku Jeshi la Polisi likiendelea kumsaka mtuhumiwa kwa ajili ya kumfikisha katika vyombo vya sheria kujibu shtaka la kujeruhi kwa makusudi.
mwisho.

Na Ezekiel Kamanga-Mbeya yetu



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com