THE UNITED
REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE
OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
Telephone:
255-22-2114512, 2116898
Fax: 255-22-2113425 |
PRESIDENT’S
OFFICE,
THE STATE HOUSE,
P.O.
BOX 9120,
DAR ES SALAAM.
Tanzania.
|
TAARIFA KWA
VYOMBO VYA HABARI
SALAMU ZA
RAMBIRAMBI ZA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA DKT. JAKAYA
MRISHO KIKWETE
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia Salamu za
Rambirambi Dkt. Jacob Chimeledya, Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, kuomboleza
kifo cha Askofu Godfrey Mdimi Mhogolo wa Dayosisi ya Kati, Dodoma kilichotokea
tarehe 27 Machi, 2014 katika Hospitali ya Mil Park nchini Afrika Kusini
alikokuwa amepelekwa kwa matibabu.
“Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo
cha Mtumishi wa Mungu, Askofu Godfrey Mdimi Mhogolo aliyelitumikia Kanisa lake
la Anglikana kwa uaminifu na uadilifu mkubwa, na ambaye mchango wake kwa maisha
ya kiroho ya Waumini wake unajulikana kwa wengi miongoni mwetu”, amesema Rais Kikwete
katika Salamu zake za Rambirambi.
Rais Kikwete amesema kuondoka kwa Askofu Mhogolo kumeacha
pengo kubwa siyo tu kwa Waumini wa Kanisa la Anglikana katika Dayosisi yake, Dayosisi
ya Kati, Dodoma bali pia kwa Waumini wote wengine wa Madhehebu hayo kote
nchini, na kwa kweli wapenda amani wote popote walipo.
“Ni kutokana na msiba huu mkubwa, ninakutumia wewe
Dkt. Jocob Chimeledya, Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, na Waumini wote wa Kanisa hilo Salamu zangu za
Rambirambi kutoka dhati ya moyo wangu kwa kuondokewa na Mtumishi huyu wa Mungu
aliyejitoa kikamilifu kuwatumikia Waumini wa Kanisa lake”, ameongeza kusema Rais
Kikwete na kuongeza,
“Kupitia kwako naomba pia Salamu zangu za
Rambirambi na Pole nyingi ziifikie familia ya Marehemu Askofu Godfrey Mdimi
Mhogolo kwa kuondokewa na Kiongozi na mhimili wa familia yao”.
Rais Kikwete ameiomba familia ya Marehemu kuwa na
moyo wa uvumilivu na subira katika kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na
Mpendwa wao kwa kutambua kuwa yote ni Mapenzi yake Mola.
“Ninaihakikishia familia ya Marehemu kuwa binafsi niko
pamoja nao katika kuomboleza msiba huu mkubwa kwa kutambua kuwa msiba wao ni
wetu sote. Namuomba Mwenyezi Mungu,
Mwingi wa Rehema aipokee na kuilaza Mahala Pema Peponi, Roho ya Marehemu Askofu
Godfrey Mdimi Mhogolo, Amina”, amemalizia kusema Rais Kikwete katika Salamu zake.
Imetolewa
na;
Kurugenzi
ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
28
Machi,2013
Social Plugin