Sunday Mwambelo baada ya kucharangwa mapanga na bosi wake ndani ya bucha eneo la Sae Jijini Mbeya |
Ndugu jamaa na marafiki wa Sunday Mwambelo wakimjulia hali katika hospitali ya rufaa Mbeya alikolazwa baada ya kucharangwa mapanga na bosi wake aliyefahamika kwa jina la Simon Njangaje |
Sunday Mwambelo akijuliwa hali na dada yake Never Mwambinga katika hospitali ya Rufaa Mbeya alikolazwa baada ya kucharangwa mapanga na bosi wake |
WAKAZI wa kitongoji cha Sae Jijini
Mbeya hivi karibuni walimuokoa na kifo mfanyabiashara wa bucha katika
bucha ya Simon Butchery iliyopo Sae Jijini Mbeya, Sunday Mwambelo
ambaye alifungiwa katika bucha na kucharangwa mapanga na watu wawili
waliofahamika kwa majina ya Simon Njangale na Daud Edson.
Hatua hiyo ilifuatia tukio la kutisha
ambalo lilikuwa linaendelea katika moja ya vyumba vya bucha la nyama
ambapo watu watatu walifika eneo hilo majira ya saa 1:00 jioni na
kuufunga mlango wa bucha hiyo kwa nje kisha wakaanza kumcharanga mapanga
muuza nyama huyo.
Ilidaiwa kuwa mara baada ya watu hao
kuingia katika bucha hilo walizima mshumaa ambapo mmoja wao alibaki
mlangoni na wawili kati yao waliingia buchani na kuchukua panga na
shoka kisha kuanza kumuadhibu Sunday ambaye ndiye muuzaji wa nyama
katika bucha hiyo.
Mashuhuda wa tukio hilo walidai kuwa
mmoja kati ya watu hao ndiye mmiliki wa bucha hiyo na kuwa walifikia
hatua hiyo baada ya mfanyakazi wa buchani hapo kuingiza hasara ya
sh.25,000 ambazo ni sehemu ya fedha za mauzo ya siku hiyo.
Kwa mujibu wa Mwambelo ambaye amedumu
katika biashara hiyo kwa zaidi ya miaka 10 ni kwamba mara baada ya
kuulizwa kuhusu hasara ya kiasi hicho cha fedha alimwambia tajiri yake
kuwa atafidia hasara hiyo kesho yake jambo ambalo tajiri wake
hakukubaliana nalo na hivyo kuchukua uamuzi wa kumkata kwa mapanga na
kusababisha damu nyingi kumwagika buchani.
''Ghafla walianza kunikata kata kwa
mapanga, nikaishiwa nguvu nikakaa chini huku damu zikinivuja, wasamaria
wema waliingia kuniokoa,'' alisema Mwambelo kwa taabu kutokana na
maumivu aliyonayo.
Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo
walidai kuwa baada ya kusikia purukushani katika bucha hiyo waliamua
kusogea na kuona dalili za mtu kupigwa ndipo walipoingia na kumuokoa
kijana huyo na baadaye kuwapeleka kituo cha polisi huku majeruhi
akikimbizwa hospitali.
''Wananchi walifika na kumuokoa
Sunday wakaanza kuwapa kipigo wale jamaa, wakawachukua hadi kituo cha
Polisi cha Kati na jamaa wakawekwa ndani,''alisema dada wa majeruhi
Never Mwambinga.
Never alisema kuwa jamaa hao
walidhamiria kumuua nduguyake kwani hatua ya kumcharanga kwa mapanga
huku wakiwa wamezima mshumaa na kufunga mlango ilikuwa inaashiria
dhamira mbaya.
Aidha Jeshi la Polisi kupitia kwa
mmoja wa Ofisa wa ambaye kutokana na taratibu za Jeshi hilo sio msemaji
wa Polisi alisema kuwa watu wawili ambao ni Simon Njangale mmiliki wa
bucha na mtu mmoja Daud Edson wanashikiliwa kufuatia tukio hilo huku
uchunguzi zaidi ukiendelea kwa ajili ya kuwafikisha mahakamani.
Via>> mkwinda blog