Aliyesimama ni mkuu wa wilaya ya Shinyanga Anna rose Nyamubi,kushoto ni afisa habari kitengo cha habari Umoja wa mataifa Tanzania(UNIC) bi Usia Nkhoma Ledama |
Kufuatia
kuendelea kujitokeza kwa vitendo vya mauaji ya vikongwe (hususani akina bibi),Mkuu
wa wilaya ya Shinyanga Annarose Nyamubi
ameonesha kukerwa na kusikitishwa na vitendo hivyo dhidi ya wazee na kusema
kuwa sababu kubwa inayosababisha kuendelea kutokea kwa mauaji ya vikongwe hivi
sasa katika mkoa wa Shinyanga ni urithi wa ardhi yakiwemo mashamba makubwa na
mifugo wala siyo ushirikina kama wengi wanavyofikiria.
Mkuu huyo wa
wilaya ya Shinyanga ndugu Nyamubi ameyasema hayo juzi mjini Shinyanga akiwa
mgeni rasmi wakati wa warsha iliyoandaliwa na kitengo cha habari cha Umoja wa
Mataifa Tanzania ambayo iliwakutanisha pamoja wanafunzi wa shule 10 za
sekondari ikiwemo shule ya Uhuru,Buluba,Kizumbi,Chamaguha,Mazinge pamoja na
vyuo vilivyopo katika manispaa ya Shinyanga kama vile VETA,MUCCOBS na chuo cha
Ualimu cha Shinynga kwa lengo la kuwaelimisha kuhusu kazi mbalimbali za Umoja
wa mataifa ikiwemo malengo ya millenia hapa nchini kama vile haki za
binadamu,afya ya uzazi na elimu kwa watoto.
Nyamubi
alisema Mkoa wa Shinyanga bado unakabiliwa na changamoto ya mauaji ya vikongwe
na hali hiyo inaonekana kuwa ndiyo sifa
ya mkoa na kuongeza kuwa mauaji hayo hivi sasa hayatokani na uchawi wala imani
za kishirikina bali mauaji hayo yanatokana na wanafamilia kugombania mali za
urithi katika jamii.
“Vijana
tumieni ujana wenu kuleta mabadiliko,hasa katika suala hili la mauaji ya bibi
zetu,niwaambie ukweli kwamba sababu kubwa ya mauaji ya bibi zetu leo hii siyo
ushirikina,bali sababu kubwa ni suala la ardhi kwa maana ya mashamba makubwa na
mifugo”,alieleza Nyamubi.
“Tumebaini
kuwa hawa bibi zetu wanaolengwa kuuawa ni wale ambao waume zao walishafariki
dunia,na kwa mila tulizonazo wao ndiyo warithi wa mali hizo na katika hilo bibi
hao wanasahau kuwa wana watoto wakubwa wa kiume tena wameoa ambao nao
wanazitolea macho mali zile zile halafu bibi zetu wana kitu kimoja,huwa
wanachagua mjukuu mmoja wanakuwa karibu nao,ndiyo wanaanza kuwarithisha mali
hali ambayo inaleta chuki kati ya bibi,watoto na wajukuu”,aliongeza Nyamubi.
Alifafanua
kuwa kufuatia chuki inayotokana na nani arithi mali hizo ndipo wale watoto
wanaanza kutengeneza mipango ya kumuua bibi huyo ambapo kuna watu maalum
wanaolipwa pesa kwa ajili ya kutekeleza mauaji kwa kutumia mapanga na sasa
wamebuni mbinu nyingine ya kutumia aina flani na vishoka vidogo wanawapiga
vikongwe sehemu za uti wa mgongo ili wafe bila kupiga kelele.
“Wahusika
wakuu wa mauaji ya vikongwe ni watoto,tukiwakamata wanasema,sisi tumepata hata
uthibitisho kutoka kwa waganga wa kienyeji wanasema,wale watoto waliolipia
wauaji kutokana na hofu ya kuua huwa wanakwenda kuoshwa ili kuondoa laana ya
kuua wazazi wao”,alisema Nyamubi.
Kufuatia
hali hiyo aliwataka vijana wa Shinyanga kujadili kwa kina katika kuondokana na
mauaji hayo na kwamba watumie fursa mbalimbali zinazotolewa na Umoja wa mataifa
ikiwemo kutumia miradi ya umoja huo kupiga vita mauaji hayo ambayo kwa kiasi
kikubwa yanafanywa na ndugu wa karibu katika jamii lakini wakumbuke kuwa vijana
wa leo ndiyo vikongwe wa kesho hivyo hali inaweza kuwarudia wao.
“Katika
mambo muhimu ya kuzungumzwa na kupigwa vita ni hili la mauaji ya bibi
zetu,mauaji haya yanautia aibu mkoa wetu,wenye utajiri wa kila aina,na sasa
viwanda vingi vinajengwa hapa na vingine vilishaanza kufanya kazi,kwanini
vikongwe wauawe?,je nyinyi kama vijana mnafurahia hali hii?,simameni kidete
kuielimisha jamii,na nyinyi pia mmbadilike fanyeni kazi msitegemee urithi wa
mali kutoka kwa wazazi wenu,mauaji hayo mengi yanafanywa na vijana”,aliongeza
Nyamubi.
Akizungumza
katika warsha hiyo afisa habari kitengo cha habari Umoja wa mataifa Tanzania(UNIC) bi
Usia Nkhoma Ledama alisema lengo la Umoja wa mataifa kukutana na wanafunzi wa
shule za sekondari na vyuo mkoani Shinyanga ni kuwahamasisha vijana ili
wajue kazi zizazofanywa na Umoja wa mataifa lakini pia kuwaelimisha fursa za
umoja huo kwa vijana hivyo kuwaunganisha watu wa chini na umoja huo.
Aidha afisa
habari huyo aliwataka vijana waliopo shuleni na vyuoni kutumia fursa
zinazotolewa na Umoja wa mataifa ili kuleta mabadiliko katika jamii ikiwa ni
pamoja na kupigania haki za binadamu,afya ya uzazi,amani na kuwa
wajasiriamali ili kuondokana hali ya kutegemea ajira kutoka serikalini.
Katika hatua
nyingine Ledama alitumia fursa hiyo kuwataka wazazi na walezi wa wanafunzi
kufuatilia mienendo ya wanafunzi wao na kuwasaidia kwani elimu ndiyo njia pekee
ya kuondoa umaskini katika jamii huku akiwataka vijana kuachana na ngono ili
watimize ndoto zao na kujifunza kuwa wajasiriamali.
Social Plugin