Familia ya afisa mmoja wa Elimu nchini Kenya
imepigwa na butwaa baada ya kupata jeneza dogo likiwa limewekwa kwenye
mlango wao mjini Kisumu Magharibi mwa Kenya.
Kwa mujibu wa taarifa ya gazeti la Taifa Leo,
familia ya Afisa huyo Elias Oganda, mwenye umri wa miaka 56, ilipata
jeneza hilo dogo likiwa na mzoga wa Paka nje ya mlango wao na sasa
inaishi kwa hofu kubwa.
Polisi walifungua jeneza hilo na kupata mzoga wa
Paka ndani yake. Walishuku kuwa Paka huyo alinyongwa na kuwekwa ndani
ya jeneza hilo kwani hapakuwa na dalili yoyote ya damu.
Afisa mkuu wa polisi katika eneo hilo amesema kuwa hili sio tukio la kwanza kushuhudiwa katika eneo hilo.
Bwana Oganda naye alisema kuwa jeneza hilo
liligunduliwa na mkewe Joyce Oganda, mwenye umri wa miaka 50, usiku wa
manane alipotoka nje kujisaidia.
''Nia ya mtu aliyefanya kitendo hicho
haijulikani, mimi sijawahi kuhusika na mzozo wa ardhi , familia yangu haijawahi kupata ,utulivu kwa mwaka
mmoja uliopita kwani nimekuwa nikifanyiwa uchawi mara kwa mara.'',alisema Oganda.
''Hii ni ardhi ya babaangu na sielewi kwa nini watu wanataka kunitishia maisha kwa kutumia uchawi.''
Wakazi wa eneo hilo walifika kwa wingi katika nyumba ya bwana
Oganda kushuhudia mganga wa jadi aliyeletwa katika nyumba hiyo kutoka Sirari
mpakani mwa Kenya na Tanzania kujaribu kujua ni nani aliyehusika na
kitendo hicho.
Social Plugin