BADO
tatizo la unyanyasaji dhidi ya Watoto limeendelea kukua kwa kasi,
Wilayani Babati Mkoani Manyara, ambapo Jeshi la Polisi Mkoani humo,
linamshikilia Mama wa kambo wa Mtoto wa kiume, anayedaiwa kutaka
kumlawiti mtoto wake na kisha kumchoma na kijinga sehemu za siri.
Kaimu
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani humo, Mussa Marambo alithibitisha
kukamatwa kwa mwanamke huyo mkazi wa Magugu, ambapo alisema tukio hilo
lilitokea juzi Machi 9, mwaka huu saa 12 jioni, wakati watoto hao
wakicheza mchezo wa kujificha na kumtaja mtoto anayedaiwa kufanya
kitendo hicho kuwa ni Joakim Mkumbo (9).
Alimtaja
mwanamke anayeshikiliwa kuwa ni Lydia Mkumbo (39), anayedaiwa kumchoma
sehemu za siri Mtoto wake wa kambo, kwa tuhuma za kutaka kumlawiti mtoto
wake, ambapo Jalada la mtuhumiwa huyo limepelekwa kwa Mwanasheria Mkuu
wa Serikali akisubiri kufikishwa Mahakamani, huku mlalamikaji akiwa
amelazwa katika Kituo cha Afya cha Magugu akiendelea kupata matibabu
baada ya afya yake kuelezwa kuwa ni mbaya.
“Aliumizwa
sehemu za siri kwa kumchoma na kijinga cha moto, uchunguzi wa wali
umeonyesha kuwa, chanzo cha tukio hilo kinaweza kuwa Mama huyu alihisi
huyo kijana alikuwa na nia ya kutaka kumlawiti mtoto wake” alisema
Marambo.
Tukio
hili ni la pili kutokea Wilayani humo, ambapo juma lililopita
Mwanafunzi wa Kike anayeishi na Baba yake mzazi, Mwanafunzi wa darasa la
Kwanza katika Shule ya Msingi Darajani, mwenye umri wa miaka (10)
alimtuhumu wazi wazi Baba yake mzazi kwa Mwalimu wake kuwa amekuwa
akimbaka mara kadhaa nyakati za usiku licha ya kutoa taarifa kwa ndugu
wa Mama yake bila kuchukuliwa hatua yoyote.
Kufuatia
kutokea kwa matukio kadhaa kama hayo, Kamanda huyo amewataka wananchi
kuacha tabia ya kunyamazia matukio kama hayo, na hivyo kuwataka wananchi
kushirikiana na Serikali za Mitaa kutoa taarifa hizo mapema.
Na Dotto Mnzava-Manyara