Mahakama ya Wilaya ya Mpanda mkoani Katavi imemuhukumu John Joseph
(30) kwenda jela miaka 30 baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka
mwanamke mzee wa miaka 65.
Hukumu hiyo ilitolewa juzi na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya
Wilaya ya Mpanda, Chiganga Ntengwa baada ya kuridhika na ushahidi
uliotolewa mahakamani hapo.
Awali katika kesi hiyo Mwendesha Mashitaka, Godfrey Luzabila alidai
mahakamani hapo kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo Agosti 18 mwaka jana
saa 12 jioni katika Kijiji cha Ifukutwa, Tarafa ya Kabungu wilayani
Mpanda ambako mshitakiwa alikwenda kufanya kibarua cha kutengeneza
barabara.
Alidaiwa kwamba siku ya tukio alimwona mwanamke huyo akipita
barabarani ndipo mshitakiwa alimfuata na kumvutia kichakani pembeni ya
barabara iliyokuwa ikijengwa.
Mwendesha mashitaka huyo aliiambia mahakama kuwa mshitakiwa baada ya
kumvuta kikongwe huyo porini alimlazimisha wafanye ngono kitendo
ambacho mwanamke huyo alikikataa.
Ilielezwa mahakamani hapo kwamba mbakwaji alimsihi mshitakiwa
asifanye hivyo, maombi ambayo hakukubaliana nayo ndipo alipomshika na
kumvua nguo kwa nguvu kisha kuanza kumbaka wakati mwanamke huyo akipiga
kelele za kuomba msaada.
Mwendesha mashitaka alidai mahakamani hapo kwamba kelele za mbakwaji
zilisaidia kupata msaada kutoka kwa watu watatu waliokuwa wakipita eneo
hilo ambao walikwenda na kumwona mshitakiwa akimbaka mwanamke huyo
kabla ya kukimbilia kichakani.
Hakimu Ntengwa akisoma hukumu hiyo alisema kutokana na ushahidi wa
watu watatu uliotolewa na upande wa jamhuri pamoja na taarifa ya
daktari akithibitisha ubakaji uliosababisha sehemu za siri za mwanamke
huyo kuharibika, mahakama imemtia hatiani mshitakiwa huyo na kumhukumu
kwenda jela miaka 30.
Via>>Tanzania Daima
Social Plugin