Jengo la darasa katika shule ya msingi Mwamashimba linalotumika kama makazi ya walimu.
Jengo la mwanzo kabisa katika shule ya msingi Mwamashimba ambalo hivi sasa linatumika kama jiko kwa ajili kupikia uji kwa wanafunzi,shule hiyo ni miongoni mwa shule ambazo zinapata huduma ya uji katika wilaya ya Kishapu |
Choo katika shule ya msingi Mwamashimba ambacho
kimekwama ujenzi wake.Hapo ni upande wa mbele wa choo hicho,katika upande wa nyuma katika choo hicho baadhi ya matundu yanatumiwa na wanafunzi wa shule hiyo kutokana na ukosefu wa
choo katika shule hiyo.
Moja ya matundu ya vyoo katika choo ambacho hakijakamilika ujenzi wake kinachotumiwa na wanafunzi wa shule ya msingi Mwamashimba kutokana na ukosefu wa choo katika shule hiyo. |
Shule ya msingi Mwamashimba iliyopo katika kijiji cha
Mwamashimba kata ya Mwamalasa wilayani Kishapu mkoani Shinyanga inakabiliwa na
changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa choo,uhaba wa madawati na nyumba za walimu ambapo hivi sasa
walimu wanalazimika kuishi kwenye vyumba vya madarasa.
Hayo yamebainika juzi baada ya waandishi wa habari
kutembelea shule hiyo na kujionea hali halisi ya mazingira ambapo walishuhudia
walimu wakitumia vyumba vya madarasa kama makazi yao katika shule hiyo.
Mwalimu mkuu wa shule hiyo Elias Zengo
alisema shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 1976 ina jumla ya wanafunzi 492 na
walimu tisa pekee wa kiume 8 na mwalimu wa kike mmoja.
Alisema tatizo kubwa linaloikabili shule hiyo ni
upungufu wa nyumba za walimu kwani zilizopo sasa ni nyumba mbili pekee hali
inayowafanya baadhi ya walimu kuishi kwenye vyumba vya madarasa.
Mwalimu Zengo inakabiliwa na ukosefu wa choo cha
wanafunzi hali inayowafanya wanafunzi kutumia choo ambacho hakijakamilika baada
ya ujenzi wake kukwama na kuongeza kuwa pia upungufu wa madawati unasababisha baadhi
ya wanafunzi kukaa chini.
“Kuna baadhi ya wanafunzi wanalazimika kukaa chini,hii
ni changamoto na madarasa haya hayajasakafiwa,madarasa mengine yana kokoto,hata
hivyo tayari kuna fedha zimetengwa na halmashauri ya wilaya kwa ajili ukarabati
wa madarasa haya”,aliongeza mwalimu Zengo.
Kwa upande wake afisa mtendaji wa kijiji cha
Mwamashimba ilipo shule hiyo Julius Emmanuel alikiri kuwepo kwa changamoto hizo na kuongeza
kuwa wanajiandaa kufanya mkutano na wananchi ili kuangalia namna ya kuzitatua
hizo kama vile kuchanga pesa kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu.
“Mara nyingi,wananchi wa kijiji hiki wamekuwa mstari wa
mbele kuchangia miradi ya maendeleo,hata ujenzi wa choo ambacho hakijakamilika
umetokana na nguvu zao,na ujenzi ukifikia usawa wa renta ndiyo huwa tunaomba
msaada kutoka serikalini”,alisema afisa Mtendaji.
Naye diwani wa kata ya Mwamalasa ilipo shule hiyo
ambaye pia ni mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Kishapu Justine Sheka
alisema suala la walimu kuishi kwenye vyumba vya madarasa linatokana na shule
hiyo kutokuwa na wanafunzi wa kutosha na kutokana na upungufu wa nyumba za
walimu.
“Shule hii ni kongwe imejengwa mwaka 1976,mimi ni
diwani wa kata hii kupitia CCM tangu mwaka
1994, shule hii ilikuwa na madarasa ya tope ,tukajenga mapya ,wanafunzi
wakawa wachache,na kwa sababu ya upungufu wa nyumba za walimu tukatumia busara
kuyageuza baadhi ya madarasa kuwa nyumba
za walimu”,alisema Sheka.
Hata hivyo Sheka alisema tayari jumla ya shilingi milioni 9 zimetengwa na halmashauri ya wilaya ya Kishapu kwa ajili
ya ujenzi wa vyoo katika shule hiyo na shilingi milioni 30 kwa ajili ya
madawati katika shule za msingi wilayani humo ikiwemo shule ya msingi
Mwamashimba.
Na Kadama Malunde-Kishapu
Social Plugin