MWALIMU
wa Shule ya Msingi Katani, Lingston Nelson (36) amelipa faini ya Sh
400,000 baada ya kujeruhi kwa panga na msumeno katika tukio la
kufumaniwa na mke wa mtu. Mwalimu huyo ametiwa hatiani na Hakimu wa
Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Nkasi, mkoani Rukwa, Ramadhan Mgamalila.
Akitoa
hukumu hiyo hakimu Mgamalila alisema ameridhika na ushahidi uliotolewa
upande wa mashtaka ambao uliongozwa na Mwendesha Mashtaka, Hamimu Gwelo.
Aidha
katika kesi hiyo, mtuhumiwa mwingine Betha Sangu (31) mkazi wa kijiji
cha Katani wilayani Nkasi ambaye alishtakiwa na Lingston kwa kosa la
kujeruhi, aliachiwa huru na mahakama hiyo baada ya kukosekana kwa
ushahidi wa kutosha kumhusisha na kadhia hiyo ya kujeruhi.
Betha
ndiye aliyekuwa na Lingston siku ya fumanizi. Hakimu Mgamalila alimtaka
Lingston kulipa Sh 400,000 kati ya hizo, Sh 100,000 ikiwa ni faini ya
ugoni na Sh 300,000 ikiwa ni fidia kwa majeruhi hao wawili ambapo kila
mmoja wao atalipwa Sh 150,000. Mshtakiwa alilipa kiasi hicho cha fedha
na kuachiwa huru.
Akisoma
hukumu hiyo juzi, Mgamalila aliieleza mahakama hiyo kuwa Oktoba 10,
mwaka jana saa tatu usiku kijijini Katani mshtakiwa Lingston alikuwa
akifanya mapenzi na Beatha ambaye ni mke wa kwanza wa Richard Sarungi
(33) mkazi wa kijijini humo.
Ilidaiwa
mahakamani hapo kuwa usiku huo wa tukio, Richard ambaye alikuwa
nyumbani kwa mkewe mdogo kijijini humo alipewa taarifa kuwa mkewe
alikuwa akifanya mapenzi na mwanaume mwingine nyumbani kwake mwanamke
huyo.
Kwa
mujibu wa hati hiyo ya mashtaka, Richard akifuatana na mdogo wake
aitwae Stanislaus Sarungi (28) walifika nyumbani kwa Beatha ili kufanya
fumanizi ambapo walifunga kwa nje mlango wa kuingilia kwa kufuli ili
kumzuia mgoni wake na mkewe, Beatha wasiweze kutoka wakati wakienda
kutoa taarifa kwa uongozi wa Serikali ya Kijiji hicho.
Ilidaiwa
mahakamani hapo kuwa Lingston na Beatha wakiwa ndani ya nyumba hiyo
usiku huo walisikia mlango wa kutokea nje ukifungwa kwa kufuli hivyo
waliamua kuuvunja ili waweze kutoka ndipo Lingston na mdogo wake
alipoaghairi kwenda kutoa taarifa kwa uongozi wa Serikali ya kijiji
hicho na kuanza kuushikilia mlango huo ili 'watuhumiwa' wao wasiweze
kutoka na kukimbia.
Hata
hivyo, kwa mujibu wa Mwendesha Mashitaka, Lingston na Beatha waliwazidi
nguvu Richard na mdogo wake na kuweza kuuvunja mlango huo.
Ndipo
Lingston na Beatha walipoanza kuwashambulia Richard na mdogo wake kwa
panga na msumeno ambapo kufuatia maumivu waliyoyapata kwa kipigo hicho
walipiga mayowe ya kuomba msaada ambapo majirani walifika nyumbani hapo
na kuwakamata washtakiwa hao wawili.
via>Habari Leo