Mradi wa kufuga nguruwe uliokuwa
ukitekelezwa na Kikundi cha Twaweza, Kata ya Mwendakulima, wilayani
Kahama mkoani Shinyanga umefungwa baada ya fisi kuvamia zizi na kuwatafuna wote.
Akizungumza mjini Kahama juzi, Meneja wa Shirika la
Shdepha Kahama, Venance Mzuka alisema mradi huo ni kati ya mingine
mitano inayotekelezwa kwenye kata hiyo.
Shirika hilo linasimamia vikundi 12 vya uzalishaji kwenye kata hiyo vinavyofadhiliwa na Mgodi wa Dhahabu wa Buzwagi.
Katika kikao cha wadau, Mzuka alisema ufugaji
nguruwe ndiyo ulikuwa na soko la uhakika, lakini sasa umefungwa baada ya
fisi kula mifugo hiyo.
Hata hivyo, Mzuka alisema miradi mingine ya
ufugaji kuku, mbuzi, ng’ombe, kilimo na usindikaji mafuta ya kupakia
unaendelea kwenye vikundi vinane kati ya 12 vilivyopo.
Mzuka alisema Mgodi wa Buzwagi unaomilikiwa na
Kampuni ya African Barrick Gold Mines (ABG), umechangia Sh10 milioni
huku vikundi nane vikipewa Sh6 milioni na zinazosalia zitagawiwa kwa
vinne baada ya kukamilisha usajili.
Hata hivyo, wana kikundi hao walilalamikia ukosefu
wa masoko ya kuuzia bidhaa zao, kwa madai ya kuwapo kwa gharama kubwa
ya uendeshaji ikiwamo ununuzi wa vyakula vya mifugo.
Kufuatia hali hiyo, Ofisa Maendeleo ya Jamii Mji
wa Kahama, Fanuel Reuben alisema ili kumaliza tatizo la masoko inatakiwa
kuwa na kituo rasmi cha kuuzia kitakachokuwa mjini, wateja watawafuata
moja kwa moja walipo na kununua bidhaa zao.
Na Shija Felician-Mwananchi