Imeelezwa kuwa Zahanati ya kijiji cha Singita kata ya
Usanda wilaya ya Shinyanga inakabiliwa na uhaba wa maji hali inayowalazimu akina mama wanaokwenda kujifungua kwenda na maji yao ambapo wakati mwingine hulazimika kununua hayo yanaoyouzwa shilingi mia mbili kwa dumu la lita ishirini.
Wakiongea na waandishi wa habari waliotembelea zahanati hiyo akinamama walisema wanapokwenda kujifungua wamekuwa wakilazimika kununua maji kwa ajili ya kufulia nguo zao na kuoga jambo ambalo limekuwa ni changamoto kwao kwani wanatumia gharama kubwa wakati kipato chao ni kidogo.
Walisema mbali na Zahanati hiyo kukosa huduma ya maji lakini pia katika zahanati hiyo kuna ukosefu wa dawa wa mara kwa mara,ukosefu wa maabara na baadhi ya vifaa tiba na wamekuwa wakilazimika kufuata vipimo vingine katika hospitali ya mkoa wa Shinyanga au kwenye maduka ya dawa ya watu binafsi .
“Katika suala la maji tunatumia gharama kununua dumu moja shilingi 200 kwa kipindi hiki cha masika lakini msimu wa kiangazi maji huwa adimu tunalazimika kununua dumu moja mpaka shilingi 600 ili kuweza kuoga na kufua pindi tunapojifungua,isitoshe kuna uhaba wa dawa, maabara ya kupata vipimo vya magonjwa mengine kama kifua kikuu,kichocho na mengineyo”alisema mkazi wa kijiji hicho Hawa John.
Kwa upande wake muuguzi wa zahanati hiyo Leticia Anthony alisema kuwa kweli Zahanati inachangamoto ya uhaba wa maji hivyo hata wao hulazimika kununua kwaajili ya matumizi ya usafi,pia akina mama hao wanapokuja kujifungua hulazimika kununua maji ya kuoga na kufulia dumu lenye lita ishirini shilingi 200.
“Kweli zahanati hii haina maabara,vifaa tiba,vifaa vilivyopo ni kwa ajili ya upimaji malaria na maambukizi ya virusi vya ukimwi (VVU) ikiwa wastani wagonjwa kwa siku ni 60 hadi 70 zaidi ni watoto wenye umri chini ya miaka mitano huja kwa maradhi ya malaria na wakubwa kwa maradhi ya kikohozi ambapo wanaokwenda kujifungua kwa mwezi hufikia zaidi ya 40”alisema Antony.
Naye ofisa afya kata ya Usanda Mussa Chande alisema kuwa Zahanati hiyo inahudumia vijiji vitano vya Singita, Shagaluba,Manyada, Nzagaluba, na Igaganulwa na katika kata nzima kuna idadi ya watu zaidi ya 15,000
Diwani wa kata hiyo Abeid Aljabir alikiri kuwepo kwa uhaba wa maji katika Zahanati hiyo na kwamba tayari kuna mabomba ya maji ambayo tangu yawekwe hayajawahi kutoa maji hali ambayo imekuwa ikiwalazimu akinamama kununua maji huku akiiomba serikali kuwapatia maji kutoka mradi wa ziwa Victoria ili kuondoa kero hiyo.
via>>Sungwakareny blog