Jana April 16 2014 UKAWA wakiongozwa na Profesa Ibrahim Lipumba wakati bunge likiwa katikati waligoma kuendelea nalo na kuamua kutoka nje kwa kile wanachosema ni ubaguzi na matusi pamoja na mapungufu mengine ambayo hawawezi kuyavumilia.
Baada ya hayo mwenyekiti wa bunge la katiba Mh. Samwel Sitta leo April 17 2014 akatumia sekunde kadhaa tu baada ya bunge kuanza kwa kusema ‘jana kumetokea jambo moja la kusikitisha na kwa hakika baadhi yetu tumesononeka sana na tukio la jana la wenzetu wanaitwa UKAWA kutoka nje ya ukumbu huu na hadi sasa hawajaniambia kama wametoka moja kwa moja au vp, kwa vyovyote vile jambo lile halikustahili’
‘Katika nchi yoyote kwa Mwananchi kuteuliwa kuwa miongoni mwa wale ambao wanaaminiwa na nchi kutunga katiba mpya ya nchi ni heshima ya kipekee kabisa, ni dhamana ambayo inatakiwa kuchukuliwa kwa uzito wowote kwa sababu utungaji wa katiba ni jambo la mara moja pengine kwa vizazi viwili vitatu’
‘Nilivyokua naangalia jana katika TBC1 maelezo yaliyotolewa na kiongozi wa UKAWA Prof. Ibrahim Lipumba kwamba wametoka kwa sababu ya lugha ya matusi na ubaguzi, kwa sababu ya Waziri mmoja wa serikali yetu amenukuliwa katika gazeti eti kasema mambo ambayo wao yamewaudhi yanadhihirisha ubaguzi bila hata Waziri huyo kupewa nafasi ya kueleza aliyoyasema’
‘Tumemuita Mh. Lukuvi alikua anaelekea Airport kwa matibabu, tumemuita arudi hapa na atatoa maelezo ambayo kama ni yale aliyoniambia mimi basi sijui watu walimnukuu vipi mpaka wenzetu kuona kwamba aliyoyasema yamewaudhi kiasi hicho lakini ukweli utabainika’
‘Wakati wote tumeushuhudia mwendelezo ambao tumeendelea kuuvumilia kwa nia njema kwamba tufikie mwisho mwema wa kutunga katiba, nyinyi nyote mnafahamu kanuni za bunge hili maalum zinapendelea wachache na tumefanya hivyo makusudi, ofisi yangu imekua wazi kupokea malalamiko ya yeyote ambae kaonewa’
‘Nimeitisha mkutano wa dharura wa kamati ya uongozi ili tuweze kuelewana namna ya kushughulikia jambo hili, ikiwa wenzetu wanatusikia na ikiwa bado wako Dodoma kwa sababu baadhi yao ni wajumbe wa kamati ya uongozi, waje watueleze kwa undani hatma ya vitendo vyao kwa sababu vina athari kisheria na kiutawala, wamejiuzulu au kutoka nje kuonyesha hisia zao alafu watarejea?’ wawepo ili tuzungumze tusaidiane’
‘Kazi iliyopo mbele yetu sio kazi ambayo unaweza kuisusa tu, mi sipendi niingie katika kauli matusi na ubaguzi lakini katika maeneo ya haki za binadamu, mtu anaedai kabaguliwa alafu anaondoka na kundi lake wanaimba Interahamwe, huu ni mwaka wa 20 toka mauaji ya Kimbari kule Rwanda, na neno iterahamwe hapa Afrika ni tusi la mwisho kabisa kwa sababu lina maana ya mtu mwenye chuki ambae yuko tayari kutekeleza mauaji tena ya Kimbari’
‘Sisi tumevumilia hata jina la mkusanyiko wao, (UKAWA) wao wanadai ndio umoja wa katiba ya Wananchi kama vile tunachokifanya humu sio cha Wananchi lakini tumevumilia tu manake hata jina hilo ni la kibaguzi, itakuaje kikundi kitoke nje chenyewe ndio kiseme ndio kinatunga au kinasimamia Wananchi kuliko sisi wengine wote tuliomo humu’
‘Sababu za kitendo chao jana hazitoshi, mlango wangu uko wazi na nimeongea pia na Waziri mkuu, yeye kama kiongozi pia wa chama cha mapinduzi pia mlango wake uko wazi, kama kuna jambo limejificha tujadiliane ili turudi kuendelea kutunga katiba ya Wananchi’