WANNE WAFARIKI KWA KUPONDWA NA UDONGO WAKICHIMBA DHAHABU HUKO KAHAMA


Watu wanne wamefariki dunia na wengine kadhaa bado wamenasa kwenye kifusi katika machimbo madogo ya Kalole kata ya Lunguya wilayani Kahama mkoani Shinyanga kufuatia kuporomoka kwa duara waliyokuwa wanachimba dhahabu.

Diwani wa Kata ya Lunguya Benedicto Manwari amesema tukio hilo limetokea jana jioni, na kwamba hadi kufikia jioni ya leo miili ya watu wanne imeopolewa na majeruhi mmoja ambaye anapatiwa matibabu katika kituo cha Afya Lunguya.

Manuari amesema miili hiyo mitatu ni ya wakazi wa hapo Kalole na mmoja ni wa kutoka Bariadi mkoani Simiyu na tayari umekwishasafirishwa na kwamba Yule majeruhi ambaye amevunjika mkono na ana jeraha usoni ni mtu wa Morogoro.

Amesema kufuatia sensa iliyofanywa, inakisiwa watu watatu wakazi wa kijijini hapo bado wamenasa katika kifusi hicho ingawa juhudi za uopoaji bado zinaendelea japokuwa hakuna msaada wowote wa zana za kisasa ulioweza kupatikana.

Manuari amesema Serikali ngazi ya wilaya imepewa taarifa hizo na Jeshi la Polisi limekwishafika kwenye eneo la tukio.

Balaa la watu kupoteza maisha katika machimbo madogo ya madini bado halijapata jibu la kudumu kwa wilaya ya Kahama ambayo imekuwa ikiibuka kugunduliwa madini karibu kila sehemu ya ardhi yake.
via>>Kahama fm

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post