NB-Picha haihusiani na tukio kwenye habari |
Wanafunzi wawili wa darasa la pili katika Shule ya Msingi Goba, Dar es Salaam, wamefariki dunia wakati wakiogelea.
Wanafunzi hao wametajwa kuwa ni Frank Charles (11) na Videson Peter (11), wote wakazi wa Goba.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura, alisema kuwa tukio hilo lilitokea juzi, saa 5 asubuhi wakati wanafunzi hao walipokuwa wakiogelea katika dimbwi la maji ya mvua.
Alisema wanafunzi hao ghafla walizama na kunywa maji mengi na kufariki dunia papo hapo.
Kwa mujibu wa Kamanda Wambura, maiti zote ziliopolewa na wananchi wa eneo hilo na miili yao imehifadhiwa Hospitali ya Mwananyamala.
Wakati huohuo, Askari wa JWTZ kikosi cha Navy Kigamboni, Emmanuel Kamugisha anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka kati ya 20 na 25, amefariki dunia baada ya kugongwa na gari.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Englibert Kiondo, alisema ajali hiyo ilitokea juzi, saa 7 mchana eneo la Mgulani, huko barabara ya Kilwa na kuhusisha gari T 141 CVJ Dong Fen iliyokuwa ikiendeshwa na Athumani Kibuda (48), mkazi wa Morogoro.
Alisema dereva huyo aliyekuwa akitokea Mivinjeni kuelekea Keko, wakati akizunguka mzunguko wa Mgulani, aligongana na pikipiki T 428 CKU aina ya Fekon ikiendeshwa na askari wa JWTZ MT Florian Kamugisha ambaye alikuwa amembeba abiria Emmanuel, wote ni askari JWTZ Navy Kigamboni.
Alisema katika ajali hiyo, Florian alipata majeraha sehemu mbalimbali mwilini na amelazwa hospitali ya Lugalo. Maiti imehifadhiwa hospitalini hapo, na dereva wa gari hilo anashikiliwa na polisi.
Social Plugin