Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Unyama!! MAMA MJAMZITO APIGWA NA MMEWE,AKATWA MGUU KWA PANGA,AMWAGIWA TINDIKALI,MME AJIFANYA AMEZIMIA


“Ni zaidi ya miezi sita tangu nifanyiwe ukatili na mume wangu na mama mkwe. Nahangaika kuuguza mguu niliokatwa kwa panga  kunyunyiziwa maji ya betri. sijui kama utapona. 
Kichanga nacho kinasumbua, jamani nimekosa nini mimi kwa Mungu.”
Ni maneno yenye kutia simanzi na ambayo yanaamsha kilio. 

Maneno ya  ya Anna Sabai (PICHANI)(20) mkazi wa Kitongoji cha Manyata Kijiji cha Nyamakendo Kata ya Mbalibali, wilayani Serengeti, ambaye anapaza sauti kutaka kujua  walipo wanaharakati ambao kwa hali aliyonayo , angeweza kupata msaada kutoka kwao.
Ukatili aliofanyiwa Anna, mama wa watoto wawili katika ndoa yake na Hamisi Sabai (20) yenye migogoro na ambayo inazidi kuuweka Mkoa wa Mara kwenye taswira mbaya kutokana na uwingi wa matukio ya ukatili dhidi ya wanawake.
Agosti Mosi,  2013 ikiwa ni siku ambayo wakazi wa wilaya hiyo humiminika mnadani, Anna akiwa na uja uzito wa miezi  tisa na akihesabu siku tu kwa ajili ya kujifungua, aliamriwa na mume wake kwenda kuchunga ng’ombe, bila kujali hali yake.
“Kwa kweli nilikuwa na hali mbaya sana,” anakumbuka Anna wakati anaongea  kuhusu ukatili dhidi yake.

 “Nikiwa malishoni nilikaa chini ya kivuli huku ng’ombe wakiendelea kula majani. Hali ilivyozidi kuwa mbaya nilisinzia.


 Alipokuja mume wangu akanikuta nimelala na hapo hapo akaanza kunishambulia kwa kipigo, akidai kuwa nilikuwa na mwanamume kutokana na mapenzi kunoga ndio maana nilisinzia na kuacha ng’ombe wanazagaa.”
Anasema pamoja na kujieleza na kwa kuzingatia hali yake, walipofika nyumbani mama mkwe wake Bhoke Sabai alizidi kumtia hasira kijana wake  akidai kuwa nilikuwa na mwanaume, natakiwa kupewa kipigo ili iwe fundisho.
“Pamoja na kuwa wakati ananipiga sikuwa najitetea, bado akaona aache fimbo na akachukua panga na kunikata mguu wa kushoto,” anasema Anna huku akitokwa na machozi.
“Niliumia sana... nikatamani kufa, maana hali ilikuwa mbaya. Sikuwa na msaada. Baadaye akanifungia ndani ili watu wasijue; wala hakuna kwenda kutibiwa.”
Amwagiwa tindikali ili kuzuia damu isitoke 
Huku akiwa amebeba mtoto wake na kutembea kwa shida, Anna anasema ili watu wasijue unyama aliotendewa, walileta maji ya betri na kumwagia kwenye kidonda. 
“Maumivu yalikuwa zaidi ya uchungu wa kujifungua. Nilifikia hatua kama ningepata kitu cha kujimaliza, ningejiua. Nilikuwa nasumbuliwa na mimba na huku naumizwa hivi,” analalamika. “Jamani wanaharakati wanaotetea wanawake wako wapi maana nitakatwa mguu hivi hivi.”
Anasema matokeo yake mguu ukaoza kwa kuwa alikaa ndani muda mrefu na kwamba ndugu zake hawakuambiwa na mama mkwe wake alikuwa akiendelea kumkejeli kila wakati.
 Sijaona watu wenye roho ya kikatili kama hao, kwa kuwa walilenga kuniua bila kosa,” anasema.
 
Aokolewa na mama yake mzazi
Anasema kuwa akiwa amekata tamaa kwa kuwa alikuwa anafungiwa ndani ili majirani wasijue, kuna wakati alilazimika kumlilia Mungu, kwa nini afe bila ndugu zake kumwona. Ndipo bila kutarajia alishtukia mama yake mzazi, Mnanka Chacha (48) akifika hapo  baada ya kutaarifiwa na majirani.
“Nilipomwona mama nikasema basi sasa hata kama nikifa, niko katika mikono salama kwa kuwa huenda maiti yangu itapewa heshima kama binadamu. Nilijua kama ningefia mkononi mwa hao  huenda maiti ingetupwa kama mbwa. Nilijisikia ahueni kwa kumuona mama,” anabainisha.
Afikishwa hospitali kwa matibabu
Anasema kwa kupitia polisi mama yake alimfikisha Hospitali Teule ya Nyerere kwa ajili ya matibabu na madaktari walipomwona walimwambia kuwa hawana uwezo tena wa kumtibu kwa hali aliyonayo. Hivyo wakamwandikia barua kwenda Hospitali ya Rufaa ya Bugando ya jijini Mwanza.
Akosa pesa 
Kutokana na ukata wake, alishindwa kwenda Bugando na kuamua kurudi nyumbani kwake kwa ajili ya kutafuta wasamaria wema, ili aweze kwenda naye Mwanza kwa ajili ya matibabu.
Mume achana barua ya rufaa
Katika kuhakikisha juhudi za kupelekwa hospitali hazizai matunda, akiamini kuwa mume wake alikuwa ameishajirudi, alimpa barua ya rufaa ili watafute fedha za matibabu, lakini yeye akaichana na kumuacha asijue la kufanya.
“Alichana barua ya rufaa ikawa sina namna yoyote ya kwenda kutibiwa Hospitali ya Rufaa ya Bugando. Ikabidi nikae tu nyumbani nikiangalia mguu wangu unaoza. Kwa kweli nahitaji msaada kwa watu wanaoguswa maana kula yangu na hata ya mtoto ni ya shida. Siwezi kwenda zaidi ya hapa,” anasema.
Anabainisha kuwa mumewe alichana barua kwa madai kuwa nimetoa siri polisi na kwa watu wengine na ndio maana akaamua kumkomoa kwa kuichana ili kupoteza ushahidi.

Ajifungua mtoto wa kiume
Agosti 24, 2013 ikiwa ni siku 24 tangu amefanyiwe ukatili huo, alijifungua mtoto wake wa pili wa kiume ambaye ndiye anazunguka naye kwa sasa  na kama si  msaada wa wasamaria  wema  kumpeleka Kituo cha Afya cha Machochwe, huenda angepata tabu zaidi.
“Kwa sasa hakuna fedha zozote za matumizi ambayo mume wangu anatoa  kwa ajili ya mtoto. Dada amenichukua  na sasa niko kwake Mtaa wa Bomani mjini Mugumu na mwanangu huyu maana yule wa kwanza alifariki dunia,” anabainisha.
Anawaomba wanawake wanaofanyiwa ukatili wafike polisi kutoa taarifa, kwa kuwa amebaini polisi kuna Dawati la Jinsia na mhusika wa dawati, aaliyemtaja kwa jina la Sijali, amekuwa kama ndugu. Anamnunulia dawa na amehangaika naye kwa muda mrefu bila kuchoka.
Dawati la Jinsia wafanikisha kuwanasa watuhumiwa
Katibu wa Dawati la Jinsia Polisi Wilaya ya Serengeti, Sajenti Sijali Nyambuche anasema kwa muda mrefu wamekuwa wakiwasaka watuhumiwa, lakini wanakosa ushirikiano kutoka kwa jamii ikiwemo baadhi ya viongozi.
“Tukajifanya kusahau, nao wakajisahau wakaendelea na maisha ikiwemo kilimo cha tumbaku na tukafanikiwa kuwakamata kirahisi, mama na mtoto kwa tuhuma za kujeruhi,” anasema Sijali.
Anasema wamewafungulia jalada namba MUG/DAW/IR/30/2014 kwa tuhuma za kujeruhi. Katibu wa dawati amekuwa akimpeleka hospitali ili kupata matibabu ya mguu.   
        
Daktari anasema misuli ilivurugwa
Dk. Richard wa Hospitali Teule ya Nyerere anasema baada ya kupiga picha ya X-ray wamebaini kuwa mishipa haikukatwa wakati wa shambulio hilo, bali kuna misuli iliyoharibiwa, kutokana na hali hiyo mguu huo utakuwa kama mwenye ugonjwa wa matende.
“Ni bora akabaki hivyo, akawa anapata dawa inapotokea maumivu...kwa kuwa vidole vimeshakufa ganzi. Zaidi ya hapo ni kukata mguu na kumfanya mlemavu na pia kupata maumivu mapya,” alisema mganga huyo na kushauri  aendelee kupata dawa badala ya kukata mguu.
Mume ajifanya amezimia asitoe maelezo

Anna anadai kuwa baada ya Sabai na mama yake kukamatwa na kulala mahabusu, baba huyo alijiangusha na kujifanya amezimia baada ya kutakiwa  kutoa maelezo. Katika maelezo yake baada ya kuzinduka, Sabai alidai mkewe alilala na mwanamme mwingine  ambaye hakumtaja na kuacha ng’ombe wanazunguka.
Hata hivyo, alikana kumwekea maji ya betri kwenye kidonda, lakini akashindwa kueleza sababu za kumkata mguu, kutompeleka hospitali na kuchana barua ya rufaa. Mama yake alidai yeye hakuhusika na ukatili huo.
Mratibu wa Kitengo cha Kuzuia Ukatili wa Kijinsia wa CCT wilayani Serengeti, Sophia Mchonvu, anasema matukio ya ukatili wa kijinsia yameshika kasi wilayani hapo na kuomba vyombo husika kutoa adhabu kali ili liwe fundisho .
Tukio kama hilo lilitokea mwaka 2000 wakati mwanamke aitwaye Kadogo Waya alipopigwa na mume wake kutokana na wivu wa mapenzi na kumwagiwa tindikali na kusababisha miguu kuoza na baadaye kukatwa. Hivi karibuni mkazi mwingine wa Kijiji cha Bisarara wilayani hapa alimjeruhi  mke wake na kumng’ata mtoto akidai mkewe aligoma kwenda kuchunga ng’ombe usiku.

 Na Anthony Mayunga, Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com