Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Uchakachuaji miradi ya maendeleo!!! TAKUKURU YAWATAKA WABUNGE ,MADIWANI NA WAKURUGENZI WA HALMASHAURI KUSOMA TAARIFA ZA MIRADI NA KUWAELIMISHA KUHUSU MIRADI HIYO

Kamanda wa taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU)mkoa wa Shinyanga Gasto Mkono
Wabunge ,madiwani na wakurugenzi wa halmashauri za wilaya mkoani Shinyanga wametakiwa kuwaelimisha wananchi kuhusu elimu ya uraia na  miradi mbalimbali wanayoianzisha katika maeneo yao ili kujua gharama za miradi.

Wito huo umetolewa  jana na kamanda wa taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa mkoa wa Shinyanga (TAKUKURU) Gasto Mkono  kwenye kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa huo kilichofanyika mjini  Shinyanga.

Mkono amesema kama wananchi wataelimishwa kuhusu miradi ya maendeleo itasaidia kwa kiasi kikubwa kupiga vita rushwa kwani takwimu zinaonesha kuwa miradi mingi inajengwa chini ya viwango na kusababisha wananchi kulalamika kuwa kuna rushwa imefanyika kutokana na kutojua gharama za miradi hiyo.

Kamanda huyo wa TAKUKURU mkoa amesema ni vyema madiwani,wabunge na wakurugenzi wa halmashauri wakawa wanatangaza miradi inayotekelezwa katika halmashauri za wilaya ili kupunguza kasi ya rushwa katika mkoa wa Shinyanga ambapo hivi sasa kuna malalamiko kuhusu miradi ya maendeleo ambayo baadhi imekuwa ikijengwa chini ya kiwango mfano ile ya barabara ambapo baadhi ya viongozi na wakandarasi wamekuwa wakilalamikiwa kuhusika zaidi.

Amewataka viongozi na wadau mbalimbali likiwemo jeshi la polisi kuendelea kushirikiana na taasisi yake huku akiwataka viongozi kuacha uoga  katika kupambana na rushwa pamoja na kwamba vita hiyo ni nzito kwani miongoni mwa wala rushwa ni watu wa karibu kabisa kama vile ndugu na marafiki.

Takwimu za mkoa wa Shinyanga katika kipindi cha kuanzia mwezi Januari hadi Desemba 2013 zinaonesha kuwa jumla ya tuhuma 15 kuhusiana na rushwa zilipatikana,ambapo kati ya tuhuma hizo 15,9 zimehusisha idara ya afya,3 zilihusisha halmashauri(TASAF) na 3 zilihusisha idara ya elimu,na katika kipindi hicho majalada 10 yalifunguliwa,8 yakapelekwa kwa mkurugenzi wa mashtaka(DPP)  wakati majalada manne,yalipata vibali vya mashitaka.

Katika kipindi hicho pia TAKUKURU imeshinda kesi 7 na kushindwa kesi 5 na jumla ya kesi mpya zilizofunguliwa mahakamani ni kesi saba.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com