Baadhi ya makahaba wenye umri mdogo wakiwa kwenye mawindo yao. |
Watoto wa kike wenye umri wa hadi miaka 14
wanadaiwa kufanyishwa biashara ya ukahaba China kutokana na
kusafirishwa na baadhi ya Watanzania wasio waaminifu.
Mji uliotajwa kuwa na watoto hao kutoka nchini China ni wa Guangzhou.
Imeelezwa wamekuwa wakinyang'anywa hati zao za kusafiria na kuwataka watoe dola za Marekani 8,000 kuzigomboa.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe
aliyasema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu
masuala mbalimbali yanayohusu wizara yake nchini China.
Alisema mwezi uliopita alipata mwaliko nchini humo na kubaini kuwapo biashara hiyo katika mji wa Guangzhou.
Alisema kutokana na taarifa hizo, ameitaarifu Wizara ya Mambo ya
Ndani kuunda timu kwenda nchini humo na pia kubaini wanaoendesha
biashara hiyo kuhakikisha inakomeshwa mara moja.
Alisema imebainika wapo baadhi ya Watanzania wanakwenda China kwa kutumia nyaraka bandia hati za kusafiria za nchi nyingine.
Hata hivyo alisema siyo kwamba Watanzania walioko mji huo wote
wanaendesha biashara haramu au hawakai kihalali kwa kuwa wapo wengi na
wameanzisha ofisi ya diaspora wakiishi kihalali.
"Lakini wapo walioanzisha biashara hiyo na kuvunja heshima ya
binadamu na nchi kwani kuna msichana mmoja alifariki kwa kuuawa nchini
humo wiki iliyopita na upelelezi unaendelea," alisema Membe.
Alisisitiza kuwepo Watanzania wanaoishi nje ya nchi zaidi ya milioni
tatu na wengi wao wakiishi vizuri. Lakini wengine wanashutumiwa kwa
kutoitendea haki nchi kwa kufanya vitendo visivyo halali.
Aliomba Watanzania hususan watoto wa
dogo wa kike kutorubuniwa kupelekwa nje kwa ahadi za kupata pesa na maisha mazuri.
Membe alisema ni vyema kutii kanuni na sheria kupunguza wanaopata
matatizo ikiwa ni pamoja na kukataa kutumika kubeba dawa za kulevya kwa
kupewa fedha kidogo ambapo wakati mwingine husababisha kifo.
Alisema Oktoba mwaka huu, Rais Jakaya Kikwete anatarajia kufanya
ziara China na ni mategemeo kwamba matatizo yaliyojitokeza wakati wa
ziara yake yatakuwa yamefanyiwa kazi.
Wakati huo huo Waziri Membe alisema nchi 10 zinatarajia kufungua
balozi zake nchini. Miongoni mwake ni Australia, Kuwait na Comoro.
Alisema kwa sasa nchi hizo zinatafutiwa viwanja kwa ajili ya balozi
hizo pamoja na maeneo ya kuishi jambo ambalo litaongeza ajira na
mzunguko wa fedha.
Social Plugin