Geita Bwana!!! MSINGI WA JENGO LA ZAHANATI WACHAKACHULIWA,WAJAZWA MATOPE NA MAWE,WANANCHI WASHTUKIA DILI

Wananchi wa kijiji cha Bugulula katika kata ya Bugulula wilayani Geita wameshtukia ufisadi wa shilingi milioni 36 za kumlipa mkandarasi aliyejenga msingi katika jengo zahanati la Baba, mama na mtoto huku msingi huo ukionekana umejazwa matope na mawe na baada ya kuweka jamvi ukatitia.

Afisa mtendaji wa kata hiyo kishawasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli za maendeleo katika kata yake mbele ya baraza la madiwani mwezi wa kwanza mwaka huu  huku akieleza kuwa kazi imekamilika kwa asilimia mia moja wakati wakati inadaiwa kuwa anatambua kuwa  kuna uchakachuaji kwenye msingi huo.

Imebainika kuwa mkandarasi huyo tangu aanze kujenga msingi huo mwaka jana baada ya kuchimba msingi, udongo alioutoa kwenye msingi aliuweka tena wakati anamwaga jamvi ndipo ikawa chanzo cha kupasuka msingi huo na kutitia huku akionesha udongo uliokuwa umewekwa kinyume na utaratibu wa ujenzi wa majengo.

Inadaiwa kuwa ufisadi huo ambao unadaiwa kuwa kwenye mgororo mrefu kwa baadhi ya viongozi kuanzia ngazi ya kijiji hadi wilayani umeshindwa  kuwawajibisha katika kuhujumu ujenzi huo kwani hata wao wamekuwa ni sehemu ya kulalamikiwa na wanachi hao na hawataki hata kujionyesha mbele ya wananchi ili watoe majibu.

Mmoja wa wananchi hao Philemon Diyunga alisema kuwa.....

"kijiji hiki kina ubadhirifu mwingi  wa mali za wananchi wakati hata diwani wetu ni mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya lakini hatuoni chochote anachosimamia huenda naye anahusika na ufisadi huu sisi tumechoka na tabia za viongozi hawa’’.

Aidha aliongeza kuwa msingi wa jengo hilo ni kielelezo cha ufisadi unaoendekezwa na viongozi hao.

Naye mama mmoja aliyejitambulisha jina laRosemary Francis aliyekutwa katika zahanati hapo alisema ....... 

‘’Tunapata shida sana akina mama wakati wa kujifungua ukipatwa na uchungu inabidi uende geita ukiangalia na umbali uliopo tunapata taabu sana kwanza hakuna vitanda na sehemu yenyewe ni ndogo hivyo tunaomba jengo hili wangelimaliza haraka ili ili tupate huduma kwa karibu’’.

Mwenyekiti wa kijiji hicho Bahati Matati alipotafutwa kujibu tuhuma hizo alisema kuwa ni kweli msingi huo umejengwa lakini baada ya kuumaliza waligundua kuwa umetitia na kumwamru mkandarasi aurudie.

"Hadi sasa hivi tangu tukubaliane naye kuwa mwezi wa tatu tarehe 30 angekuwa amekuja kubomoa na kujenga upya hajaonekana hadi sasa hivi",alisema mwenyekiti huyo.

Hata hivyo kaimu afisa mtendaji wa kijijji hicho Juma Mkingi baada ya kuulizwa uwepo wa msingi wa jengo la Baba mama na mtoto linalojengwa kwa zaidi ya sh milioni 190 huku msingi wake uliogharimu mil 36 ukiwa haujakamilika alisema......

"Ni kweli mwandishi msingi huo uko chini ya kiwango kama ulivyouona lakini ni matatizo madogo madogo tu hayo’’.
Na Valence Robert-Geita

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post