Wananchi katika kata ya Isulwa Butundwe wilayani
Geita mkoani Geita wametishia kuifunga ofisi ya mtendaji wa kata hiyo Sadik
Masalu kwa tuhuma ya kutumia pesa za watoto wanaoishi mazingira magumu kwa
matumizi yao binafsi.
Afisa
mtendaji huyo anadaiwa kushirikiana na diwani wa kata hiyo kupitia CCM James Maweda
kutumia kwa matumizi yao binafsi shilingi milioni moja na laki 8 pesa za watoto
yatima zilizotengwa kwa ajili ya kuwasomesha.
Wakiongea kwa nyakati tofauti jana wananchi hao walisema
kuwa shilingi laki nane zilitolewa na halmashauri ya wilaya ya Geita kwa ajili
ya kusomesha watoto wenye mazingira magumu wanatoka kata hiyo.
Waliongeza kuwa shilingi milioni moja ni marejesho ya asilimia
ishirini ya mapato yanayorudishwa katani kutokana na mapato yanayokusanywa kwa
ajili ya maendeleo ya kata na zote zimetumiwa na viongozi hao kwa matumizi yao
binafsi.
Aidha walisema kuwa mara baada ya kusubiri kwa muda
mrefu kuwa watoto wenye mazingira magumu wataenda shuleni lakini haikuwa hivyo
na baada ya kufuatilia wakagundua kuwa mtendaji huyo alienda kuzichukua benki
ya NMB tawi la Geita.
Walifafanua kuwa baada ya kuchukua pesa hizo alizifanyia
matumizi yake binafsi na kukaa kimya bila kutoa taarifa kwa wananchi huku
diwani wa kata hiyo akishirikiana naye.
Viongozi hao walipobanwa zaidi mbele ya mkuu wa wilaya
na mkurugenzi wa halmashauri walikiri kwa pamoja na kupewa muda wa mwezi mmoja
wawe wamerudisha pesa hizo.
Hata hivyo pamoja na kupewa mwezi mzima jambo la kushangaza mwezi umeisha na hawajarudisha
na hawajachukuliwa hatua.
Mtendaji wa kata hiyo Sadik Masalu alikiri kuwepo kwa
tatizo hilo na kusema kuwa ni kweli alizichukua pesa hizo lakini kwa sababu alikuwa
na matatizo ya kifamilia akapeleka watoto wake shuleni.
“Kwa kweli
nilizitumia na hata baada ya kikao kilipokuja cha kunijadili nilikiri na kuomba
wanipe muda wa kuzirudisha mbele ya mkuu wa wilaya na mkurugenzi mtendaji wa
halmashauri ya wilaya”,alisema.
Naye diwani wa kata
hiyo James Maweda alisema yeye hahusiki
na tuhuma hizo isipokuwa mtendaji wa kata ndiyo alizichukua pesa hizo na
kuzitumia kwa matumizi yake binafsi na ameshapewa muda wa mwezi mmoja
azirudishe.
Kwa upande wa mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya
wilaya ya Geita Ali Kidwaka alipoulizwa kuwa ni hatua gani alizozichukua dhidi
ya ubadhilifu huo alisema kuwa taarifa hizo anazo na anazidi kuzifuatilia
kwa kuchunguza zaidi hususani kwa mtumishi wake ambaye ni mtendaji wa kata
Sadik Masalu.
Hata hivyo aliongeza kuwa hatua kali zitachukuliwa
dhidi ya wahusika wa ubadhilifu wa fedha hizo.
Na Valence Robert -Geita.
Social Plugin