Hofu imezidi kutanda miongoni mwa jamii hasa kundi la vikongwe baada ya vikongwe wanne kuuawa kikatili kwa kukatwa mapanga wilayani Geita,matukio hayo yakihusishwa na imani za kishirikina na migogoro ya urithi wa ng’ombe na mashamba katika kipindi cha wiki moja.
Matukio hayo yametokea siku chache baada ya mkuu wa wilaya,Manzie Mangochie kutoa kauli mwishoni mwa wiki iliyopita ya kuwachukulia hatua za kisheria viongozi wa maeneo yatakapotokea mauaji ya vikongwe.
‘’Tunayo matatizo ya mauaji ya vikongwe,hali hii ni Aibu na hakuna mwenye mamlaka ya kuondoa uhai wa binadamu,kuua mtu wa Mungu?,nendeni kuanzia sasa mkaimarishe ulinzi kwenye maeneo yenu likitokea tukio tutawakamata viongozi wa eneo husika’’alisema dc kwenye kikao cha madiwani.
Kamanda wa polisi mkoani Geita Joseph Konyo,akithibitisha jana(leo) kutokea kwa matukio hayo alisema tukio la kwanza lilitokea Aprili 23,mwaka huu saa 2 usiku katika kijiji cha Katoma baada ya watu wasiojulikana kufika nyumbani kwa Kulwa Kapalata(67)kuomba maji kabla ya kumshambulia kwa kumkata kwa mapanga kikongwe huyo na kusababisha kifo chake.
Aidha Konyo alisema Aprili 27,mwaka huu vikongwe watatu waliuawa kwa nyakati tofauti katika vijiji vya Kagu,Butundwe na Kasamwa wilayani hapa kwa kushambuliwa kwa mapanga na watu wasiojulikana.
Aliwataja Waliouawa kwamba ni,Joyce Dotto(70)mkazi wa Butundwe ambaye aliuawa na watu wasiojulikana akiwa eneo la shule ya msingi Chikobe akiwa njiani kurudi nyumbani akitokea kwenye Klabu ya pombe za kienyeji.
Mwingine ni Yombo Petrol(50)Mkazi wa Kanyala Kasamwa,akiwa nyumbani alivamiwa nyumbani kwake saa 1 usiku na watu watatu waliomshambulia kwa mapanga sehemu za shingoni na mikono na kusababisha kifo chake kisha wauaji walichukua ng’ombe wawili wakaondoka nao.
Hata hivyo ng'ombe hao walikutwa hatua chache kutoka nyumbani kwa kikongwe huyo wakiwa wamekatwa miguu yote na wauaji hao.
Katika tukio la tatu kikongwe mwingine aliyeuawa ni Kabula Yohana(60)mkazi wa kitongoji cha Nchankungu kijiji cha Kagu,ambaye aliuawa kikatili kwa kukatwa mapanga na kundi la watu wasiojulikana idadi yao na mara baada ya kufanya mauaji hayo waliotoweka kusiko julikana.
Katika kipindi cha mwaka jana vikongwe 15 waliuawa kikatili mkoani Geita kwa imani za kishirikina na migogoro ya urithi wa mashamba na mifugo katika wilaya za Geita,Chato na Bukombe.
Kufuatia mauaji hayo baadhi ya vikongwe wanaishi kwa hofu kwenye familia zao kutokana na kutuhumiwa kuhusika katika vifo vya baadhi ya ndugu,majirani na jamaa zao baada ya kwenda kupigiwa ramli kwa waganga wa kienyeji kutaka kujua waliohusika na vifo vya ndugu zao.
via>>geitayetu
Social Plugin