Baadhi ya wadau wa zao la Pamba katika mikoa ya
Shinyanga na Mwanza wamewaomba wakuu wa mikoa na wilaya kutumia busara zaidi
pale wanapowahamasisha wakulima na wanunuzi wa zao hilo kuhusiana na
utekelezaji wa mpango wa kilimo cha mkataba badala ya kutumia vitisho.
Ombi hilo limetolewa juzi na baadhi ya
wawekezaji katika zao la Pamba katika mikoa ya Shinyanga na Mwanza kufuatia
tukio la hivi karibuni la mkuu wa mkoa wa Geita, Magalula Said Magalula kutoa
amri ya kuwekwa ndani kwa wawakilishi wa makampuni matatu ya ununuzi wa pamba
katika mkoa wake.
Wakizungumza na waandishi wa habari mjini
Kahama baadhi ya wamiliki wa makampuni ambayo wawakilishi wao waliwekwa ndani
kwa masaa manne kutokana na agizo la mkuu huyo wa mkoa walidai kuwa kitendo
alichokifanya kilikuwa ni kinyume na dhana nzima ya utawala bora.
Wawakilishi waliowekwa ndani hivi karibuni kwa amri hiyo ya
mkuu wa mkoa wakati wa kikao cha wadau wa zao la pamba mkoani Geita ni pamoja
na mwakilishi wa kampuni ya Fresho Investment Ltd., Kahama Oil Mill Ltd. na ICK
Cotton Co. Ltd.
Walisema suala la kilimo cha mkataba ambacho
kina lengo la kumkomboa mkulima aweze kunufaika na kilimo chake cha zao la
pamba linaungwa mkono na kila mdau wa zao hilo isipokuwa kinachotakiwa kabla ya
utekelezaji wake ni kuondoa changamoto zote zilizobainika katika kikao cha
wadau kilichofanyika jijini Mwanza Oktoba 20, 2013.
Mmoja wa wamiliki wa makampuni ya ununuzi wa
pamba mjini Kahama (jina tunalo) alisema kitendo alichokifanya mkuu wa mkoa wa Geita ni cha
kusitikisha na kinaweza kusababisha watu washindwe kutekeleza vyema mpango huo
wa kilimo cha mkataba iwapo wataamua kuutekeleza kwa shinikizo la viongozi wakuu
wa serikali badala ya hiari yao wenyewe.
“Binafsi sikuridhishwa na hatua ya mkuu wa
mkoa, kutumia vitisho kwa lengo la kututisha siyo suluhisho la watu kutekeleza
kilimo cha mkataba, kuweka ndani watu ni kuwadhalilisha, na ikiwezekana
tunaweza kumpeleka mahakamani ili atusafishe, maana kitendo chake kimeonesha sisi
siyo waaminifu kwa wakulima tunaofanya nao kazi,”
“Ametoa agizo watu wamewekwa ndani, baada ya
masaa manne polisi wamewaachia kutokana na kukosa shitaka la kuwafungulia, sasa
huu siyo utawala bora, kilimo cha mkataba kitafanikiwa vizuri kwa watu
kuelimishwa kwa kina lakini pia ni pamoja na kuondoa changamoto zote
zilizojitokeza wakati wa majaribio yake,” alieleza mdau huyo.
Hata hivyo kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Geita,
Magalula Said Magalula akizungumzia tishio la kutaka kupelekwa mahakamani kama
ilivyodaiwa na baadhi ya wawekezaji hao alisema hiyo ni haki yao ya kikatiba
iwapo wataamua kufanya hivyo na yeye atakwenda kutoa ushahidi wake kwa nini
alitoa amri hiyo.
“Kama hawa wenzangu wataamua kunipeleka
mahakamani, hiyo ni haki yao kabisa, lakini agizo langu lilitokana na wao
kukiuka makubaliano tuliyokuwa tumekubaliana katika kikao cha wadau wote wa zao
la pamba kilichofanyika hivi karibuni, walipewa viuatilifu wakiviuze kwa
wakulima kwa mkopo wao waliuza kwa fedha taslimu,”
“Lakini hata kama
walikuwa na tatizo katika
kusambaza viuatilivu hivyo kwa njia ya mkopo basi ilikuwa ni wajibu wao
waje
ofisini wanieleze tatizo, hawakufanya hivyo waliuza kwa fedha taslimu
lakini
hata hivyo fedha za mauzo hawakuzirejesha bodi ya pamba, kitendo chao
kilisababisha baadhi ya wakulima wakose viuatilivu kwa vile hawana
fedha,” alieleza Magalula.
Kwa upande mwingine mkuu huyo alishindwa kufafanua iwapo
wawekezaji hao walifikishwa mahakamani baada ya kutoa agizo wakamatwe na
wawekwe ndani ambapo alisema anayepaswa kutoa jibu iwapo walipelekwa mahakamani
au hawakupelekwa ni kamanda wa polisi wa mkoa wa Geita.
Hata hivyo taarifa kutoka Jeshi la Polisi
mkoani Geita zilieleza watuhumiwa wote waliokuwa wamekamatwa waliachiwa huru baada ya kukosekana kwa kifungu cha sheria ambacho
kingetumika kuweza kuwafikisha mahakamani.