Na Edward Kondela – Mwandishi wa habari (UTSS)
Shirika
la Under The Same Sun (UTSS) limetoa ufafanuzi wa taarifa iliyoripotiwa na
baadhi ya vyombo vya habari hapa nchini,ukiwemo mtandao huu wa Malunde1 blog ikimhusu mkazi mmoja wa mkoa wa Tabora
anayedaiwa kupata albinism ukubwani kuwa hana hali hiyo bali ana ugonjwa wa
vitiligo.
Akizungumza
katika ofisi za UTSS jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo hapa
nchini Vicky Ntetema, ameitaka jamii kuelewa kuwa albinism ni hali ya kurithi
kutoka kwa wazazi wote wawili na kwamba hauwezi kupata kwa kuathiriwa na dawa.
“Haiwezekani
mtu azaliwe bila albinism halafu aje apate albinism ukubwani, ni kwamba baba na
mama wanakuwa na vinasaba vinavyokuwa na albinism na vinapokutana wakati wa
kutunga mtoto ndipo mtoto mwenye albinism anazaliwa hivyo ni lazima urithi
kutoka kwa wazazi wako” amesema Vicky Ntetema.
Kwa
upande wake Dokta Jeff Luande mtaalam wa magonjwa ya saratani na mwenye uzoefu
mkubwa juu ya albinism kutoka Hospitali ya Ocean Road jijini Dar es Salaam, amesema
kukosekana kwa taarifa sahihi kunaweza kumsababishia mgonjwa kutofahamu hali
yake na hata kushindwa kupata matibabu au ushauri.
“Ngozi
kubadilika kuwa nyeupe, kwa mtu wa kawaida atajua ni albinism lakini kutumia
hili neno kwa huyu Bwana Masokola siyo sahihi, yeye amepata ugonjwa unaoitwa vitiligo
mara nyingi huwa yanatokea madoadoa meupe kwenye ngozi” amebainisha Dokta
Luande.
Amefafanua
kuwa ugonjwa huo huweza kutokea kutokana na matumizi ya dawa mbalimbali
zikiwemo zenye sulphur japokuwa ni kesi chache sana kwa mtu kubadilika mwili
mzima kama Bwana Masokola, ambaye huenda alipata ugonjwa huo baada ya kutumia dawa
yenye sulphur iliyoharibu mfumo wa kutengeneza rangi asili ya mwili.
Ameongeza
kuwa mtu aliyepata ugonjwa wa vitiligo kama Bwana Masokola, anapaswa kujikinga
na jua kama mtu mwenye albinism ili asipate saratani ya ngozi kwa kuwa ngozi
yake haina uwezo wa kuhimili miale ya jua.
Hivi
karibuni katika mitandao ya kijamii na gazeti moja hapa nchini limemripoti Bwana
Hafidh Masokola Damson mkazi wa mkoa wa Tabora anayedai kupata albinism baada
ya kunywa dawa aina ya Metakelfin hali iliyosababisha baadhi ya maswali kwa
jamii.